Charles James, Michuzi TV
SERIKALI imesema imepanga kuhakikisha ndani ya miaka mitano ijayo Watanzania asilimia 80 wawe wanapata na kutumia huduma za Intaneti huku pia Mkonga wa Taifa ukiwafikia watanzania kwa asilimia hizo hizo 80.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma leo na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile alipokua akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kwenye semina iliyoandaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) yenye lengo la kuwapa uelewa wajumbe wa kamati hiyo kuhusu mfuko huo.
Dk Ndugulile amesema Wizara ya Mawasiliano ni mojawapo ya wizara ambayo kwa kiasi kikubwa inagusa kila wizara hivyo wako kwenye maandalizi ya kufanya mapinduzi ya kidigitali lakini pia kutengeneza matumizi wezeshi ya Tehama serikalini na kwenye sekta binafsi.
" Mfuko huu umeanzishwa mahususi kwa lengo la kupeleka mawasiliano kwa kila mtanzania, mawasiliano hayo siyo ya Simu pekee bali hata Televisheni na Radio nazo tumekua tukizipa msaada mkubwa katika kuhakikisha zinarusha vema matangazo yao.
Lengo letu ni kuhakikisha kupitia mkonga wetu wa taifa serikali siyo tu inatoa huduma ya mawasiliano kwa wananchi wake lakini pia inakusanya mapato ambayo yatasaidia pia kukuza uchumi wetu," Amesema Dk Ndugulile.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba amesema tayari wameshaini mikakati ya kufikisha mawasiliano kwenye kata 1,057 zenye vijiji 3,303 vyenye watanzania 12,981 huku kata 371 ambazo bado zitakamilika Oktoba mwaka huu.
Amesema Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote tayari ushakamilisha miradi katika kata 686 zenye vijiji 2,489 ambavyo vina wakazi Milioni Nane sawa na asilimia 65 ya miradi yote.
" Siyo hivyo tu pia tuna miradi ya kuwezesha shule zetu za umma kuunganishwa na mitandao ya intaneti na tayari tumeshafanya hivyo kwa baadhi ya shule lakini pia tuna miradi ya Tiba Mtandao ambapo kwa kushirikiana na wadau wa afya tayari tumeanza ambapo sasa Mgonjwa aliyepo Hospitali ya Rufaa Morogoro anaweza kuwasiliana na Daktari aliyepo Hospitali ya Muhimbili, " Amesema Mashiba.
Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba akitoa mada kwenye semina ambayo Mfuko huo iliuandaa kwa ajili ya wabunge ambao ni wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya miundombinu.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile akizungumza mbele ya wajumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya miundombinu katika semina iliyoandaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote UCSAF leo jijini Dodoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...