Na Munir Shemweta, WANMM LINDI
Katika
 kinachoonekana kusogeza huduma za Mabaraza ya Ardhi na Nyumba katika 
wilaya mbalimbali nchini, Serikali imewaelekeza Makatibu Tawala wa mikoa
 kuhakikisha wajumbe Washauri wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba wanateuliwa
 kwa ajili ya kuhudumia wilaya zisizokuwa na Mabaraza ili kuondoa kero 
kwa wananchi  kutembea umbali mrefu kuzifuata huduma hizo.
Hayo 
yameelezwa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt 
Angeline Mabula tarehe 5 Januari 2021 mkoani Lindi wakati akizungunza na
 Watendaji wa Sekta ya Ardhi, uongozi wa mkoa wa Lindi na Wakurugenzi wa
 halmashauri za mkoa huo akiwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa 
sekta ya ardhi na kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serilali kupitia 
kodi ya pango la ardhi. 
Maelezo ya Dkt Mabula yanafuatia 
kuelezwa na Mkuu wa mkoa wa Lindi Godfrey Zambi kuwa mkoa wake una 
Baraza moja la Ardhi na Nyumba linalohudumia wilaya zote tano za mkoa 
huo jambo alilolieleza kuwa limekuwa likileta usumbufu na kero kwa 
wananchi kutembea umbali mrefu.
" Mkoa wetu una Baraza moja tu la
 Ardhi na Nyumba la wilaya linalohudumia wilaya za mkoa huu, fikiria mtu
 anatoka Liwale kuja hapa umbali wa kilometa 250  au Kilwa Kimeta 200 ni
 kumuumiza mwananchi" Alisema Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi. 
Kwa
 sasa kuna jumla ya Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya 57 yanayotoa 
huduma nchini wakati sheria inataka kuwa na Mabaraza 139 jambo 
linalosababisha baadhi ya wilaya kukosa huduma za Mabaraza na kuwafanya 
wananchi kuzifuata  huduma kwa kutembea umbali mrefu.
Dkt Mabula 
alisema, baada ya Serikali kuona wananchi wanapata shida ya kuzipata 
huduma za Mabaraza ya ardhi sasa imeamua kuwaelekeza Makatibu Tawala wa 
Mikoa kuteua  wajumbe Washauri wa Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na 
Nyumba la wilaya sambamba na  Wakurugenzi wa Halmashauri kutakiwa 
kutenga ofisi itakayoendesha Mashauri na kuwa na Watumishi kama Makarani
 ili kuwawezesha Wenyeviti kufanya kazi  kulingana na mahitaji ya wilaya
 husika. 
"Pamoja na kuwa na Mabaraza ya Ardhi katika wilaya 
mbalimbali lakini tumeona bado kuna 'gape' mahali hasa zile wilaya 
ambazo hazina Mabaraza ya Wilaya, maana Baraza la wilaya moja 
linahudunia wilaya tatu kwa hiyo bado hatujatatua tatizo la wananchi 
kusafiri umbali mrefu ili kusogeza huduma kwa wananchi wanaoteseka" 
Alisema Dkt Mabula.
Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya kwa 
mujibu wa sheria Na 2 ya mwaka 2002 lina wajumbe wasiozidi saba na 
watatu kati yao ni wanawake na kuteuliwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na 
Maendeleo ya Makazi kutokana na Mapendekezo ya Mkuu wa Mkoa kutoka 
katika eneo la wilaya husika. 
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula 
akizungumza katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Lindi tarehe 5 Januari 2021 
wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya Ardhi na 
uhamasishaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi. 
Kushoto ni Mkuu wa mkoa wa Lindi Godfrey Zambi na kulia ni Afisa Tawala 
wa Wizara ya Ardhi Baraka Mraha.   



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...