Na
Albano Midelo
MTO Ruvuma ni miongoni
mwa vivutio vitano vya utalii vinavyoubeba Mkoa wa Ruvuma.Vivutio vingine ni
ziwa Nyasa,Makumbusho ya Taifa ya Majimaji,ushoroba wa Selous-Niassa,Hifadhi ya
Taifa ya Nyerere na utalii wa kiutamaduni na kihistoria.
Mratibu wa Utalii Kanda
ya Kusini Deborah Mwakanosya anasema Mto Ruvuma umeubeba Mkoa wa Ruvuma kwa
kuwa umepita katika wilaya zote tano ambazo ni Songea,Mbinga,Nyasa,Namtumbo na
Tunduru.
Mwakanosya anasema Mto
Ruvuma ndiyo Mto mrefu kuliko yote katika nchi za Afrika Mashariki na miongoni
mwa mito maarufu barani Afrika ukiwa umeanzia kwenye misitu ya milima ya
Matogoro Manispaa ya Songea na kumwaga maji yake Bahari ya Hindi.
“Mto Ruvuma
umedhihirisha maajabu ya Mungu ambayo hayawezi kusimuliwa katika mikoa mingine
nchini,ispokuwa Mkoa wa Ruvuma,katika milima ya Matogoro Manispaa ya Songea
tunakutana na chanzo cha mto Ruvuma,ukiona chanzo hicho,ni mfano wa kisima
kidogo sana ambacho kimetoa mfereji mdogo,lakini kazi yake huko mbele huwezi
kuongelea katika hali ya kawaida na kueleweka kwa jamii’’,anasisitiza
Mwakanosya.
Anasema kisima hicho
kidogo chenye mfereji mdogo kwenye milima ya Matogoro kipo meta 1500 toka usawa
wa bahari kimekwenda kuunda mto maarufu duniani unaoitwa Ruvuma ukiwa na urefu
za kilometa zaidi ya 800 na upana wa kati ya meta 300 hadi 500 kutegemea na
eneo lililopo kwa sababu kuna baadhi ya maeneo mto huo una upana mkubwa zaidi.
Kwa mujibu wa mhifadhi
huyo,Mto Ruvuma umebeba fukwe mbalimbali
zinazovutia wageni wengi ambapo anazitaja fukwe nyingi za kuvutia zinapatikana
kwa wingi katika hifadhi ya Taifa ya mazingira asilia ya Mwambesi iliyopo
wilayani Tunduru.
Anasema katika hifadhi
hiyo ,Mto Ruvuma umetengeneza visiwa na fukwe nzuri za kuvutia ambazo zinamwezesha
mtalii kuogelea na kuona wanyama wengi ambao wapo katika hifadhi hiyo kando
kando ya Mto Ruvuma wakiwemo tembo,mamba,simba,jamii ya swala na samaki wa aina
mbalimbali.
Hata hivyo Mratibu huyo
wa Utalii Kanda ya Kusini anasema ili mto huo uweze kufika katika Bahari ya
Hindi na kumwaga maji yake,unaanzia wilaya ya Songea milima ya Matogoro,unapita
katika shamba maarufu la AVIV ambalo wanaendesha kilimo cha umwagiliaji wa zao
la kahawa kupitia mto Ruvuma ambapo wameajiriwa watumishi zaidi ya 3000.
Kutokea hapo mto huo umepita hadi katika
eneo la Tulila wilayani Mbinga ambako Shirika la watawa wa katoliki wa
mtakatifu Agnes wameweka mradi mkubwa wa umeme wa maji kwenye maporomoko ya Mto
Ruvuma Chanzo
hicho kinamilikiwa na watawa wabenediktine wa Mtakatifu Agnes Chipole Jimbo Kuu
Katoliki la Songea.
Akizungumza kwa niaba ya Mama Mkuu wa Shirika
hilo,Sr.Richards Chiwinga(OSB) anasema wana mashine mbili ambazo zina uwezo wa kuzalisha
megawatts tano.
Analitaja bwawa la Tulila kuwa lina ukubwa wa
meta za ujazo milioni 1.14,likiwa na urefu wa meta 750 toka usawa wa bahari na
usawa wa maji(level) ni meta 748 na kwamba maji yakizidi kiwango hicho
yanamwagika.
Maporomoko ya Mto Ruvuma katika eneo la Tulila yana mandhari nzuri ya kuvutia unaweza kufanya utalii wa kupiga picha, kuogelea, kuendesha mtumbwi, pia kuna fukwe nzuri kutoka katika mto Ruvuma ambao ni miongoni mwa mito maarufu barani Afrika ambao unamwaga maji yake Bahari ya Hindi.
Mto Ruvuma katika
Wilaya ya Nyasa umepita kwenye Pori la Akiba la Liparamba ambako katika eneo la
Nakatuta kuna maporomoko mazuri ya maji ya mto Ruvuma ambayo yanavutia wageni
wengi pia katika eneo hilo mtalii anaweza kufanya utalii wa kuvua samaki na
kupanda kwenye tabaka la jiwe kando kando yam to Ruvuma..
Safari ya mto Ruvuma kutoka
Liparamba imeendelea hadi eneo la Mkenda mpakani mwa Tanzania na Msumbiji
ambako kumejengwa daraja kubwa lenye urefu wa meta 98 linalogawa Tanzania na
Msumbuji kupitia Mto Ruvuma.
Mwakanosya anabainisha
zaidi kuwa Mto Ruvuma umeendelea hadi katika wilaya ya Namtumbo kwenye Jumuiya
za uhifadhi wanyamapori vijijini ambazo ni Kimbanda,Kisungule na Chingoli na
kwamba Mto Ruvuma unaendelea hadi katika msitu wa Hifadhi ya mazingira asilia
Mwambesi wilayani Tunduru.
“Mto Ruvuma katika
hifadhi ya mwambesi kuna vivutio vya aina zote ikiwemo michezo ya kuendesha
mitumbwi ambayo kwa mara ya kwanza Tanzania mchezo wa kuendesha mitumbwi
ulizinduliwa mwaka 2019 katika eneo la Wenje Mto Ruvuma na watalii 22 ambao
walitoka nchi 16 duniani
walishiriki’’,anasisitiza Mwakanosya.
Anasema mto huo
ukishapita katika wilaya zote za mkoa wa Ruvuma unaendelea na safari yake hadi
katika daraja la umoja wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara na kuendelea hadi mkoani
Mtwara.
Mto Ruvuma unamwaga
maji yake katika Bahari ya Hindi kwenye eneo la kati ya Mtwara nchini Tanzania
na Rasi ya Delgado nchini Msumbiji.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...