Na Judith Mhina Maelezo
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa, amesema
kujikosoa ni kujisahihisha maneno aliyoyanukuu kutoka kwa muasisi wa Taifa la
Tanzania Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Maneno
hayo ameyatamka wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha 14 cha mwaka huu kwa Maafisa
Habari, Mawasiliano na Uhusiano Serikalini kilichofanyika katika Chuo Kikuu cha
Sayansi na Tekinolojia Mbeya (MUST) hivi karibuni.
Waziri
Bashungwa amenukuu maneno hayo kutokana na hali halisi ya Maafisa Habari wa
Serikali hapa nchini ambao wana wajibu wa kujikosoa na kujirekebisha katika kutimiza majukumu yao kama kaulimbiu ya
Kikao Kazi hicho inavyosema, “Taarifa kwa Umma ni Takwa la Kisheria, Viongozi wa
Umma na Maafisa Habari Tuwajibike.”
Aliongeza
kuwa, ili kutimiza takwa hilo wote kwa
pamoja wana wajibu wa kuhakikisha
wanasimamia kama viongozi ili walengwa ambao ni Mafisa Habari wa
Serikali watangaze na kusemea kazi zote
za Serikali ikiwemo miradi ya kimkakati, Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali
kwa ustawi wa wananchi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.
“Tuna
taarifa kuwa baadhi ya Maafisa Habari
walioko katika utumishi wa Umma ni watu
ambao hawataki kujituma na kuwa wabunifu
ingawa wanawezeshwa kwa kupewa vifaa vya kazi na kushirikishwa ndani ya menejimenti husika, pamoja na kushirikishwa
katika ziara zote lakini hawatimizi wajibu wao.” alisema Waziri
Bashungwa.
Aidha,
katika dhana nzima ya kujikosoa na kujisahihisha kama alivyosema Mwalimu
Nyerere, upo wajibu wa kukitendea haki Kikao
Kazi hicho, ambacho ni cha siku tano kuanzia
Mei 24-28, 2021 ili kuwa chachu ya
kuleta mageuzi makubwa katika kuhakikisha
Maafisa Habari wanaisemea na kuitangaza Serikali ili Umma wa Tanzania
wajue kile ambacho Serikali yao inafanya.
Katika
suala zima la wajibu wa mwajiri, Maafisa Habari wengi wapo Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI), Wakala wa Serikali, Taasisi za Umma
na Wizara. Kuna changamoto kadhaa zinazowakabili maafisa hao kama vile kuwa
chini ya mtumishi wa Kitengo cha TEHAMA, au kuonekana kama mpiga picha tu
wakati wa matukio mbalimbali na kutoshirikishwa katika maamuzi ya Menejimenti husika.
Amesema
kuwa Sheria ya Huduma za Habari namba 12 ya mwaka 2016 na kanuni zake za Mwaka
2017 pamoja na Sheria ya Haki ya kupata Taarifa Na. 06 ya mwaka 2016 ndivyo
vinavyomfanya Afisa Habari kutambulika na kutimiza wajibu wake. Sheria hizi
zinajenga taaluma ya Habari na kuifanya kutambulika rasmi.
Waziri
Bashungwa amebainisha changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika Halmashauri
za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji, zikiwepo za Maafisa Habari kuchanganywa na
Watumishi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambao wakati mwingine
huweza kukorofisha mawasiliano ya kimtandao na hivyo kukwamisha kazi za maafisa
habari.
Kuhusu
suala la kutokuwa na vitendea kazi pamoja na kupewa majukumu ambayo si yao na kushirikishwa
tu pale yanapotokea matukio Waziri Bashungwa alitoa maelekezo kwa Katibu Mkuu
Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kuangalia suala hilo na kuona umuhimu wa
kuwashirikisha maafisa Habari katika vikao vya maamuzi ili kuwa na uelewa mpana utakaowasaidia kutangaza
na kusemea kazi nzuri zinazofanywa na Serikali.
Kuokana
na changamoto mbalimbali zilizoainishwa na Waziri Bashungwa, Idara ya Habari (MAELEZO)
ilipata fursa ya kufanya mahojiano na baadhi ya
Maafisa Habari Grace Gwemagobe wa Mkoa wa Songwe ambaye alisema “Maafisa
Habari walio wengi katika Mikoa na Halmashauri mbalimbali nchini wana changamoto
ya utendaji wa kazi, kwa kuwa inategemea kiongozi anayemkuta katika sehemu
husika ana utashi gani juu ya kada ya Afisa Habari. Aidha, mara nyingi inakuwa kama ni hisani, au kujuana na kiongozi wako badala ya kusimama
kwenye mfumo halisi ulivyo wa kiutumishi
au kulingana na taratibu za kusimamia utumishi wa umma.
Gwemagobe
ameongeza kuwa yeye yupo chini ya Idara ya Utawala na Rasilimali watu ambapo kiongozi wake ni Katibu Tawala
Msaidizi sehemu ya Utawala na Rasilimali watu, na Maafisa Habari wengi hawajui miongozo ya uendeshaji (PMG) katika Sekretarieti ya Mkoa. Hatua hiyo inasababisha
Maafisa Habari wengi wa Mkoa kuishia kuwa Katibu wa
Wakuu wa Mikoa badala ya kufanya
kazi za Afisa Habari kama ilivyoelekezwa
katika taratibu za utumishi wa umma.
Naye
Afisa Habari wa Halmashauri ya Mji wa Mufindi Ndimiyake Mwakapiso amesema “ Ofisi
za Serikali ni za umma kwa hiyo kama Mkuu wa Kitengo au idara ni Afisa Habari
au Mtumishi wa TEHAMA haina tatizo
lolote kwani tunafanya kazi kwa kushirikiana
na mambo yanaenda tu”.
Mwakapiso
pia ameongeza kuwa kuna baadhi ya
Halmashauri Maafisa Habari ndio wakuu wa
vitengo na wanawasimamia watumishi wa TEHAMA, kwa nia njema tu na kusisitiza
kuwa wanafanya bila tatizo lolote.
Naye
Afisa Habari ambaye hakutaka jina lake litajwa amesema “Mimi binafsi katika
ofisi yangu sina vitendea kazi wala hakuna kitengo cha habari tunawekwa mahala
popote kiongozi wetu anapodhani tunaweza kuwa hapo. Pia hatuna bajeti ya kitengo, vilevile mara
nyingi wakuu wa idara wenye miradi mbalimbali hawatushirikishi kwa kuhofia
tukienda kwenye miradi tutadai kulipwa fedha na wao hawako tayari kulipa posho
ya Afisa Habari badala ya yeye na wahusika katika ofisi yake”.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...