Na Mwandishi Maalum

Waandishi wawili wa Tanzania (Bara na Visiwani), Veronica Mrema (Matukio na Maisha Blog) na Pandu Abdalla, wametwaa tuzo mbili zinazoangazia umahiri katika uandishi wa habari za magonjwa yasiyoambukiza (NCDs), Ukanda wa Afrika Mashariki (EAC).

Tuzo hizo EAMNA zimetolewa kwa mara ya kwanza na Jukwaa la Mashirikisho ya Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza Afrika Mashariki (EANCDA), kutambua mchango na juhudi za waandishi hao katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo.

Akizungumza mwishoni mwa wiki katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya kuelimisha jamii kuhusu Magonjwa Yasiyoambukiza (TOANCD), ambayo wanachama wake ni waandishi wa habari zinazohusu magonjwa hayo, 

Meneja wa Programu wa Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), Happy Nchimbi alisema waandishi hao wameing'arisha Tanzania.

“Tuzo hizi zilitangazwa hivi karibuni, Tanzania Bara hakuna mwandishi aliyejitokeza kutuma kazi isipokuwa Veronica, alikuwa peke yake…, kwa kweli nimefurahi kuona amehudhuria kikao hiki leo.

“Mambo yamekwenda vizuri, ameshinda, tunampongeza… kwa kweli ametutoa kimasomaso,” alisema Happy.

Happy alisema waandishi wa habari wanafanya kazi kubwa na nzuri nchini katika kuelimisha jamii kuhusu magonjwa hayo huku akiwahimiza kuchangamka kuwasilisha kazi mashindano yanapotangazwa.

Kwa upande wa Zanzibar, washiriki walikuwa wawili akiwamo Pandu Abdalla na mwenzake Khadija Khamis ambapo Pandu aliibuka kidedea.

Mwenyekiti wa TOANCD, Leon Bahati aliwapongeza washindi hao kwa kuing’arisha bendera ya Tanzania na kusisitiza kwamba tuzo hiyo ni chachu kwa wanahabari nchini kuendeleza mapambano dhidi ya magonjwa hayo.

Tuzo hiyo za EAMNA zilizotolewa na EANCDA zilihusisha washiriki kutoka Tanzania, Zanzibar, Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda lengo ikiwa ni kutambua mchango wa waandishi wa habari  katika mapambano dhidi ya NCDs.

EANCDA katika tuzo hizo pia imewatambua waandishi bora kwa upande wa gazetini, redioni, runinga na mtandaoni (online).

Kwa mujibu wa EANCDA, katika nchi hizo zaidi ya waandishi 150 wamefikiwa na Mashirikisho hayo na kupatiwa mafunzo jinsi ya kuelimisha jamii kuhusu magonjwa hayo na hata watunga sera kuweza kuchukua hatua katika kuyakabili.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...