BARAZA la madiwani la
Halmashauri ya wilaya ya Songea limesikitishwa na wasimamizi wa Idara ya Elimu kushindwa
kusimamia taaluma na kusababisha Halmashauri hiyo kushika mkia kati ya
Halmashauri nane za Mkoa wa Ruvuma katika matokeo ya mtihani darasa la saba 2020.
Matokeo ya mtihani wa
Taifa wa Darasa la saba 2020,yanaonesha kuwa Halmashauri hiyo ilifaulisha kwa
asilimia 66.66 hivyo kuwa ya mwisho kimkoa.
Akizungumza kwenye
mkutano wa Baraza la madiwani,Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Menas Komba
ameiagiza Idara ya elimu msingi na
sekondari kuanza kuchukua hatua kwa wasimamizi na walimu ambao hawafany ikazi.
“Sisi kama Baraza la
madiwani sasa tutashughulika nao,tunataka Halmashauri ya Songea kielimu tuwe
juu,serikali imetoa fedha za utoaji wa elimu bure,waratibu elimu kata wamepewa
pikipiki,wanalipwa posho za madaraka shilingi 250,000 kila mwezi, wakuu wa shule
za msingi wote wanalipwa posho za madaraka hawafanyi kazi kikamilifu.’’ alisisitiza
Komba.
Ametoa rai kwa maafisa
elimu na wanaohusika kuchukua hatua na kwamba wanaoshindwa kusimamia elimu ameshauri wasihamishwe badala yake washushwe
vyeo na kwa kutoa mapendekezo kwa Mkurugenzi na kuletwa kwenye kikao cha
madiwani ili kushughulika nao.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Afya na Maji katika Baraza hilo Manfred Mzuyu
amesema kamati yake ilifanya utafiti kwa kutembelea kata,baada ya matokeo
mabaya ya elimu ya msingi na kubaini kuwa
baadhi ya waratibu elimu kata, pikipiki walizopewa na serikali
wanazitumia kwa matumizi yao na hawaishi kwenye vituo vyao vya kazi.
Kwa upande wake Diwani
wa Kata ya Kizuka Jacob Nditi amesema,uchunguzi walioufanya wamebaini
wasimamizi wa elimu wakiwemo waratibu Elimu Kata na walimu wakuu baadhi yao
hawasimami walimu ili kujua iwapo walimu wanafundisha ipasavyo.
“Kwanini baadhi ya waratibu hawaishi kwenye vituo vyao
vya kazi,sababu ni nini zinazosababisha
kupata ufaulu wa chini sana na kusababisha Halmashauri yetu kupata
aibu’’,alihoji Diwani Nditi.
Naye Diwani wa Kata ya
Mpitimbi Issa Said Kindamba amesema iwapo walimu wangewajibika ipasavyo
darasani kwa usimamizi wa walimu wakuu,Halmashauri isingepata ufaulu wa hatari na kusababisha Halmashauri
kushika nafasi ya mwisho kimkoa.
“Wilaya yetu imechafuka
kwa sababu ya kutofahamu mtu na uwajibikaji wake kwenye eneo ambalo
anasimamia,naomba utengenezwe mfumo wa
walimu kutambua wajibu wao kwa watoto na Taifa’’,alisema.
Diwani wa Kata ya
Kilagano ametoa rai kwa timu ya ukaguzi wa elimu,kueleza changamoto zipi
zinazoikabili sekta ya elimu hadi kutoa matokeo ya chini ya ufaulu.
Akijibu hoja hizo Afisa
Elimu Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Songea Tanu Kameka amekiri ufaulu sio wa
kuridhisha ambapo ameyataja matokeo ya mwaka 2019 ya darasa la saba Halmashauri
ilifaulisha kwa asilimia 71.99 na mwaka 2020 ufaulu ulikuwa wa asilimia 66.66.
Kameka amesema
wamefanya tathmini ya elimu kwa kupita
kata zote na kuwahusisha wadau wote wa elimu ambapo hivi sasa wanakusudia
kufanya ufuatiliaji wa hali ya juu mwaka mzima na kuchukua hatua kwa wasimamizi
wa elimu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...