Na Shukrani Kawogo, Njombe.
Wazazi wilayani Ludewa mkoani Njombe wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kutimiza ndoto za watoto wao badala ya kuwashawishi watoto hao kufanya vibaya katika mitihani yao ya kuhitimu elimu ya msingi na sekondari ili waweze kuwasaidia shughuli zao za nyumbani na mashambani.
Hayo ameyasema katibu wa mbunge wa jimbo la Ludewa Alphonce Mwapinga alipomuwakilisha mbunge wa jimbo hilo Joseph Kamonga katika hafla ya kuwakaribisha kidato cha kwanza katika shule ya Nicopolis Academy na Andrea Tsere Open School iliyopo wilayani humo.
Amesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwaambia watoto kuwa wasifanye vizuri katika mitihani yao ya mwisho kwa kukwepa majukumu yao ya kuwaendeleza kitu ambacho kinarudisha nyuma maendeleo ya elimu wilayani humo.
“Hawa watoto wanapaswa kujenga misingi ya maisha yao ya baadae, hivyo mzazi unapomzuia mtoto asifanye vizuri kwenye mitihani yake unakuwa humtendei haki na unamzuia kutimiza malengo yake, hivyo kila mzazi atambue kuwa watoto wana haki ya kupata elimu na mweye jukumu la kwanza la kuhakikisha mtoto huyo anapata elimu hiyo ni mzazi ”, Alisema Mwapinga.
Naye mkurugenzi wa shule ya Nicopolis Academy Augustino Mwinuka amesema kwa kushirikiana na Andrea Tsere open school wamekuwa wakipokea wanafunzi ambao waliishia njiani katika masomo yao na wanahitaji kujiendeleza ambapo walianza na wafunzi kumi na nne na sasa wanafunzi walioanza kuwapokea wamefikia 150 huku bado wakiendelea kupokea wanafunzi wengine.
Amesema kumekuwa na muitikio mkubwa kwa wanfaunzi kutoka maeneo mbalimbali nje ya Ludewa hivyo amewataka wanaludewa kutumia fursa hii ya kuwapa elimu watoto wao kwakuwa shule binafsi zilizopo katika wilaya hiyo ni chache ukilinganisha na uhitaji wa wanafunzi.
Aliongeza kuwa shule yake imejipanga vyema katika kutoa elimu bora kwani imelenga kutoa msaada wa kuwapa elimu bure wanafunzi wasio jiweza na waishio katika mazingira magumu ambapo watoto hao watasoma bure bila kulipia gharama yoyote huku kwa wale wanaojiweza watalipia ada kidogo ili kuweza kuendesha shule hiyo.
“Shule hii tayari imejipanga kutoa elimu kuanzia chekechea mpaka kidato cha nne pia kuna mkakati wa kuanzisha chuo cha ufundi hivyo tunaamini tutaweza kuwasaidia wanafunzi katika ngazi zote na kuwafanya waweze kutimiza malengo yao kielimu”, Alisema Mwinuka.
Aidha kwa upande wa mmoja wa wanafunzi hao Daniel Komba amesema wamekuwa wakifundishwa vyema na walimu wao japo wanakabiliwa na changamoto ya vifaa vya michezo hivyo wanaiomba serikali kupitia mbunge wao Joseph Kamonga kuwasaidia vifaa hivyo vikiwemo mipara na jezi.
Mkurugenzi wa shule ya Nicopolis Academy Augustino Mwinuka akiongea na wazazi pamoja na wanafunzi (hawapo pichani) katika hafla ya kuwakaribisha wanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule hiyo.
Katibu wa mbunge wa jimbo la Ludewa Alphonce Mwapinga akiongea na wazazi na wanafunzi wa shule ya Nicopolis Academy na Andrea Tsere Open School wakati wa sherehe ya kuwakaribusha wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza katika shule hiyo.
Wanafunzi wa kidato cha kwanza, wakiwa wamesimama kuwasalimia wageni waalikwa katika hafla ya kuwakaribisha wanafunzi hao.
Wanafunzi wa Nicopolis Academy na Andrea Tsere open school wakisoma risala yao mbele mgeni rasmi katika hafla ya kuwakaribisha wanafunzi wa kidato cha kwanza iliyofanyika shuleni hapo. Kutoka kushoto ni Eliza Haule na Oliver Godwin.
Mwenyekiti wa bodi ya shule ya Nicopolis Academy Nickson Mahundi (Aliyesimama) akizungumza na wazazi pamoja na wanafunzi (hawapo pichani) katika hafla ya kuwakaribisha wanafunzi wa kidato cha kwanza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...