Kuokotoze ramani na kisha kuijenga
ni kutokuthamini kile unachokwenda kujenga licha ya kwamba unatumia
mamilioni ya pesa kujenga. Inashangaza sana kwamba unakuta mtu anaenda
kujenga nyumba ya milioni 90 lakini naokoteza ramani au anatafuta ramani
ambayo imetumiwa na mtu mwingine wakati gharama ya kutumia mtaalamu kwa
huduma yote ya ushauri pamoja na michoro labda ni 600,000/= ambayo
haifiki hata 1% ya gharama yote ya ujenzi. Maamuzi ya aina hii ni
maamuzi ambayo kwa vyovyote vile yanaambatana na hasara kubwa.
Madhara ya kuokoteza na kupata ramani ya nyumba kisha ukaijenga.
Iwe ni kutoka kwenye mitandao, au ni kutoka kwa mafundi wa
mitaani au kwa namna nyingine yoyote ile, kuokoteza ramani na kisha
kuijenga ni kushindwa kuuthamini mradi unaotaka kuujenga licha ya kwamba
unakwenda kutumia pesa nyingi sana kuujenga, na madhara yake ni kama
ifuatavyo.
-Utashindwa kupata unachotaka: Unapookoteza ramani
maana yake ni kwamba unalazimika kukubaliana na chochote kilichoko
kwenye ramani hiyo hata kama wewe binafsi una machaguo yako ya tofauti,
na kitu cha kushangaza ni kwamba huwa ni vigumu sana kukuta mahitaji ya
mtu mmoja yakafanana na mwingine kwa kila kitu, mara nyingi lazima
utakuta kuna vitu huvihitaji vipo na ambavyo unahitaji havipo.
Kila mtu
huwa na vipaumbele tofauti na mwingine, na hili ni kutoka kwenye uzoefu
kwa maana ya kwamba karibu kila kazi tunayokutana nayo huwa ni vigumu
kukuta inafanana na kazi ya mtu mwingine kwa vipaumbele vya kimahitaji,
achilia mbali utofauti wa ukubwa wa viwanja, utamaduni n.k.,. Unastahili
kufanya kitu cha peke yako kinachoendana na vipaumbele vyako.
-Hutaifurahia kazi yako: Kitu ambacho hujaweka akili
yako kwenye kuamua kiweje kadiri ya vipaumbele vyako nay ale
unayoyapenda huwa ni vigumu kufurahia, hata kama ikitokea ukapenda aina
fulani ya jengo au nyumba kutokana na muundo wake, bado kwa ndani kuna
vitu hutavifurahia namna jinsi vilivyopangika hivyo unachotakiwa ni
kuchukua picha ya lile jengo ulilolipenda na kisha kumuonyesha mtaalamu
kumwambia kwamba nataka liwe na muonekano huu kisha alipangilie upya kwa
ndani na kuchora upya lakini mwisho wa siku libaki na mwonekano ule
unaoupenda wewe.
-Unaweza kujuta sana baadaye: Utakapookoteza ramani,
kisha ikajengwa kama ilivyo au hata kama itabdilishwa lakini kienyeji
bila kutumia utaalamu sahihi na kushindwa kufikia vile unavyotaka wewe,
mara nyingi changamoto zake unakuja kukutana nazo baada ya kuanza
kulitumia jengo hilo na hapo ndipo unapokutana na uhalisia ambao
hukujihangaisha kuitazama kwa umakini lakini sasa unalazimika
kukabiliana nao wakati tayari jengo limekamilika na hapo ndipo
utakapojikuta unajuta kwa nini hukuweka umakini mwanzoni au kutafuta
mtaalamu wa kukuhakikishia kwamba mambo yanafanyika kwa usahihi, ambapo
inaweza kukulazimu sasa wakati huu kutafuta upya mtaalamu kuja
kurekebisha changamoto hizo kwa gharama kubwa sana zitakazohusisha
kuchora tena, kubomoa na kujenga ili kupata hasa unachotaka.
-Ukikutana na changamoto katikati utashindwa kuitatua:
Unapokutana na changamoto wakati wa kujenga, kitu unachofanya na kumwita
yule mtalaamu aliyechora kuja kuitatua kwa sababu yeye ndiye mwenye
uelewa wa kile alichofanya na ndiye mwenye nakala tete original ya mradi
husika kwa ajili ya kufanya mabadiliko yoyote yanayoweza kujitokeza,
lakini inapotokea sasa umeokoteza ramani pale inapotokea changamoto
yoyote ya kiufundi unakuwa huna msaada wa moja kwa moja na wakati
mwingine itakulazimu kufanya tena kienyeji kwa ugumu au kuharibu zaidi.
-Unaweza kushtakiwa: Itakapotokea yule aliyefanya kazi
husika akagundua kwamba kazi yake inatumika sehemu nyingine bila yeye
kujulishwa wala kufahamu chochote anaweza kuchukua hatua za kisheria
zitakazokuingiza kwenye gharama pengine kubwa kuliko ambayo ungelipia
raani husika.
-Unafanya kosa kisheria na kimaadili: Ni kosa kisheria
kutumia kazi ya mtu bila idhini yake na pia kosa kimaadili kutumia kazi
ya mtu kwa siri bila mwenyewe kujua kwani unakuwa umemwibia kazi hiyo.
-Kila ramani ina lengo tofauti: Karibu kila ramani
inayofanywa na wataalamu huwa ina malengo yake tofauti kutokana na
sababu mbalimbli, kwa mfano unaweza kuokoteza ramani ukaijenga kumbe
ramani yenyewe ilifanyika katika kiwanja ambacho ni kidogo sana hivyo
ikalazimika kuipunguza sana na hata kupunguza baadhi ya vitu muhimu
ndani ili iendane na kiwanja husika lakini wewe huna changamoto ya aina
hiyo na pengine unahitaji vyumba vyenye nafasi kubwa.
Au pia inawezekana
nyumba hiyo ilifanyw akwa ajili ya mtu mwenye familia kubwa na anaishi
na wazazi wake pamoja na ndugu wengine lakini wewe una familia ndogo na
unaishi na mwenza wako pamoja na watoto wawili peke yake na hivyo huwezi
kuwa unaendana na mahitaji yao. Mwisho ni utamaduni wa tofauti,
inawezekana wewe ni mtu unayependa kusoma nap engine ungehitahi maktaba
ndani ya nyumba wakati huyo mwingine anapenda sinema na anahitaji chumba
cha sinema au wewe ni mtu wa maombi sana nap engine ungehitaji chumba
maalumu kwa ajili ya sala wakati ramani uliyoiokoteza ni ya mtu
anayependa kunywa wine na bia mida ya jioni hivyo alikuwa akihitaji baa
ndani ya nyumba.
NB: Umuhimu wa kumtafuta mtaalamu kukufanyia ramani yako
mwenyewe inayozingatia vipaumbele vyako ni mkubwa sana hasa ukizingatia
kiasi cha fedha unayokwenda kuwekeza kwenye mradi huo ambao mwisho wa
siku pia utadumu kwa miaka mingi mbeleni, kwani ramani ya ujenzi
inaongeza thamani kubwa sana kwenye nyumba yako na kutoipa kipaumbele
sio rahisi kubaki salama.
Architect Sebastian Moshi
Whatsapp/Call +255717452790.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...