WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameiagiza Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kuwanyang'anya wale wote walioshindwa kuendeleza vitalu walivyokodishwa katika ranchi za kampuni hiyo kwa sababu wamekiuka masharti ya mkataba.
Ndaki alitoa agizo hilo alipokutana na Viongozi wa Chama cha Wafugaji katika kikao cha kujadili Maendeleo ya Sekta ya Mifugo kilichofanyika jijiji Dodoma Februari 10, 2021.
Alisema kuwa kuna watu wengi wamekodishwa maeneo katika ranchi za taifa lakini wamezitelekeza na wengine wamekodisha watu wengine ambao wanatumia maeneo hayo kinyume na makubaliano ya mkataba.
"Ikifika tarehe 15 mwezi huu, wale wote waliochukua vitalu na wamekodisha watu wengine wanyang'anywe maeneo hayo na hatutajali mikataba yao kwani wameshakiuka masharti," alisema Ndaki
Aliongeza kwa kusema kuwa baada ya tarehe 15 kupita wataanza kuwasaka wote waliochukua maeneo hayo na kuwanyang'anya ili wapewe wafugaji makini waweze kutumia maeneo hayo kuweka mifugo yao.
Kuhusu baadhi ya Wananchi wanaoishi karibu na ranchi kuvamia maeneo hayo, Ndaki alitumia nafasi hiyo pia kuwataka waondoke katika maeneo hayo na wasipofanya hivyo wataondolewa.
Aliendelea kusema kuwa wameanza mikakati ya kuiweka vizuri NARCO ili maeneo makubwa iliyonayo ambayo mengine hawayatumii vizuri yagawiwe kwa wafugaji watakaoweza kuyatumia kufanya ufugaji wa kisasa nah atua waliyoanza nayo ni kupunguza bei ya kukodisha vitalu.
"Tumekubaliana kuwa bei ya kukodisha kitalu iwe ni shilingi elfu tatu mia tano (3500) kwa Ekari moja na sio zaidi ya hapo," alisema Ndaki
Waziri Ndaki alisema kuwa wameielekeza NARCO kuwa katika yale maeneo waliyoyatenga kwa ajili ya ukodishaji watenge asilimia thelathini (30) kwa ajili ya kuwakodisha wafugaji wanaoishi karibu na maeneo ya ranchi hizo ili kupunguza migogoro na uvamizi wa maeneo hayo.
"Hata maeneo yetu yaliyotengwa kwa ajili ya kupumzishia mifugo (holding grounds) tutayapunguza ili nayo tuwape NARCO ili wayakodishe kwa wafugaji wetu, tunaamua kufanya haya ili kutibu tatizo la malisho na wafugaji waondokane na kutangatanga," alifafanua Ndaki
Mapema wiki hii Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NARCO, Paul Kimiti alitangaza kuwa ekari moja ya kitalu katika ranchi hizo itakodishwa kwa shilingi elfu tatu mia tano (3500).
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (kulia) akiteta jambo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro walipokutana katika kikao cha kujadili Maendeleo ya Sekta ya Mifugo kilichofanyika jijini Dodoma Februari 10, 2021.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akifafanua jambo kwa baadhi ya wafugaji waliohudhuria kikao cha kujadili Maendeleo ya Sekta ya Mifugo kilichofanyika jijiji Dodoma Februari 10, 2021.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akiongea na Wafugaji (hawapo pichani) katika kikao cha kujadili Maendeleo ya Sekta ya Mifugo kilichofanyika jijiji Dodoma Februari 10, 2021.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...