Na Amiri Kilagalila,Njombe
Askofu mkuu wa kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Mussa Magwesela,amekemea vikali watanzani wanaoendelea kuombeana na kutangaza vifo badala ya kuombeana amani huku akisikitishwa na vitendo hivyo vilivyoanza kuongezeka zaidi hivi karibuni mara baada ya janga la Corona lililoikumba Dunia.
Magwesela amebainisha hayo mkoani Njombe wakati wa ibada ya kuwekwa wakfu kwa kazi ya kichungaji Mch.Lucas Ndugu pamoja na uzinduzi wa pastoreti mpya ya Njombe.
“Tuache kutamkiana mabaya iwe kwa mtazamo wa kisiasa au kiimani tukasahau undugu wetu na mshikamano wetu na kwasababu hiyo niwasihi sana viongozi wa kisiasa,wakidini,wakiharakati tuweze kuungana na kutakiana mema katika kipindi hiki” alisema Askofu Magwesela
Vile vile amesema Maradhi ya Corona yanawaangamiza wengi katika ulimwengu hivyo misimamo katika kukabiliana na janga hilo isiwe chanzo cha kuvurugana.
“Tumeshuhudia misimamo tofauti na pengine tumehitilafiana kuona ni namna gani tunaukabili ugonjwa huu.Mtumishi wa Mungu peke yake ndiye anayeweza kuwa faraja,anayeweza kuleta matumaini,anayeweza kuonyesha njia ili kuwasaidia watu” Askofu mkuu wa kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Mussa Magwesela
Kwa upande wake mchungaji mpya wa Pastorate ya Njombe Mch,Lucas Ndugu amesema kanisa lina dhamana kubwa ya kuhimiza kurejesha amani hivyo atashirikiana na viongozi wengine katika kuitunza amani.
“Viongozi tuna nafasi kubwa ya kusababisha amani ya nchi yetu hasa kwa kuwafundisha watu kumjua Mungu kwasababu hata mafundisho yanasema mjue sana Mungu ili uwe na amani kwa hiyo bado hata amani ya nchi ina tutegemea”alisema Mch,Lucas Ndugu
Kwa upande wao baadhi ya waumini wa kanisa hilo akiwemo Chritina Job Mwang’ondya wamesema wanaamini amani ya nchi italindwa na watanzania wenyewe hivyo ni rai kwa kila mtanzania kuitunza tunu hiyo huku pia wakitoa pongezi kwa kanisa lao kupata mchungaji mpya pamoja na kuzinduliwa kwa Pastorate hiyo.
Askofu mkuu wa kanisa la Africa Inland Church
Tanzania (AICT) Mussa Magwesela ameongoza ibada ya kuwekwa wakfu kwa kazi ya
kichungaji Mch.Lucas Ndugu pamoja na uzinduzi wa pastoreti mpya ya Njombe,na
kuwataka watanzania kuendelea kuitunza amani ili kujiletea maendeleo.
Askofu mkuu wa kanisa la Africa Inland Church
Tanzania (AICT) Mussa Magwesela akizungumza umuhimu wa kutunza amani pamoja na
kuendelea kudumisha amani hususani katika kipindi hiki kigumu cha mlipuko wa
maradhi ya Corona.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...