JESHI la Polisi Mkoani Tanga limemkamata mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam Simon Tarimo(37) akiwa amebeba mirungi bunda 1,685 ambazo ni sawa na kilogramu 133 ikiwa imehifadhiwa ndani ya mifuko sita ya Salfate kwenye gari la kusafirishia maiti .
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga Blasius Chatanda amesema gari hilo lilikamatwa Januari 12,2021 , saa nane usiku huko kwenye Kijiji cha Manga Kata ya Mkata Tarafa ya Mazingira wilayani Handeni.
Akieleza namna walivyofanikiwa kukamatwa kwa gari na mtuhumiwa huyo, amesema askari waliokuwa doria walilishtukia na walipotaka kulisimamisha dereva akataka kukimbia na wakamkimbiza na kufanikiwa kumkamata na walimuhoji sababu za kukimbia akiwa amesimamishwa na Polisi.
Amesema baada ya hapo askari hao walitaka kulipekua na walipolipekua gari wakakuta kwenye eneo la kuweka maiti wakakuta mafurushi sita yakiwa yamehifadhiwa mirungi ndani yake na ni eneo ambalo wakati wa kwenda lilikaa Jeneza na wakati wanarudi ndipo walipoweka mirungi.
Kamanda huyo amesema katika mahojiano na dereva huyo alisema baada ya kupelekea maiti Makanya Usangi wakati wa kurudi njiani eneo ambalo aliweka maiti akaaamua kuweka mirungi akiamini angeweza kusafiri salama na asipekuliwe kwa sababu anaamini watanzania hawana utamaduni wa kukagua na kupekua magari ambayo yamebeba maiti.
Alilitaja gari la kusafirisha miili ya marehemu ambalo limekamatwa na mirungi hiyo kuwa ni lenye namba za usajili T.569 DSZ aina ya Volvo ambalo ni maalumu kwa kubebea miiili ya marehemu ambalo linamilikiwa na mali ya Nuru Funeral Service iliyopo jijini Dar es Salaam.
Kamanda Chatanda amesema mtuhumiwa huyo alikuwa akisafirisha mirungi hiyo akitokea Usangi kuelekea Dar es Salaam ambapo mbinu iliyotumika ni kuweka mfuko kwenye Jokofu linalotumika kuhifadhia Jeneza lenye maiti wakati wa kusafirisha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...