Na Jusline Marco-Arusha
Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii Dkt.Allan Kijazi amewaagiza wakuu wa Taasisis zote zilizo chini ya wizara ya maliasili na utalii kuwapandisha vyeo watumishi wenye utendaji mzuri na wanaostahili kabla ya Mei 31 mwaka huu pamoja na kuendelea kuwapa mafunzo ya muda mfupi na mrefu ili kuweza kuwajengea uwezo na weledi utakao wawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi unaotarajiwa.
Akisoma hotuba ya Waziri wa maliasili na utalii Dkt.Damas Ndumbaro katika ufunguzi wa Mkutano wa 28 wa baraza la wafanyakazi wa wizara ya maliasili na utalii ambapo amewataka wafanyakazi hao kuzingatia sheria, kanuni na miongozo katika kusimamia ukusanyaji wa maduhuli ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea.
Aidha amesema serikali inatoa kipaumbele katika kuboresha maslahi ya watumishi ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ya msingi kwa ufanisi unatarajiwa na wananchi ambapo serikali imetoa kibali cha kuwapandisha vyeo watumishi wenye utendaji mzuri na waliotengewa nafasi katika mwaka wa fedha 2018/19 na 2020/21.
Dkt.Allan Kijazi ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza hilo amesema kuwa suala la ukusanyaji wa maduhuli ni suala muhimu kwa wizara kama inavyoelekezwa katika sheria,kanuni na miongozo mbalimbali ya serikali ambapo amewataka kukuza wigo wa bidhaa za utalii ili kufikia watalii milioni 5 na kuongeza mapato kufikia dola za kimarekani bilioni 6 ifikapo mwaka 2025.
Ameongeza kuwa ili kufikia azma hiyo wanapaswa kuimarisha utalii wa uwindaji wanyama pori, kukuza utalii wa mikutano pamoja na kuendeleza utalii wa fukwe sambamba na kuimarisha usimamizi, ulinzi na uhifadhi wa maliasili kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho kwa kuendelea kujenga uwezo wa wadau katika kusimamia rasilimali za wanyapori,misitu na nyuki pamoja na kudhibiti ujangili wa wanyama pori na mazao ya misitu na nyuki kwa kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia uwekezaji katika sekta .
“Lakini pia tunatakiwa kuendelea kusimamia, kuendeleza na kulinda malikale kwa manufaa ya taifa kwa kuboresha usimamizi, matumizi na uhifadhi wa maeneo ya malikale na urithi wa utamaduni ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu wezeshi ya utalii katika maeneo hayo kwa kuweka mazingira ya kuvutia wawekezaji na kuhamasisha kufanyika kwa matamasha ya kitamaduni,” Alisema Dkt.Kijazi
Vilevile ameeleza kuwa wizara hiyo imeanzisha Jeshi la uhifadhi la wanayama pori na misitu kwa lengo la kuendelea kulinda, kusimamia na kuhifadhi rasilimali hizo ambapo pamoja na hayo jeshi hilo linalenga kuimarisha nidhamu kwa watumishi na weledi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku .
“Ninawaomba muendelee kuimarisha nidhamu, ukakamavu na uadilifu katika kutekeleza majukumu yenu ya uhifadhi na ni matumaini yangu kuwa matukio ya ujangili na biashara haramu ya mazao ya wanyapori na misitu yatapungua kwa kiasi kikubwa kutokana na jitihada zinazoendelea kufanywa na Jeshi letu la uhifadhi wa wanayama pori na misitu,” Alisema Dkt.Kijazi
Lucius Mwenda mkurugenzi wa idara ya utawala na rasilimali watu amesema waliyoyasikia katika mkutano huo yatawasaidia kujua mwajiri anataka nini na kitu kilichopangwa na wao watahusika katika kutekeleza na kusema kuwa asilimia kubwa inategemea mwajiri kuwapa vitendea kazi, kujali maslahi ya wafanyakazi pamoja na utayari wa wafanyakazi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi {TUGHE} tawi la maliasili na utalii,Antony Tibaijuka ameeleza kuwa nafasi waliyopewa kupitia bajeti pamoja na kupewa ruhusa ya kuzungumza yale waliyonayo ni jambo ambalo litawafanya wafanyakazi kutekeleza majukumu yao vizuri na kufikia malengo yanayo hitajika.
Katibu Mkuu wa wizara ya Maliasili na Utalii Dkt.Allan Kijazi akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa 28 wa baraza la wafanyakazi wa wizara ya maliasili na utalii uliofanyajika jijini Arusha.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...