Na: Moshy Kiyungi,Tabora

Februari, 2021.

 Imetimia miaka mitano tangu afariki dunia Kassim Mapili tarehe kama ya leo  02Februari 02, 2016 jijini Dar es Salaam kwa maradhi ya shinikizo la damu akiwa nyumbani kwake maeneo ya Tabata jijini Dar es Salaam.

Baada ya kutoka kuangalia mtanange kwenye luninga baina ya timu za Arsenal na Barcelona, nguli alipoingia chumbani mwake hakutoka tena majirani zake wakalazimika kutoa taarifa polisi ambao waliofika na kuvunja mlango wa chumba chake, wakabaini kuwa ameshafariki dunia.

Mwili wa marhemu Mapili ulikutwa ukiwa na taulo kiunoni ambayo ni ishara kuwa aidha alikuwa anakwenda au ametoka kuoga.

Siku zake za mwishoni kabla ya kifo chake Kassim Mapili alilazwa kwa miezi kadhaa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili kutokana na kuwa na tatizo la moyo.

Mkongwe huyo wakati akiwa katika maumivu aliwahi kutamka kuwa wakati akiwa anaumwa alisaidiwa na Salma Moshi, msanii mkongwe anayeishi nchini Marekani ambaye alimkatia Bima ya Afya, hali yake iliimarika.

Kassim Mapili alikuwa na vipaji vingi vya kutunga, kuimba nyimbo za muziki wa dansi na kupiga gitaa, alianza tasnia hiyo kabla ya nchi yetu ya Tanganyika haijapata Uhuru.

Licha ya umri wake kumtupa mkono nguli huyo wakati wote alionekana mwenye nguvu, mtanashati, mcheshi wenye kujipenda wala  hakuwa na dalili za ‘kuchoka’ kama walivyo Wazee wengine wenye umri kama wake.

Wasifu.

Enzi za uhai wake Kassim Mapili aliwahi kuzungumza na gazeti hili alisema kwamba  alizaliwa katika kijiji cha Lipuyu kilichopo tarafa ya Lionya, Wilaya Nachingwea mkoani Lindi mwaka 1937.

Alipata elimu ya msingi na  ya Kiislam kwenye madrasa ambako alikuwa mahiri wa kughani Kaswida, hata mapenzi ya kuimba yalianzia kwenye madrasa hiyo  kijijini kwake Lipuyu mkoani humo.

Jina lake lilianza kusikika katika ulimwengu wa muziki mara baada ya kujiunga katika bendi ya White Jazz iliyokuwepo mjini Lindi mwaka 1958, ambapo sifa zake za kupiga muziki zilizagaa sehemu mbalimbali hadi mikoa ya jirani, mwaka uliofuatia wa 1959  akaenda kujiunga na bendi ya Mtwara Jazz.

Kassim Mapili alikuwa akiwindwa na bendi nyingi kufuatia weledi wake katika muziki, bendi ya Holulu ya mjini humo ikamshawishi kwa ahadi ya kumpatia maslahi manono, hakufanya ajizi kujiunga na bendi hiyo mwaka 1962.

Nchi yetu ya Tanganyika wakati huo  ilikuwa tayari imepata Uhuru Chama TANU kiliazisha vikundi vya Vijana kukitangaza ambapo Mapili akaoneka anafaa kusaidia kufanya kazi hiyo, mwaka 1963 akachukuliwa kwenda katika bendi ya Jamhuri Jazz iliyokuwa ya vijana wa TANU (TANU Youth League) ya mjini Lindi.

Baada ya kufanya kazi nzuri akateuliwa kuwa mwasisi wa bendi nyingine kama hiyo mjini Tunduru mkoani Ruvuma mwaka 1964.

Maslahi alilazimika kwenda kujiunga na bendi ya Luck Star iliyokuwa na makazi yake Kilwa Masoko mkoani Lindi, alikoahidiwa kulipwa ‘kitita kinene’ cha  pesa mwaka 1965, hata hivyo hakudumu kwa kipindi kirefu katika bendi hiyo alichukuliwa mwaka huohuo kwenda kujiunga na bendi ya Kilwa Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Ahmed Kipande.

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) lilianzisha bendi mbili za muziki wa dansi za JKT  ‘Kimbunga Stereo’ na JKT  ‘Kimulimuli’ mwaka 1965 lilimchukuwa kwenda kuwa muasisi wa bendi ya JKT Kimbunga Stereo iliyokuwa na makazi kwenye kambi ya Mgulani jijini Dar es Salaam

Desemba 15, 1965 Jeshi la Polisi lilimpa ajira akawa mwasisi wa bendi ya Polisi Jazz  ‘Wana Vanga Vanga’ iliyokuwa ikipiga muziki wake katika ukumbi wa Polisi Barracks, jijini Dar es Salaam.

Afande Kassim Mapili talanta zake katika muziki zifanya Desemba 23, 1965 kuteuliwa kuwa mwalimu wa bendi ya  Wanawake iliyojulikana kama Woman Jazz Band, ikimilikiwa na Umoja wa Vijana TANU (TANU Youth League) aliyosafiri nayo kwenda nchini Kenya kwenye sherehe za siku ya Kenyata (Kenyata Day).
Jomo Kenyeta alikuwa rais wa kwanza wa nchi hiyo, hivi sasa mwanawe Uhuru Kenyata ndiye rais wa nchi hiyo.

Woman Jazz ilisambaratika mwaka 1974 ndiyo ikwa chanzo cha kuanzishwa kwa bendi ya Vijana Jazz,  baada ya kukusanya vijana wa wakati huo akina Hemed Maneti,  Hassan Dalali, Manitu Mussa, Hamza Kalala ‘Komandoo’ Chakupele, Abdallah Kwesa , Agrey Ndumbaro na wengine wengi.

Aidha Kassim Mapili aliteuliwa kuwa mlezi wa bendi ya Super Matimila mwaka 1974 pia aliteuliwa kuwa mkufunzi wa bendi ya Gold All iStars mwaka 1977.

Aidhaalishiriki kikamilifu katika uundwaji upya wa bendi ya Super Volcano, akiwa na Taji binti ya Mbaraka Mwinshehe.

Kassim Mapili alistaafu toka jeshi la Polisi  Mei 05, 1981 akiwa na cheo cha Sajenti  mwaka huohuo akaenda kujiunga na bendi ya Tanzania Stars Ushirika Jazz, waliokuwa wakiporomosha muziki wao kwa mtindo wa ‘Watunjatanjata’

Wakati wa uhai wake nguli huyo alikuwa  akiitwa kuhudhuria makongamano mengi likiwemo la Wanamuziki iliyofanyika mjini Bagamoyo mwaka 1982, ambalo liliyofikia uamuzi wa kuundwa kwa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA) ambapo Kassim Mapili alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho.

Kila palipokuwa pakifanyika jambo la jema kwa manufaa ya muziki hapa nchini, Mapili alishiriki kikamilifu kutoa michango wake wa mawazo ya katika tasnia ya muziki akipambania haki za wanamuziki wenziwe.

Mwaka 1986 alichaguliwa kuwa mmoja wa washiriki katika uundwaji wa kundi la wanamuziki 57 lililoitwa Tanzania All Stars, pia mwaka huohuo alishiriki katika tamasha la utoaji  wa zawadi kwa Wasanii wakongwe, akiwemo Mzee Morris Nyunyusa, Mzee Makongoro, Mzee Salehe Mwinamila, Mbaraka Mwinshehe na wengine.

Kassim Mapili mwaka 1988 alikuwa mwasisi katika shindano la nyimbo kumi bora za wanamuziki wa dansi (Top Ten Show) akiwa kama Mwenyekiti wa CHAMUDATA.

Mwaka 1993 alikuwa mstari wa mbele wa uanzishwaji wa bendi ya Wazee ya Shikamoo Jazz, ambayo hadi sasa bado ipo inaongozwa na mzee Salimu Zahoro.

Mapili alikuwa na sifa ambayo baadhi ya wanamuziki wengine hawana ambaye ambaye katika hakuwahi kunywa pombe wala sigara katika maisha yake yote, bali alijali zaidi kula chakula vizuri na  kufanya mazoezi ya viungo kila siku.

Wakati wa uhai wake alisema kuwa yeye hakuwa mtu tegemezi kwa watoto wake kwakuwa alifanikiwa kumiliki bendi ya Orchestra Mapili Jazz iliyomuongezea kipato zaidi.

“Bendi yangu huwa inawasisimua mno wapenzi wa muziki wa zamani kwa kuwapigia nyimbo za zamani kwa maombi yao maalum…”  alitamka Mapili.

Kassim alijigamba kwamba wakati akipiga gitaa huimba  kufanya ‘shoo’ mwenyewe  akiwakumbusha wazee wenzake mitindo yao ya  zamani ya Twist, Chacha, Pachanga na Bumping.

“Ninauheshimu sana muziki kwani ndiyo ulionilea hadi sasa,  nimekulia na kuzeeka nikiwa katika muziki, sijawahi kufanya kazi nyigine tofauti na muziki katika maisha yangu yote, hata nilipopata ajira katika Jeshi la Polisi, nilikuwa nafanya kazi ya muziki…” abainisha hayo Mapili.

Sifa nyingine za mkongwe huyo alikuwa mstari wa mbele katika shughuli takriban zote za kifamiliya za wasanii na wanamuziki wenzake hapa nchini, hakubagua kama ni Mtanzania ama raia wa nchi nyingine.

Aliwasihi vijana kujifunza kupiga ala za muziki ili wafikie malengo yao ya kuwa wanamuziki watakao kubalika kimataifa.

Kassim Mapili alifariki dunia akiwa ametimiza miaka 79, ameacha mjane na watoto watatu Kuruthum, Said na Hassan kati yao hakuna hata mmoja aliyefuata nyao zake katika muziki.

Mungu aipumzishe roho yake pahala pema peponi, Amina.

Mwisho.

Mwandishi wa makal hii anapatikana kwa namba 0713331200, 0784331200, 0736331200 na 076733120

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...