Na Kassim Nyaki-NCAA
Wananchi
kwa vijiji sita katika kata za Ngorongoro na Misigyo wanaoshi ndani ya
Hifadhi ya Ngorongoro wamenufaika na mradi wa simba kwa kupata shilingi
milioni 3 kwa kila Kijiji kutoka shirika la Kopelion Inc.
Kwa
mujibu wa muanzilishi na mtafiti mkuu wa Shirika la Kopelion Bibi
Ingela Janssan maarufu kama ‘mama Simba’ vijiji viliovyonufaka na mradi
huo ni Olorobi, Kayapus na Mokilal kutoka kata ya Ngorongoro na Vijiji
vya Misigyo, Loongoijoo na Kaitakiteng kutoka kata ya Misigyo.
Kwa mujibu wa Ingela Janssan mradi huo ulianzishwa mwezi oktoba mwaka
jana kama sehemu ya majaribio kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya
Ngorongoro (NCAA) kwa ajili ya Uhifadhi wa Mnyama Simba kupitia
ushirikishwaji wa Jamii kwa lengo la kupunguza mgogoro wa wananchi na
Simba katika maeneo ya hifadhi.
“Miaka 100
iliyopita duniani kote ilikadiriwa kuwa na simba 200,000, lakini kwa
sasa inakadiriwa kuwa na Simba 20,000 utaona kwa kiasi kikubwa simba
wamepungua kwa miaka 25 iliyopita, hivyo Shirika letu kwa kushirikiana
na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro na wadau wengine tunashirikiana na
jamii zilizoko maeneo ya Hifadhi kumlinda simba na kutomuona kama adui
wa mifugo na maisha ya watu ili Simba wazidi kuongezeka” amesema Ingela.
Ingela ameongeza kuwa kupitia uhifadhi shirikishi Shirika lake kwa
kushirikiana na Wadau mbalimbali linatoa malipo ya motisha kwa ajili ya
Uhifadhi wa Simba ambapo wananchi wanapomuona katika maeneo ya makazi
yao wanapaswa kutoa taarifa ya uwepo wa Simba hao bila kuwadhuru na
utaratibu huo unalenga kupunguza migogoro ya Wananchi na mnyama simba
(human-Lion Conflict).
Kwa upande wake mwenyekiti
wa Bodi Shirika la Kopelion Dkt. Bernard Kissui ameleza kuwa kihistoria
Simba walikuwa wengi sana duniani lakini kwa mujibu wa tafiti
mbalimbali idadi yao porini imekuwa ikipungua kutokana na mgogoro ya
Simba na binadamu hasa Simba wanapokula mifugo ya Wananchi na kuongeza
kuwa shirika la Kopelion lina lengo la kujenga mahusiano ya kijamii
kupitia program ya Uhifadhi Shirikishi.
“Mdadi
huu ulianza mwaka jana na tuliamua kuanza na kata mbili kama sehemu ya
majaribio kwa miaka mitatu ijayo, miezi minne iliyopita tumeona imeleta
manufaa makubwa kwa jamii kuhamasika katika mradi huu ndio maana leo
tumetoa malipo ya motisha kwenye vijiji sita vya kata 2 na kadri mradi
utakavyofanikiwa tutaongeza maeneo mengine” aliongeza Dkt Kissui.
Dkt Kissui amefafanua kuwa utoaji wa malipo kwa wananchi wa kata hizo
mbili ni faida inayotokana na kuwepo na Simba katika jamii ambapo
utaratibu huo unalenga kungeza idadi ya Simba kupitia uhifadhi
Shirikishi ili Simba waendelee kuwepo na Jamii izidi kunufaika badala ya
kumuona Simba kama adui yao.
Mratibu wa Mradi huo
kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw, Bashir Nchira ametoa rai
kwa wanufaika wa Mradi huo kuutekeleza kwa ufanisi na uzalaendo ili
waendelee kupata faida za mradi kupitia Hifadhi ya Ngorongoro na wadau
wa maendeleo.
“Kupitia ushirikishwaji huo huko
tuendako Simba atazidi kuonekana rafiki wa uhifadhi na si uadui,
Nawaomba muendelee kutoa ushirikiano kwa mashirika mbalimbali
yanayofanya tafiti za wanyamapori ndani ya hifadhi yetu” alisema Nchira.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro
ameupongeza mradi huo na kushauri shirika hilo kuongeza mradi wa Wanyama
wengine kama Fisi na Tembo ambao pia wamekuwa wakichangia migogoro na
wananchi. Aidha amewaasa viongozi wa vijiji vilivyonufaika na mradi huo
kuhakikisha wanabuni miradi yenye tija itakayosaidia wananchi na
kuhakikisha hakuna ubadhirifu ktika mradi huo.
Mratibu wa Mradi wa Simba kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw. Bashir Nchira akizungumza na wananchi wa kata ya Ngorogoro na Misigyo kabla hawajakabidhiwa malipo ya Motisha kwa ajili ya uhifadhi wa Simba.
Muanzilishi na mtafiti mkuu wa Shirika la Kopelion Inc Bibi Ingela Janssan maarufu kama ‘mama Simba’ akiongea na wananchi wa kata ya Ngorongoro kuhusu mradi wa kuhifadhi Simba katika maeneo yao wakati wa Sherehe wa kukabidhi hundi kwa wananchi wa vijiji vitatu vya kata hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...