Na: Moshy Kiyungi,Tabora.
Januari, 2021.
Kikumbi Mwanza Mpango King Kiki haonekani jukwaani kutumbuiza muziki kwakuwa anasumbuliwa na maradhi ya Uti wa mgongo kwa kipindi kirefu sasa.
Hali ya mkongwe huyo siyo njema kabisa hawezi kusimama wala kufanya chochote bila ya kupatiwa msaada, anatumia kiti cha kusukuma cha wagonjwa Wheel Chair, itakuwa jambo la kiungwana kwa wapenzi na wadau wa muziki kwenda kumfariji hata kumuwezesha kuzikabili changamoto za matibabu.
Ikumbukwe kwamba Benno Villa Anthony mtunzi na mwanamuziki wa bendi ya DDC Mlimani Park alitunga wimbo wa Nani kaiona kesho, ukikemea watu kutoa misaada wakati wa msiba badala ya kujadili gharama za matibabu akiwa mgonjwa, akifariki huja na magari ya kifahari na Kamera za video mazishini!
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli aliguswa na hali yake alimpigia simu akamuombea kwa mungu amponye haraka maradhi yanayomsibu nguli huyo.
Aidha Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa alikwenda kumjulia hali nyumbani kwake Mtoni kwa Azizi Ali jijini Dar es Salaam, akamuahidi kuwa serikali itamsaidia kuweza kumudu gharama za matibabu.
Namshukuru rais wetu Dk. John Magufuli alinipigia simu akaniombea kwa mungu nipone haraka, hata Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alifika hapa nyumbani kunijulia hali na kunipa ahadi kuwa serikali itanisaidia…alisema Kiki.
Kikumbi Mwanza Mpango Januari 01, 2021 alitimiza miaka 74 ya kuzaliwa kwake ambaye katika maisha yake hajafanya kazi nyingine tofauti na muziki, uliomjengea umaarufu kwa wapenzi wa muziki wa dansi kila kona ndani na nje ya nchi kufuati utunzi na uimbaji wa nyimbo zenye jumbe mahsusi kwa jamii.
Kiki amefanya mambo mengi katika tasnia ya muziki wa dansi likiwemo la kuendeleza vipaji vya vijana kupitia weledi wake, tangu alipoingi nchini kwa mara ya kwanza miaka ya 1970 akiwa na bendi ya Orchestra Fouvette toka nchini Zaire wakati huo.
Wanamuziki wa bendi hiyo baada ya kufanya mambo makubwa ya burudani nchini, walirudi kwao ambako walibadilisha jina ikawa Safari Nkoi.
Mkongwe huyu miaka michache iliyopita alifanya mahojiano maalumu na mwandishi wa makala haya akayataja majina yake kuwa ni Kikumbi Mwanza Mpango, alizaliwa Januari 01, 1947 katika mji wa Lubumbashi uliopo mkoa Katanga nchini Kongo Belgium ambayo sasa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
“Mimi ni mtoto wa tano kwa kuzaliwa toka kwa wazazi wangu Katambo Wabando Paulino na mama yangu ni Mwanza Jumban
Kwa upande wa elimu King Kiki alianza masomo ya awali mwaka 1953 akiwa na umri wa miaka sita mjini Lubumbashi, baadaye baba yake akahamia katika mji wa Likwasi ambako aliendelea na elimu hiyo katika shule ya Officialle Laique de Kolwezi.
Kikumbu alibuni njia za kujiendeleza kimuziki akawa anachukua ujuzi wa kucheza mitaani, akaupeleka shuleni ambako aliwatafuta wenzake watatu wakaanzisha kikundi cha muziki wa dansi wote wakiwa darasa la tano, wakiimba na kucheza hata walimu wao waliupenda muziki huo kila sherehe za shule waliitwa kutoa burudani.
Sifa za umahiri wao zikazagaa maeneo mengi ikizingatiwa kwamba walikuwa vijana wadogo wakifanya mambo makubwa.
“Hata wazazi wa wanafunzi waliokuwa jirani na shule yetu wakiwa na sherehe zao majumbani walitualika kwenda kuimba na kucheza bure…” alitamka King Kiki.
Mbali na kupenda muziki Kiki alikuwa kichwa darasani, hakuwahi kuwa mtu wa tatu kila anapofanya mtihani akifeli sana alishika nafasi ya pili.
Alikumbuka wakati akiwa na umri wa miaka sita akisoma shule ya awali mwaka 1952, kundi la muziki kutoka nchini Afrika Kusini likiambatana na mwanamuziki Miriam Makeba ‘Mama Afrika’, lilifanya ziara nchini mwao.
“Kaka yangu Koroumba Joseph alikuwa akinipenda sana, hivyo muda mwingi nilikuwa nikiongozana naye kwenye dansi, hasa mwishoni mwa wiki, hata kwenye onesho la Miriam Makeba alinipeleka...” alisema King Kiki.
Miriam Makeba alikuwa akiongoza safu ya uimbaji ambao waliimba na kucheza kama vile hawana mifupa kwenye miguu na mwili kwa ujumla.
King Kiki alinogewa vilivyo na uimbaji wa Makeba ambaye kumbukumbu zake hazikumtoka kichwani mwake, akaahidi kufuata nyayo zake.
“Kwa kweli nimezunguka nchi nyingi kufanya muziki, nimeona shoo nyingi za Kimataifa hakuna aliyewahi kuvunja rekodi ya kile nilichokiona siku hiyo kwa Miriam Makeba...” alisisitiza King Kiki.
Akiwa bado masomoni mwaka 1958 alifanikiwa kuanzisha kikundi cha muziki alichokiita Bantu Negro kilichokuwa kinapiga muziki wa Afrika ya Kusini, kikaweza kubadili muziki huo kwenda kwenye muziki wa rhumba.
Kikumbi alijiunga kidato cha kwanza katika sekondari ya Attene Iwayala ambako alipendekezwa kufanya fani mbalimbali zikiwemo za maigizo, ngoma, kuimba na kucheza.
Muziki ulikuwa umemtawala mno hivyo mwaka 1962 ilimlazimu kuacha shule akiwa Sekondari kidato cha tatu, akaenda kujiunga na bendi ya Norvella Jazz, ambako aliikuta ikiwa vyombo vya muziki vichakavu, wakalazimika kutafuta vyombo vingine vizuri vya muziki, hivyo wakapita katika vikundi mbalimbali vya muziki hadi mkoa wa Kasai (Mbudji Mai), walikutana na vikundi kutoka mkoa wa Kinshasha vya African Jazz, Conga Success, Negro Succes, Eco Bantu, African Fiesta vita vilivyomfanya kupata uzoefu zaidi katika muziki wa rhumba mwaka 1965.
Kiki wakati akifanya muziki alikumbana na kizingiti toka kwa wazazi wake ambao hawakupenda awe mwanamuziki, wao walitaka aendelee na masomo akawa akichapwa ili aende shule lakini hakubadili msimamo wake.
“hata kaka yangu alikuwa akinifunga kamba nyuma ya baiskeli huku niburuzwa umbali wa mrefu kama adhabu ya kutokwenda shule, lakini yote hayo haikusaidia…” alitamka Kiki huku akitabasamu.
Alisema ukali wa kaka na wazazi wake alilazimika kutoroka nyumbani kwao akaenda kujihifadhi kwa marafiki zake, baadaye wazazi wake walimuita kumuuliza iwapo anatakuwa tayari kufanya kazi nyingine tofauti na muziki, Kiki alijibu kwamba muziki umemteka sana na kwamba atakufa nao.
Majibu hayo yalifanya baba yake kukubaliana na matakwa yake akamtakia mafanikio mema.
“Baba aliposema hivyo nilirukaruka kwa furaha, nikajihisi kama nilikuwa naelea katika dunia ya wapenda muziki…” anasema Kiki.
Ili kuwathibitishia wazazi wake kuwa muziki unalipa, alipeleka kiasi cha pesa alizovuna kutokana na kazi hiyo.
“Nilipiga muziki kwa kipindi cha miezi mitatu mfululizo, baadhi ya pesa nilizopata nilimpelekea baba yangu kumdhihirishia kuwa muziki unanilipa…” Kiki alitamka.
Hata hivyo mzazi wake pamoja na kuzipokea pesa hizo, bado alikuwa akimshauri kwamba anayo nafasi ya kurudi shule kuendelea na masomo.
Kauli hizo za wazee wake akaona bora awe mbali na nyumbani hivyo mwaka 1964, akaenda mkoa wa Kasai ambako alijiunga na bendi ya Norvella Jazz alikopiga muziki hadi mwaka 1967 ilikasambaratika.
Mwaka 1968 Kiki alirudi mkoa wa Katanga ambako alikutana na Fred Ndala Kasheba aliyemkaribisha kujiunga katika bendi ya Orchestra Fouvette ambako alianza kuimba nyimbo mbili zilizotamba sana za Jacqueline na Kamarade ya Nzela, zilizompa nafasi ya kufuatana na bendi ya Orchestra Fouvette kuja nchini Tanzania.
Baada ya kufanikiwa kuzikonga nyoyo za wapenzi na mashabiki wa muziki wa dansi katika maonesho yao kadhaa, walirejea nchini kwao ambako walibadili jina la bendi, ikaitwa Safari Nkoi.
Mwaka 1977 Kikumbi Mwanza Mpango akiwa nchini mwake alifuatwa na Chibangu Katayi ‘Mzee Paul’, ili aje Tanzania kujiunga katika bendi ya Maquis du Zaire, iliyokuwa na tayari ipo katika jiji la Dar es Salaam.
Kabla ya kuondoka huko aliwapendekeza baadhi ya wanamuziki kuja nao kuimarisha bendi ya Maquis du Zaire akina Nkashama Kanku Kelly, Mutombo Sozy na Ilunga Banza ‘Mchafu’.
Wakiwa safarini walipitia mji wa Kamina ambako walimpata Ngalula Tshiandanda aliyekuwa dada mnenguaji katika bendi ya Sakayonsa ya mjini humo.
Baada ya kutua katika bendi hiyo Kiki alianza kuonesha cheche zake akabuni mtindo wa Kamanyola uliokuja kuwa ukawa gumzo hususan katika jiji la Dar es Salaam na viunga vyake, ukachukua nafasi ya mtindo wa Chakula Kapombe uliotumiwa awali.
Alieleza maana halisi ya Kamanyola akisema ni mji ulioko nchini mwao Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
“Nilitunga mtindo huo baada ya kujiunga na bendi hiyo mwaka 1977, ambao niliongeza kionjo cha ya ‘bila jasho’ kwakuwa mtu atacheza muziki huo taratibu kwa raha zake huku akijidai…” Kiki alifafanua.
Umahiri wa kutunga na kuimba Kiki aliedelea kuachia vibao vingine vya ‘Nimepigwa Ngwala’, Kiongo na ‘Kyembe’, Kibwe Mutondo na Sofia.
Zingine ni Mokili, Yoka Mateya Babote, Dora mtoto wa Dodoma, Sababu ya Nini, Usinifiche siri na Noele Krismas.
Kiki alishirikiana vyema na watunzi na waimbaji akina Mbuya Makonga ‘Adios’, Mutombo Lufungula ‘Audax’, Mukumbule Lolembo ‘Parashi’, Abubakar Kasongo Mpinda ‘Clyton’, Mbombo wa Mbomboka, Tshimanga Kalala Assosa, Kiniki Kieto, na Masiya Radi ‘Dikuba Kuba’ ikikamilishwa na Issa Nundu na Tabia Mwanjelwa.
Kikumbi Mwanza baada ya miaka miwili alikwenda kujiunga na bendi ya Orchestra Safari Soud (OSS), iliyokuwa na makao yake katika Kimara Resort huko Kimara, jijini Dar es Salaam, ambako alishirikiana na waimbaji wa bendi hiyo akina Skassy Kasambula, Monga Stani Liki, Mobali Jumbe, Kalala Mbwebwe, Tshibanda Sony na Kabeya Badu.
Kiki alionesha umahiri wake kwa kutunga na kuimba nyimbo pamoja na kutambulisha mtindo mpya wa ‘Masantula Ngoma ya Mpwita’. Nyimbo hizo ni za Mimi Msafiri, Mama Kabibi na nyingine nyingi
Nguli huyo alijikomboa baada ya kuanzisha bendi yake ya King Kiki Double O, iliyokuwa ikitumia mtindo wa ‘Embalasasa’ iliyoachia vibao vya Kitoto chaanza tambaa, Njigina, Salamule, Mtoto wa Elia, Sababu ya Nini, Malalamiko na nyingine.
Uchakavu wa vyombo viliponza bendi hiyo hadi kusambaratika baada ya muda mfupi, Kiki alianza kufanya muziki wa kujitegemea wakati mwingine akipita katika bendi mbalimbali ikiwemo ya Orchestra Sambuluma ‘Wana Zuke Muselebende’ ikiongozwa na Chimbwiza Mbambu Nguza ‘Vicking’.
Mwaka 1994 aliungana na Fred Ndala Kasheba, wakaunda bendi ya Zaita Musica iliyopata umaarufu mkubwa baada ya kuachia kibao cha ‘Kesi ya Kanga’, hapo ndipo mtindo wa ‘Kitambaa Cheupe‘ ulipozaliwa.
Kiki alikiri kwamba mtindo huo ndiyo hadi leo unaoipa wateja wanaopenda kucheza muziki wa kistaarabu huku wakipeperusha vitambaa vyeupe mikononi toka kwa bendi ya La Capitale aliyoiunda baada ya kifo cha Ndala Kasheba.
Katika bendi hiyo aliungana na mwimbaji mahiri Baziano Bwetti ambaye walikuwa pamoja katika bendi ya Orchestra Fouvette huko Zaire.
Kiki baada ya kuishi nchini kwa kipindi kirefu aliomba Uraia wa Tanzania amabapo alizifuata taratibu zote za Idara ya Uhamiaji, hatimaye mwaka 1997 alikubaliwa kuwa raia halali wa Tanzania.
Mkongwe huyo alipendwa sana na wapenzi na mashabiki wake wakampachaki majina ya ‘Bwana Mukubwa’ ambaye ana imani bendi yake ya La Capitale ‘Wazee Sugu’ iliyoundwa mwaka 2003, ndiyo bora kwa muziki wa dansi kwa sasa.
Alisema kuwa huenda bendi hiyo ndiyo atakayozeekea nayo, usemi huo yawezekana ukatimia kufuatia maradhi yanayomsumbua hivi sasa.
Kiki aliweza kusimulia siri ya mafanikio ya kung’ara kwake,
“Inawezekana kung’aa kwangu katika muziki kunatokana na nyota njema iliyojionyesha mapema, kwani nilizaliwa Januari Mosi, saa 11 alfajiri…” alijisifia Kikumbi Mwanza Mpango.
Bwana Mukubwa alielezea baadhi ya mafanikio aliyoyapata katika muziki kuwa ni pamoja na kuweza kukidhi maisha yake na familiya yake pia kumiliki bendi mbili ingine ipo katika jiji la Mwanza.
Kikumbi Mwanza Mpango ‘King Kiki’ ni baba wa familia ya mke na watoto kadhaa. Kati yao ni binti mmoja pekee aliyefuata nyayo za baba yake katika uimbaji.
Wahenga walinena kuwa “Gogo lililokuvusha usilitukane” Kiki alisisitiza kwamba kamwe hataisahau bendi ya Norvella Jazz aliyoanza nayo muziki mwaka 1962 huko nyumbani kwao Katanga, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kiki ni miongoni mwa nguli ambao hali zao kiafya siyo nzuri wakiendelea na matibabu majumbani mwao akina Salim Zahoro, Hassan Rehani Bichuka, Hussein Jumbe na Rashidi Pembe.
Mungu awaondoshee maradhi yao waweze kuendelee na shughuli zao za muziki.
Mwisho.
Mwandishi wa makala haya napatikana kwa namba: 0784331200, 0736331200, 0713331200 na 0767331200.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...