TANZANIA imedhamiria
kuendelea kuongoza barani Afrika kwa uzalishaji wa zao la pareto toka tani 3000
mwaka 2021 hadi kufikia malengo ya tani 9,000 kutokana na uwepo wa viwanda vitatu
vya kuongeza thamani zao hilo.
Hayo yamebainishwa leo
(28.05.2021) jijini Dodoma wakati wa
kikao cha wadau wa zao la pareto toka mikoa sita nchini kilichoshirikisha
viongozi wa mikoa, wilaya ,halmashauri, makampuni ya pareto na wawakilishi wa
wakulima.
Akizungumza kwenye kikao
hicho Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe aliwapongeza wadau kwa kuweka lengo
hilo la kufikisha tani 9,000 za maua ya pareto ambapo viwanda vitatu vilivyopo
sasa vitaweza kuinunua yote kulingana na uwezo wake.
Bashe alisema ili kufikia
malengo hayo ya uzalishaji wizara kupitia Bodi ya Pareto na Taasisi ya Utafiti
wa Kilimo (TARI) itawekeza kwenye utafiti wa mbegu bora za pareto na
kuhakikisha zinapatikana kwa wingi na kugawiwa kwa wakulima nchini.
“Tunahitaji mbegu bora za
pareto tani 3 ili zitumike kuzalisha tani 9,000 za pareto baada ya mwaka
mmoja ambapo viwanda viko tayari
kuinunua toka kwa wakulima” alisisitiza Bashe
Naibu Waziri huyo
alizipongeza Kampuni ya Pareto Tanzania (PCT) ambayo itanunua tani
6,000 kwa mwaka huku kampuni ya TAN Extract Ltd ikihitaji tani 1,000 na kampuni
ya PYTECH Ltd ikihitaji tani 2,000 za
maua ya pareto itakayozalishwa na wakulima msimu wa 2022/23.
Katika hatua nyingine Bashe
alibainisha mikakati ya wizara kuhakikisha zao la pareto linakuwa na tija na
uzalishaji wake unaongezeka zaidi ambapo alitaja mambo sita .
Kwanza kuongeza utafiti na
uzalishaji wa mbegu bora tani 3 kupitia TARI,
pili kuanzisha mfumo wa kilimo mkataba (Contract Farming), tatu
kuanzisha mfumo wa ushirika kwa kuanzisha AMCOS za wakulima wa pareto.
Mkakati wa nne ni kuhamsisha
Halmashauri kutenga mashamba vitalu
(Block Farming )kisha kugawa kwa wakulima ambapo lengo kuanzia ekari 200 ,tano
ni kusajili na kuwatambua wakulima wa pareto na sita wizara itaendelea na
juhudi za kuondoa migogoro baina ya wanunuzi kwa kutenga kanda ( Zone of
production).
Kwa upande wake Mkulima bora wa zao la pareto Mzee Anangisye
Mwankina kutoka Kata ya Ipelele Kijiji cha Makwaranga Tarafa ya Magoma
wilaya ya Makete ametoa ombi kwa wizara
ya Kilimo kuwashirikisha viongozi wa
wilaya nchini kutoa ushirikiano wa karibu kwa wakulima wa pareto ili ubora wa
zao uongezeke hatua itakokuza bei.
Mwankina ambaye amekuwa
mkulima bora wa pareto tangu mwaka 2014 hadi sasa ametoa ombi kwa Rais Samia
Suluhu Hassan kwenda kutembelea wakulima wa Makete hatua itakayoongeza ari ya
Kilimo hicho.
“Ninalima ekari 3 ambapo kwa mwaka navuna kilo 800 na ubora
wangu umefikia 1.8% lakini tatizo letu mabenki yanatukopesha kwa riba kubwa mno
hatua inayotukwamisha. Tufikishie salamu kwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan
aje atutembelee Makete” alisema Mzee
Mwankina.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Bodi ya Pareto nchini Lucas Ayo alisema uzalishaji wa zao la pareto
umeongezeka toka tani 2,011 mwaka 2015/16 hadi kufikia tani 2,510 mwaka 2019/20
kati ya lengo la kuzalisha tani 3,000.
Aidha alibainisha kuwa tija
imeongezeka toka wastani wa kilo 250 kwa ekari mwaka 2015/16 hadi kufikia kilo
270 kwa ekari mwaka 2019/20 huku wastani wa bei ya chini anayolipwa mkulima
imepanda toka shilingi 1500 mwaka 2015/16 hadi shilingi 2,400 mwaka 2019/20 na
shilingi 2,500 mwaka 2020/21 kwa kilo moja ya pareto.
Ayo alitaja mkakati wa Bodi
ya Pareto katika mwaka 2021/22 ni kuongeza utafiti wa kina kuhusu matumizi
mbalimbali ya bidhaa za pareto ikiwemo visumbufu vya mimea mashambani, majumbani
na kwenye maghala ya mazao hatua itakayochochea kukuza kilimo na tija cha zao
la pareto.
Naye Mbunge wa Mbeya Vijijini Oran Njeza alisema wakulima wa Mbeya vijijini
wanaomba Wizara ifanye zao la pareto kuwa zao la kimkakati kwani ndilo
linategemewa zaidi kimapato.
Mdau huyo alitoa wito kwa Wizara
ya Kilimo ichukue hatua za haraka
kuisaidia bodi ya pareto kifedha na watumishi ili isimamaie zao hili kwa ufanisi
na kuwa sasa bodi haifanyi vizuri kwenye usimamizi wa zao hatua inayopelekea
wakulima wakate tama.
“Zao la pareto kwa muda
mrefu limekosa ushindani hatua inayosababisha liwe na bei ndogo, hivyo wizara
ihamasishe wawekezaji zaidi wa viwanda vya kuongeza thamnai zao la pareto”
alisema Njeza.
Kuhusu suala la kutenga
maeneo ya kilimo Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya wilaya ya Mbulu Hudson
Kamoga alisema wamelenga kuongeza eneo la uzalishaji pareto toka ekari 40 za
sasa hadi kufikia ekari 100 kwa kutumia Block Farming hatua itakayokuza
uzalishaji ambapo msimu huu wamezalisha tani 4.3 za pareto .
Zao la pareto kwa sasa
linalimwa kwenye mikoa ya sita ya
Arusha, Manyara, Songwe, Njombe na Iringa ambapo Bodi imefanikiwa hadi kufikia Februari 2021
imesajili wakulima 10,586 kwenye mfumo
wake wa utambuzi na huduma kwa wakulima.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...