Charles James, Michuzi TV
AHADI imetimia! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile kukabidhi jezi seti mbili na mipira mitatu kwa Timu ya Mpira ya Vijana wa Bodaboa Wilayani Buhigwe, Kigoma.
Mei 13 mwaka huu akiwa katika ziara ya kampeni za kumnadi mgombea Ubunge wa Jimbo la Buhigwe, Kavejuru Felixi katika uchaguzi uliofanyika Mei 16 mwaka huu, Mbunge Ditopile alikutana na vijana wa Bodaboda wa kituo cha Buhigwe ambapo walimuomba awasaidie kupata jezi na mipira kwa ajili ya Timu yao inayoshiriki mashindano mbalimbali.
Katika kutimiza ahadi hiyo Mbunge Ditopile amekabidhi mipira hiyo leo, ambapo Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Buhigwe, Agnes Ndoliki amekabidhi kwa niaba ya Mbunge huyo.
" Niliahidi kuwapatia vifaa vya michezo hapa Buhigwe, leo nimefanya hivyo niwaombe mtumie vifaa hivi kama ambavyo mliomba katika kufanya mazoezi ya kujiweka fiti kiafya lakini pia kuendeleza vipaji vyenu, michezo ni ajira na Mkoa wa Kigoma umetoa mastaa wengi sana katika Soka, Juma Kaseja ni mfano wa Kigoma.
Niwapongeze sana kwa kukipa kura za kishindo Chama chetu CCM katika uchaguzi mdogo wa Ubunge uliofanyika Mei 16, mmeonesha imani yenu kubwa kwa CCM na mmempa heshima kubwa Rais Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais Dk Philip Mpango," Amesema Ditopile kupitia kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Buhigwe.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodaboda hao, amemshukuru Mbunge Ditopile kwa moyo wake wa kukumbuka ahadi ambayo aliiahidi huku akimuombea dua na kumtaka kuendelea na moyo huo huo wa kusaidia makundi mbalimbali licha ya yeye kuwa Mbunge anayetokana na kundi la Wanawake.
" Tunaomba mtufikishie salamu kwa Mariam Ditopile, ameonesha moyo wa tofauti sana, kitendo cha kutimiza ahadi aliyotuahidi tena tukiwa sio wananchi wa Jimbo lake wala hatutokani na kundi analoliongoza imeonesha jinsi gani ni kiongozi mwenye kujali na mwenye upendo, tunamshukuru Sana," Amesema Mwenyekiti huyo.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...