Na Mwandishi wetu, Kiteto
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU, imemfikisha
Mahakamani mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Orkitikiti, Kijiji cha
Engong'ongare Wilayani Kiteto, Oscar Waluye na kusomewa mashtaka ya
udanganyifu wa mtihani.
Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Alli Sadiki Hajji akizungumza
na waandishi wa habari amesema pia, mwalimu huyo Waluye, amefukuzwa
kazi na mamlaka yake ya nidhamu.
Hajji amesema Waluye ameshtakiwa kwa kufanya udanganyifu katika
mtihani wa darasa la saba iliyofanyika Oktoba 2020 kitendo ambacho ni
kinyume cha kifungu cha 23 na 24 (1) sheria ya baraza la mitihani la
Taifa.
Amesema kesi hiyo ya jinai imefikishwa mbele ya hakimu mfawidhi wa wa
mahakama ya wilaya ya Kiteto, Joakim Mwakyolo na mwendesha mashtaka wa polisi Wilfred John.
"Hata hivyo, mshtakiwa amekana shtaka hilo na kushindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo kupelekwa rumande na kesi hiyo itatajwa tena Februari 16
mwaka huu," amesema Hajji.
Amesema uchunguzi wa TAKUKURU Wilayani Kiteto umeonyesha kwamba Waluye aliwalazimisha wanafunzi wawili wa darasa la sita wa shule hiyo
kufanya mitihani ya darasa la saba badala ya watahiniwa ambao uwezo
wao darasani unaelezwa ni wa kiwango cha chini.
"Pia Waluye alimkaririsha mwanafunzi mmoja aliyehitimu shuleni hapo
mwaka 2019," amesema Hajji.
Amesema wanafunzi hao wawili wa darasa la sita na mmoja wa darasa la
saba aliyehitimu mwaka 2019 walikamatwa na makachero wa TAKUKURU
tayari wakiwa wamefanya mitihani ya masomo ya Kiswahili na Hisabati
kwa niaba ya wanafunzi wenzao wanaodaiwa kuwa na uwezo mdogo huku
aliyekaririshwa akifanya mtihani wa mwanafunzi mtoro.
Amesema katika mahojiano na maofisa wa TAKUKURU Wilayani Kiteto,
Waluye alikiri kutenda makosa hayo kwa maelezo kuwa alitaka shule hiyo
ionekane imefaulisha vizuri.
"Kitendo hicho ni kinyume cha maadili kwa kuwa kinawajengea watoto
ambao ni Taifa la kesho tabia za ukiukwaji wa maadili na wakati wote
kuwa tegemezi," amesema Hajji.
Ametoa rai kwa wazazi, walezi na walimu kuwalea watoto katika njia
iwapasao kwani hawataiacha hata watakapokuwa wazee (Biblia Mithali
22:6.)
"Nitumie nafasi hii kuwafahamisha watumishi wa umma Mkoani Manyara
kwamba kuanzia sasa watakaodhihirika kutenda makosa ya jinai na Rushwa
tutakuwa tunawafikisha kwanza kwenye mamlaka zao za nidhamu na
kuwashtaki kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma na wasiendelee
kupokea mishahara bila kuifanyia kazi," amesema Hajji.
Amesema baada ya kuondolewa kwenye utumishi, mashtaka ya jinai
yatafuata kama ilivyofanyika kwa Mwalimu Waluye kwa kuwa jinai haina
ukomo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...