Na Mwandishi Maalum (ORCI) – Dar es Salaam
BENKI ya Azania imeamua kuwapa fursa wafanyakazi wake kufanyiwa uchunguzi wa homa ya ini na wataalamu mabingwa wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), kuelekea kilele cha Siku ya saratani Duniani ambayo huadhimishwa Februari 4, kila mwaka.
Wafanyakazi wasiokutwa na maambukizi ya homa hiyo wanapatiwa chanjo ya Hepatitis B ili kuwakinga dhidi ya maambukizi hayo, imeelezwa.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa ORCI, Dk. Crispin kahesa amesema watatoa huduma hiyo kwa wafanyakazi wa benki hiyo iliyosambaa zaidi ya mikoa 11 ikiwa na matawi zaidi ya 25.
“Lengo ni kuwapa chanjo wafanyakazi 550 na zoezi hili limeanza leo,” amebainisha.
Amebainisha mikoa watakayoifikia na kuwapa huduma hiyo wafanyakazi wa benki hiyo ni Dar es salaam, Dodoma, Morogoro, Arusha, Moshi, Mbeya,Tunduma, Geita, Simiyu, Mwanza na Shinyanga.
“Tunazidi kuhamasisha jamii kushiriki na kujitokeza kufanya upimaji na kupokea huduma za kujikinga dhidi ya Saratani,” ametoa rai.
Dk. Kahesa amesema Ocean Road imekuwa ikitoa huduma katika jamii kupitia kampeni kwa wananchi, maeneo ya mahali pa kazi na vyuoni.
“Huduma hii inapatikana katika taasisi yetu hapa Dar es Salaam, lakini pia tuna utaratibu maalum na rafiki kuweza kuwafikia wananchi popote walipo mahala pa kazi, vyuoni na kwengineko.
“Hivyo, kwa wale wanaohitaji tuwafikie popote walipo wasisite kuwasiliana nasi kwa utaratibu maalum kwa kuwalisiliana nasi,” amesisitiza.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...