IMEELEZWA kuwa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), unatarajiwa kuwekwa mifumo ya kisasa ambayo itasaidia kuzuia ajali ambazo zinaweza kujitokeza wakati wa uendeshaji wa reli hiyo na ambao hautamruhusu dereva kuzidi ama kupunguza mwendo uliowekwa.
Hayo yamesemwa na Meneja Msaidizi wa mradi wa reli ya Kisasa, kipande cha Morogoro - Makutopora (Km 422) kutoka Shirika la Reli Tanzania (TRC), Mhandisi Christopher Mang’wela, wakati akizungumza na wahandisi kutoka Serikalini na Sekta Binafsi ambao wametembelea mradi huo uliofika asilimia 61, jijini Dodoma, kwa ajili ya kujifunza utekelezaji wa mradi kuanzia hatua mbalimbali zilizotekelezwa.
“Kama mnavyoona, mradi umefika asilimia 61, na uendeshaji wake utakuwa ni wa kisasa kwani utawekwa vifaa maalum vya kumuongoza dereva wa treni ili kuzuia ajali.” amesema Mhandisi Mang'wela.
Awali, akizungumza kwa niaba ya wahandisi hao, Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Mhandisi Patrick Barozi, ameeleza kuwa anaona nia ipo na uwezo kwa watanzania katika kusimamia miradi mikubwa inayoendelea nchini huku tukiwa na usimamizi mdogo kutoka wenzetu wa nje na hivyo kuwaleta wahandisi wetu katika mradi kutaongeza chachu ya kuchukua zabuni nyingi za miradi mikubwa inayoatarajiwa kuanza na kuendelea hapa nchini.
"Kwa kawaida miradi ina hatua tano za utekelezaji ikiwemo kuibua mradi, kupanga jinsi ya kutekeleza mradi, utekelezaji wa mradi, ufuatiliaji wa utekelezaji wa mradi na kufunga mradi ambapo hivi ni lazima vizingatiwe ili mradi ufanikiwe”, amesisitiza Mlinga.
Naye, Mhandisi kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Nyandalo Hezron, amesema kuwa wamefurahishwa na mafunzo hayo kwani yamewasaidia kujua uhalisia wa yale waliyojifunza darasani na kuyaleta katika utekelezaji ambayo yawakumbusha miongozo mbalimbali katika usimiamizi wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi inayoendelea.
Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) ulioanza mwezi Aprili 2017 wenye
lengo la kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji nchini na nchi za jirani
unaendelea kutekelezwa ambapo hivi karibuni kazi za ujenzi sehemu ya Isaka –
Mwanza yenye urefu wa kilometa 341 unatarajiwa kuanza.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...