NA DENIS MLOWE, IRINGA
KUELEKEA
maadhimisho ya siku ya Mwanamke Duniani Machi 8 mwaka huu, Mbunge wa
Viti Maalum Mkoa wa Iringa (CCM) ,Ritta Kabati, amewataka wazazi
hususani wanawake kuachana na tamaduni za kisasa katika mfumo wa malezi
ya watoto na kurudi katika malezi kwa kuzingatia tamaduni zetu za
Kitanzania.
Alisema
ifike wakati wazazi wa sasa wakubali kuwa kuna mahali wameteleza warudi
katika mila na desturi za Kitanzania zile ambazo ni nzuri za kulea
watoto wetu, kuna faida kubwa sana kuliko kuwalea watoto katika tamaduni
za wenzetu.
Dkt. Kabati ameyasema hayo wakati
wa uzinduzi wa wiki ya Wanawake katika halmashauri ya Manispaa ya
Iringa, iliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya sekondari Lugalo na
kuratibiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.
Dkt.
Kabati amesema ipo haja ya wazazi kukumbuka namna walivyolelewa katika
tamaduni na mila za Kitanzania ambazo kwa asilimia kubwa ziliweza
kuwaongoza watoto katika njia bora iliyowafanya watoto kuwa na heshima
na staha katika jamii.
"Ukitafuta sababu kubwa
ya mmomonyoko wa maadili kwa vijana wengi sasa, utaona Malezi ya kisasa,
kuiga mambo ya wenzetu ambayo sisi si tamaduni zetu. Hapo ndipo tatizo
lilipoanzia, Mzazi wa sasa anataka mtoto awe kama mzungu, turudi kwenye
njia zetu za Kitanzania ni bora zaidi"
Aidha,
Dkt. Kabati ameiasa jamii hususani wazazi Wanawake kuwashirikisha sana
watoto na mambo ya Dini kwami kutawafanya watoto waweze kuyajua mazuri
na mabaya ambayo Mungu hayapendi na hivyo kupunguza mambo mengi maovu
yanayotokea sasa.
"tuwapeleke watoto wetu
katika ibada na mafundisho ya dini, hii ni muhimu sana maana watoto kule
watajua lipi Mungu hapendi na lipi wafanye kumfurahisha Mungu. Hata
sisi wakati tunakuwa tumehimizwa sana mafundisho ya dini, sasa hivi
mtoto anajilea mwenyewe hii sio sawa".
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Umoja Wanawake wa CCM (UWT) mkoa wa Iringa,
Mama Nicolina Lulandala amewataka Wanawake kuungana katika nyanja ya
kiuchumi kwani kufanya hivyo kutawasaidia kuchangia pato la familia na
Taifa.
Bi. Lulandala amesema Tanzania ya sasa
inamuhitaji mwanamke mjasiriamali ambaye atasaidia Tanzania kufikia
malengo ya kuwa na uchumi utegemeao viwanda pamoja na biashara ili
kujikwamua kiuchumi katika jamii.
"Tanzania
ya sasa inamuhitaji Mwanamke mjasiriamali, Mwanamke atakayeiwezesha
Tanzania kufikia uchumi wa Kati unaotegemea Viwanda. Wanawake tuna nguvu
kubwa sana katika kunyanyua uchumi wa familia zetu na Nchi yetu kama
tutajitambua katika hilo".
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...