Jane Edward Michuzi TV, Arusha

Waziri wa Nishati Dk.Medard Kalemani, amemuagiza mkandarasi wa Kampuni ya Sagemcom kutoka nchini Ufaransa, kuhakikisha kwamba hawaruki kijiji au kitongoji chochote wakati wa mpango wa usambazaji wa umeme vijijini katika Wilaya ya Longido mkoani Arusha.

Waziri Kalemani, alitoa agizo hilo  wakati wa uzinduzi wa mradi wa umeme vijijini (REA), awamu ya tatu mzunguko wa pili mkoani Arusha na uzinduzi huo ulifanyika jana katika Kijiji cha Kiseriani Kata ya Engikaret wilayani Longido mkoani humo.

“Mkandarasi wakati wa kufanya kazi ya kusambaza umeme sitarajii kuona mnaruka baadhi ya vijiji au vitongoji katika kata hii ya Engikaret, na agiza maeneo yote yanayopitiwa na mradi huu wananchi wote wapate huduma ya umeme,”alisema Kalemani.

Alisema kwa Mkoa wa Arusha mradi huo una thamani ya Sh.bilioni 47 kwa ajili ya kusambaza nishati ya umeme kwa wananchi vijijini.

Mbali na kuzungumza hayo,Waziri Kalemani, alimuagiza mkandarasi huyo, kuhakikisha kwamba anakamilisha ujenzi wa mradi huo ndani ya miezi 12 (Mwaka mmoja), na endapo mradi hautakamilika kwa wakati hawatamuongezea muda.

Alisema kati ya vijiji 12268 hapa nchini, hadi sasa vijiji 10,400 vimeshapatiwa umeme na vijiji vingine 1600 bado havijafikiwa na umeme hivyo hadi kufikia mwisho mwa mwaka 2022 vijiji vyote vitakuwa vimeunganishiwa umeme.

Pia amemuagiza wakandarasi huo, kutokuwalipisha wananchi fedha za kununua nguzo za umeme au kuwaomba rushwa kwa kuwa watakuwa wamekwenda kinyume na makubaliano na mkataba wao.

Vile vile Waziri Dk.Kalemani, amewaagiza Mameneja wa Shirika la Umeme nchini(TANESCO), wa Mikoa,Wilaya na Kanda ndani ya miezi miwili wahakikishe wanawaunganishia umeme wananchi waliolipa fedha zao kuunganishiwa huduma hiyo,

Waziri huyo, alisema wananchi wakikamilisha utaratibu wa malipo na mambo mengine TANESCO, wanatakiwa kuwaunganishia umeme ndani ya siku 14 baada kukamilisha utaratibu wote.

Aidha aliwaomba wananchi wa eneo hilo,kuhakikisha wanatunza na kulinda miundombinu ya umeme kwa kuwa lengo la serikali ni kufikisha huduma hiyo kwa wananchi.

Naye Mkurugenzi wa REA, Mhandisi Amosi Maganga, alisema mradi wa kusambaza umeme vijijini hapa nchini, umegharimu fedha zaidi ya Trilioni tatu.

Alisema zaidi ya asilimia 84 ya vijiji vyote nchini vimeshaunganishiwa huduma ya nishati ya umeme.



 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...