Said Mwishehe, Michuzi TV
TAMASHA la muziki wa Hip Hop asili linatarajiwa
kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 25 hadi Juni 27 mwaka huu ikiwa ni
mkakati wa kuibua wasanii wasiosikia katika muziki huo.
Katika kuelekea tamasha hilo waandaaji wa tamasha
hilo wamesema kutakuwa na ratiba ya kwenda mikoani kusaka vipaji vya wasanii wa
muziki huo na baada ya hapo watakuja kushiriki kwenye tamasha kubwa ambalo
litafanyika katika tarehe hizo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo Februari 1,2021 katika Kituo cha Udamaduni
cha Alliance de France, Mwanamuziki wa muziki wa Hip Hop Farid Kubanda a.k.a Fid
Q amesema tamasha hilo litafanyika chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Ufaransa
nchini Tanzania kwa kushirikiana na wadau wengine wa muziki huo wakiwemo Art
Space ambao wametoa eneo ambalo tamasha hilo litafanyika.
"Tumekutana hapa leo kuzungumzia tamasha
ambalo liko mbele yetu, tunatarajia kulifanya Juni mwaka huu na kabla ya hapo
kutakuwa na shughuli ndogo ndogo ambazo zitaendelea na miongoni mwa shughuli
hizo ni kwenda mikoani kusaka vipaji vya muziki wa hip hop asili.
"Hivyo Februari 5 mwaka huu tutakuwa Mjini
Dodoma pale katika Klabu ya T Squre
ambayo ina hadhi, ina steji nzuri ambapo wasanii watakuwa huru kuonesha vipaji
vyao. Baada ya hapo tutakwenda Zanzibar.
"Ni matumaini yetu kupitia tamasha hilo
tunakwenda kuibua vipaji vya muziki huo ambavyo havijapata nafasi ya
kusikika.Tunawashukuru Ubalozi wa Ufaransa kwa kutusaidia katika hili na
tunatamani kuona tunalifanya kila mwaka kama wataendelea
kutufadhili,"amesema Fid Q.
Amefafanua baada ya kufanya Dodoma na Zanzibar pia
watatoa ratiba ya mikoa mingine ambayo watakwenda kuibua vipaji ambavyo mwisho
wa siku vitakutanishwa katika Jiji la Dar es Salaam kuanzia hiyo Juni 25 hadi
Juni 27 mwaka huu ambapo itakuwa siku ya Ijumaa, Jumamosi na Jumapili.
Fid Q ameongeza kupitia tamasha hilo mbali ya
kuibua vipaji, litakwenda kuutangaza zaidi muziki hu na kwamba Hip Hop ni
maisha ya kila siku ya mwanadamu, hivyo katika muziki huo kuna kitu zaidi ya
kimoja ambacho msanii anakifanya.
"Wakati tunaelekea katika tamasha hilo
tutakuwa na matukio mengi, tutawajengea uwezo wasanii ambao watapatikana,
tutawapa mafundisho ya kuutumia muziki huo katika fikra chanya zaidi kuliko
kuwaza fikra hasi,"amesema na kuongeza tamasha hilo mbali ya kuwa na
wasanii wa Tanzania litahusisha na wasanii kutoka mataifa mengine ili kuongeza
ladha ya burudani.
Kuhusu kiingilio amesema watavitangaza lakini kwa
wale ambao watakata tiketi ya siku zote tatu kwa wakati mmoja kutakuwa na
punguzo ukilinganisha na yule ambaye atakata tiketi ya siku moja moja ambayo
itakuwa juu kidogo.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara Ushirikiano na
Utamaduni kutoka Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania Cecile Frobert ameeleza
wazi Ubalozi wa Ufaransa umekuwa na mkakati wa kuhakikisha wasanii wanapata
nafasi ya kuonesha vipaji vyao, hivyo wameamua kusaidia kufanikisha tamasha
hilo la kuibua vipaji vya Hip hop asili.
Amesema ni tamasha kubwa ambalo litakuwakutanisha
wasanii kutoka mataifa megine yakiwemo ya Kenya na Uganda , hivyo amesisitiza
wataendelea kusaidia katika kuhakikisha wasanii wanasaidia katika kufanya kazi
yao ya sanaa huku akiweka wazi katika tamasha hilo ni matarajio yao kuona kuna
ushiriki wa wasanii wa kike.
Kuhusu tamasha hilo iwapo watakuwa wakilifadhili
kila mwaka, amesema ni mapema kwa sasa kutoa majibu lakini ni matumaini yao
huko mbele ya safari watajua ni jinsi gani wanaweza kusaidia kwani wamekuwa
wakifanya hivyo mara kwa mara kufanikisha matamsha mbalimbali ya wasanii wa
aina tofauti tofauti.
Wakati huo huo Mussa Sango ambaye ni moja ya
washiriki katika kuandaa tamasha hilo, amesema wanayo redio ambayo imekuwa
ikisaidia kuibua vipaji vya wasanii, hivyo kupitia tamasha hilo watakuwa na
jukumu la kusaidiana na Fid Q na wadau wengine kusaka vipaji vipya vya muziki
huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...