Watumishi
watakaokuwa wakitoa huduma kupitia Kituo cha Huduma kwa Wateja (Call centre
Customer Service) cha Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma
wanashiriki mafunzo ya namna bora ya kutoa huduma kwa umma kupitia kituo hicho
kinachotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
Akifungua
mafunzo hayo Jijini Dodoma leo kwa niaba ya Katibu Mkuu-UTUMISHI, Mkurugenzi wa
Mipango, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Cosmas
Ngangaji amesema, kituo hicho kitasaidia wadau kupewa mrejesho wa masuala ya
kiutumishi kwa wakati tofauti na ilivyo sasa ambapo wanalazimika kusubiri
wajibiwe kwa barua.
Bw. Ngangaji
amesema, utoaji wa huduma kupitia kituo hicho utapunguza adha ya wanaohitaji
huduma na kuongeza kuwa, utajenga mahusiano mazuri kati ya Ofisi ya
Rais-UTUMISHI na wadau wa masuala ya kiutumishi na utawala bora kwani
utarahisisha upokeaji wa maoni na malalamiko ya kiutumishi yanayowasilishwa na
kuyashughulikia kwa wakati.
“Ifahamike
kuwa, uanzishwaji wa kituo hicho hauondoi mifumo rasmi ya utoaji huduma na
ushughulikiaji wa malalamiko, bali ni moja ya utaratibu wa kisasa wa utoaji
huduma kwa njia ya TEHAMA.” Bw. Ngangaji amesisitiza.
Amefafanua
kuwa, Kituo hicho kitaunganishwa na Mfumo wa Kielektroniki wa Kushughulikia
Malalamiko (e-malalamiko) ambao umesanifiwa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya
Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).
Mafunzo
hayo ya siku tatu yana lengo la kujenga uelewa wa watumishi juu ya namna bora
ya kuendesha kituo hicho na kubadilishana uzoefu wa ushughulikiaji wa malalamiko na maoni ya wadau
ambayo yatakayoboresha uendeshaji wa Kituo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji wa Maadili, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Leila Mavika, amemshukuru
Bw. Ngangaji kwa maelekezo aliyoyatoa na kuahidi kuwa kituo hicho kitatumika kujenga
taswira nzuri ya Ofisi na Serikali kwa ujumla.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...