Wakati bondia Hassan Mwakinyo akifanikiwa kutwaa ubingwa wa Afrika (ABU) wa uzito wa Super Welter kwa njia ya knockout (KO) dhidi ya mpinzani wake Antonio Mayala, bondia Jongo Shaaban amewahudhunisha mashabiki wake kwa kupigwa kwa KO dhidi ya Mnigeria Olanrewaju Durodora.

Mwakinyo ametwaa ubingwa huo katika raundi ya tisa kwenye ukumbi wa Next Door Arena ijumaa usiku katika pambano kali na la kusisimua lililoandaliwa na kampuni ya Jackson Group chini ya Afisa Mtendaji Mkuu, Kelvin Twissa

Bondia huyo alikabidhiwa mkanda wa Ubingwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Damas Ndumbaro sambamba na waziri wa Michezo, Innocent Bashungwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya michezo, Yusuph Singo.

Mbali ya viongozi hao, katika makabidhiano hayo pia walikuwepo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB,Cosmas Kimaro, Mkurugenzi wa Multichoice Tanzania Jackline Woiso na Meneja Masoko wa M-Bet Tanzania, Allen Mushi.

Mwakinyo hakupata ushindi huo kirahisi kutokana na Mayala kupigana kwa mbinu kubwa huku akitengua mitego kadhaa.

Mayala aliingia raundi ya tisa kwa ‘pupa’ kwa kujua kuwa Mwakinyo amechoka, jambo ambalo lilimponza na kudumu kwenye raundi hiyo kwa sekunde 55 tu, baada ya kupigwa konde kali la mkono wa kushoto na kwenda chini moja kwa moja na kushindwa kuendelea na pambano.

Mwakinyo alisema kuwa alimshukuru Mungu kwa ushindi huo.

“Nanshukuru Mungu kwa ushindi huu, natamani kufika mbali zaidi na kupigana na mabondia wakali zaidi, duniani na niliahidi kutowaangusha watanzania na Rais Mama Samia Suluhu Hassan,” alisema Mwakinyo.

Wakati huo huo bondia aliyepewa nafasi kubwa ya kushinda ubingwa wa ABU wa uzito wa Juu, Shaaban Jongo alichapwa kwa KO na bondia Olanrewaju Durodora wa Nigeria katika raundi ya pili.

Jongo alitawala sana pambano hilo, ila alijikuta anachezea kichapo baada ya kutojilinda na kupigwa ngumi kali kutoka kwa Mnigeria huyo na kushindwa kuendelea katika pambano hilo lililodhaminiwa na Benki ya KCB, Bodi ya Utalii, DStv, Onomo Hotel, M- Bet, Plus Networks Limited.

Pia bondia Ibrahim Class alishinda kwa pointi mpinzani wake, Sibusiso Zingane wa Afrika Kusini huku bondia Hamis Palasungulu akichapwa kwa KO na Ardi Ndembo wa Congo Brazzaville katika pambano la uzito wa juu.

Naye bondia Imani Daudi akishindwa kwa pointi dhidi ya Chris Thompson na Leila Yazidu akipoteza kwa pointi dhidi ya bondia kutoka Bulgaria, Joana Nwamerue. Pia Daniel Matefu ambaye alichapwa kwa pointi na bondia wa Bulgaria Pencho Tsvetkov.


Waziri wa Maliasili na Utalii Damas Ndumbalo (wa nne kulia) akimvisha mkanda wa uzito wa Super Welter wa afrika bondia Hassan Mwakinyo. Wanaoshuhudia makabidhiano hayo ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya KCB Cosmas Kimaro (wa tatu kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice, Jakline Woiso (wa tatu kushoto) na CEO wa jackson Group Sports, Kelvin Twissa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...