NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kagahe amewataka wajasiriamali nchini kuzalisha bidhaa zenye ubora ili ziweze kuhimili ushindani wa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Naibu Waziri Kagahe, ameyasema hayo juzi mjini Babati mkoani Manyara, kwenye ufunguzi wa maonyesho ya 16 ya kanda ya kaskazini ya shirika la kuhudumia viwanda vidogo nchini Sido.

Amesema umuhimu wa kuzalisha bidhaa zenye ubora, utasababisha zipate soko ndani na nje ya nchi hivyo wajasiriamali wa Tanzania wazingatie hilo.

Pia, amesema katika kuhakikisha lengo la kukuza uchumi wa viwanda linatimia, serikali inaendelea kubuni sera na mikakati ya kukuza uwekezaji kupitia wajasiriamali wadogo.

"Serikali inaandaa sera mpya  ya maendeleo ya viwanda vidogo na biashara ndogo ambayo pamoja na mambo mengine imetazama namna bora ya kuwawezesha wajasiriamali vijana kuingia katika shughuli za kiuchumi," amesema.

Amesema serikali inaendelea na hatua mbalimbali za kuwawezesha wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa katika kukuza fursa za masoko kwa kuendelea kupanua wigo mpana wa masoko katika jumuiya ya Afrika Mashariki,nchi za SADC, ambapo pia kwa sasa serikali ipo katika hatua za mwisho kulipia mkataba wa eneo huru la biashara Afrika.

Amewataka wajasiriamali kutumia masoko hayo kikamilifu ili serikali ipate nguvu ya kuendelea kuwatafutia fursa zaidi.

Amesema sekta ya Viwanda na Biashara nchini imeendelea kuongeza miundombinu ya kufanyia kazi wajasiriamali wadogo katika mitaa ya viwanda vidogo vya Sido ambapo mpaka sasa imejenga zaidi ya majengo 15 kwenye mikoa ya Manyara, Geita, Kigoma, Mtwara na Dodoma kwa ajili ya uzalishaji, kazi hiyo ni endelevu.

Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya TEMDO iliyo chini ya wizara ya Viwanda na Biashara inayohusika na utafiti, usanifu na utengenezaji wa Teknolojia mbalimbali mhandisi Profesa Fredrick Kahimba, amewataka wenye changamoto ya teknolojia kuwasiliana nao ili kupata msaada na biashara zao kupata tija.

Amesema katika kuwafikia wajasiriamali wadogo wanawatembelea katika mikoa mbalimbali na kupitia mtandao wa  Sido.

Maonesho hayo ya 16 ya Sido  yanabebwa na kauli mbiu isemayo Maendeleo ya viwanda nuru ya maendeleo kiuchumi, yanatarajiwa kufungwa Mei 31,2021 na mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere.




 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...