Na. Georgina Misama - MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kuimarisha Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete  ili kuendelea kutoa huduma bora katika utambuzi na tiba za maradhi ya moyo ndani na nje ya nchi.

Akizunguza wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Mitambo mipya ya uchunguzi na tiba ya maradhi ya  moyo ‘Catheterization laboratory na Carto 3’  Rais Samia amesema kwamba mitambo hiyo itaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi nane Afrika zenye mitambo ya aina hiyo.

“Mitambo ya Cathelab na  Carto 3 tunayo zindua leo  ni ya kisasa zaidi na  imegharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.6 . Mitambo hii itatufanya tuwe miongoni mwa nchi nane Afrika yenye mitambo ya aina hiyo, Tanzania kwa sasa tunakwenda juu katika utambuzi na tiba za maradhi ya moyo”, anasema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia anasema kwamba Taasisi ya  JKCI imekuwa msaada mkubwa kwa Watanzania na wasio Wantaaznia kwani mpaka sasa wagonjwa wapatao 5,959 wamepatiwa matibabu ya upasuaji wa moyo ambapo kati yao wagonjwa 11 sawa na asilimia 0.2 walipoteza maisha.

Akiongelea magonjwa yasiyoambukiza , Rais Samia anasema kwamba magonjwa hayo kama vile moyo, kisukari, figo na saratani yanaongezeka duniani kote ikiwemo Tanzania ambapo ongezeko hilo linachangiwa pia na kukuwa kwa wataalam wa kugundua magonjwa hayo kwani kabla ya wataalam nchini kuwepo wagonjwa wengi walipoteza maisha pasipo kufahamu nini chanzo cha tatizo.

Takwimu za magonjwa yasiyoambukiza  duniai zinaonyesha kwamba mwaka 2016 kulitokea vifo milioni 41 sawa na asilimia 71 ya vifo vyote wakati huo ambapo kwa Tanzania asilimia 33 ya vifo vilitokana na magonjwa yasiyoambukiza huku moyo na shinikizo la damu vikisababisha vifo kwa asilimia 13

”Asilimia 13 ya vifo kutokana na magonjwa ya moyo na shinikizo la damu ni kiasi kikubwa sana kuacha itokee nchini, kwa kuzingatia hilo leo tuna furaha kubwa kuzindua mitambo hii ya tiba na uchunguzi wa moyo, lengo ni kupunguza asilimia hizo za vifo”, aliendelea kufafanua

Pamoja na kuahidi kushughulikia changamoto zinazonaikabili Taasisi hiyo ikiwepo upungufu wa watumishi na punguzo la msamaha wa matibabu, Rais  Samia pia anapongeza watumishi wa taasisi hiyo kwa kazi yao ya kipekee na yenye kuhitaji utaalamu wa aina yake, “Kazi mnaifanya sijui niipe sifa gani, maana naogopa kukufuru lakini kuweza kusimamisha moyo wa mwanadamu kwa masaa kadhaa, sio kazi ya kawaida”, anasema Rais Samia.

Kwa upande wake Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema kwamba hospitali zote za rufaa ikiwemo JKCI zipo kwenye mchakato wa kuandaa maandiko ili kuweza kupata ithibati ya kimataifa lengo ni kutengeneza utalii wa kitabibu hapa nchini.

“Tupo kwenye maboresho katika hospitali zetu zote za rufaa, tumekubaliana baada ya kupata mitambo ya kisasa sasa tuandae maandiko na kufuata taratibu zote ili tuweze kupata ithibati ya kimataifa, lengo letu kubwa ni kuifanya Tanzania kuwa kituo cha utalii katika kada hii ya afya. Hospitali zetu zote kama vile Ocean Road, MOI, Benjamini Mkapa na nyingine zinakimbizana kukamilisha jambo hilo”, anasema Dkt. Gwajima.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tasisi hiyo, Prof. Mohamed Janabi amesema kwamba idadi ya wagonjwa wanaopokelewa na kutibiwa katika taasisi hiyo inaongezeka siku hadi hadi siku na hata miundo mbinu imekuwa ikipanuliwa kukidhi uhitaji huo, ambapo ameiomba Serikali kusaidia kiasi cha shilingi bilioni 2 ili kujenga jengo jipya na  hatua za awali zimeshafanyika.

“Ujenzi wa Taasisi hii ulianza mwaka 2002 na tulianza rasmi kufanya kazi mwaka 2014 ambapo huduma zetu zimeendelea kujipanua kadri uhitaji unavyoongezeka. Tulianza na chumba kimoja cha upasuaji, na hivi sasa tunavyo vine, vitanda vilikuwa 6 na sasaiv vimefika 25 na hata upande wa watumishi wetu tupo 319 sawa na asilimia  80. Bado tunaendelea kujipanua na ningependa siku moja jengo hili libakie kuwa la watoto tu, na jengo kuwepo na jengo lingine kwaajili ya watu wazima”, anasema Prof. Janabi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akisikiliza maelezo pamoja na kukagua mtambo wa Kisasa Catheterization Laboratory uliounganishwa na mtambo wa Carto 3 system 3D and mapping electrophysiology system wenye uwezo wa kufanya uchunguzi, kufunga vifaa visaidizi vya moyo, kuzibua mishipa ya damu ya moyo na kutibu hitilafu ya mfumo wa umeme wa moyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...