TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Lindi inaendelea na utekelezaji wa majukumu yake ya kuzuia na kupambana na rushwa ili kuimarisha utawala bora na kuhakikisha haki inatamalaki.
Katika taarifa yake Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Lindi, Eng. Abnery J. Mganga iliyotolewa mbele ya waandishi wa habari, leo Machi 12, 2021, wameshirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka, kuwafikisha mahakamani watuhumiwa watatu ambao uchunguzi wa tuhuma dhidi yao umekamilika.
Taarifa hiyo imewataja watuhumiwa hao kuwa ni Abdallah Musa Mbinga, ambaye ni Mpimaji wa Ardhi (land surveyor), katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, Mohamed Musa Mtungwe, ambaye ni Mjumbe wa Serikali ya kijiji cha Nahukahuka B, Hassan Ally Mohamed, ambaye ni Mkulima na mkazi wa kijiji cha Nahukahuka B.
Imeeleza kuwa TAKUKURU Mnamo tarehe 28 Mei, 2018 Mkoani humo wa ilipokea taarifa kutoka katika vyanzo vyao vya siri, ambavyo viliwalalamikia watuhumiwa kutumia nyaraka za udanganyifu na kufanikiwa kujipatia fedha isivyo halali kinyume na sheria.
"Watuhumiwa hao walijipatia fedha zilizotolewa na kampuni iitwayo CASSAVA STARCH OF TANZANIA LIMITED kwa ajili ya kuwafidia wakulima wa kijiji cha Nahukahuka B kupisha mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza wanga, ambapo mwekezaji huyo alikuwa ametoa fidia ya jumla ya sh 450,336,500/=."
Taarifa hiyo imeeleza kuwa TAKUKURU Mkoa wa Lindi ilianzisha uchunguzi mara moja kwa lengo la kubaini na kuthibitisha ukweli wa tuhuma hizo.
"Na uchunguzi wa TAKUKURU mkoa wa Lindi ulibaini kwamba, Mtuhumiwa wa kwanza Bw. Abdallah Musa Mbinga, akiwa ni mtumishi na Mpimaji wa Ardhi (land surveyor), katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtama, alifanya mabadiliko kwenye taarifa ya uthamini wa mali za wananchi huku akijua kuwa, kufanya hivyo ni kinyume na sheria, na alifanya hivyo huku akijua wazi kwamba mabadiliko aliyokuwa akiyafanya siyo halali na kitendo hicho kingepelekea kulipa fidia kwa watu ambao hawakuwemo kwenye taarifa ya awali ya fidia kinyume na sheria." Imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, Uchunguzi ulibaini kuwa mtuhumiwa huyo aliondoa jina la kijiji cha Nahukahuka “B” kwenye orodha ya malipo na kuingiza majina ya watu watatu likiwepo jina lake mwenyewe, jina la Bw. Mohamed Musa Mtungwe, pamoja na Bw. Hassan Ally Mohamed, na hivyo kusababisha fedha kiasi cha sh. 80,956,800/= ambazo zilistahili kulipwa kama sehemu ya fidia ya Kijiji hicho - kulipwa kwa watu hao watatu akiwepo yeye mwenyewe.
Kutokana na udanganyifu huu wa kutumia nyaraka mtuhumiwa wa kwanza alijipatia sh 60,747,579/= mtuhumiwa wa pili alijipatia sh 10,047,645.79/= na mtuhumiwa wa tatu alijipatia sh 21,767,225.
Watuhumiwa walikuwa na makosa ya Kutumia nyaraka za uongo kwa lengo la kudanganya, Kinyume na Kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.
Kula njama na kutenda kosa kinyume na kifungu cha 32 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007, Kughushi nyaraka.
Kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, Pamoja na Kuisababishia Serikali hasara,
TAKUKURU mkoa wa Lindi inatoa rai kwa watumishi na wananchi wa mkoa wa Lindi kwa ujumla kujiepusha na vitendo vyovyote vya Rushwa kwani kila mmoja wetu anajua madhara yatokanayo na vitendo vya Rushwa, na kamwe TAKUKURU kwa kutumia mamlaka tuliyopewa kwa mujibu wa sheria hatutasita kuendelea kuwachukulia hatua za kisheria, ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani wale wote ambao wanajihusisha na vitendo vya Rushwa.
TAKUKURU mkoa wa Lindi inaendelea kuwashukuru wananchi, vyombo vya Habari, pamoja na taasisi mbalimbali (binafsi na za serikali) katika Mkoa wa Lindi kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuutoa kwa ofisi yetu ikiwepo kutoa taarifa mbalimbali za vitendo vya rushwa. Aidha, tunawaomba wananchi na wadau wote katika mkoa wetu, waendelee kutuunga mkono kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa kutumia njia mbalimbali hususani kupitia simu yetu ya dharura ya nambari 113 kwani mapambano dhidi ya rushwa sio ya TAKUKURU peke yake bali ni ya jamii nzima kwa ujumla.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...