Charles James, Michuzi TV

SERIKALI imetangaza tenda za masafa na Redio kwa Mikoa 20 nchini huku pia ikitangaza kutumia kiasi cha Sh Bilioni Mbili katika uimarishaji wa urushaji wa matangazo kwenye maeneo hayo.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile wakati akizindua Redio Jamii jijini Dodoma ambayo imefadhiliwa na Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote UCSAF na Shirika la Utangazaji TBC.

Dk Ndugulile amesema serikali pia inakwenda kufanya mapitio ya tozo za Redio kwenye Wilaya na maeneo ya mipakani ambapo itapunguza tozo hizo lengo likiwa ni kuongeza usikivu kwenye wilaya hizo.

Waziri Ndugulile ametoa wito kwa watanzania kufika kwenye Ofisi za Mamlaka ya Mawasiliano TCRA ili kuangalia Wilaya ambazo tenda hizo zimetangazwa ambapo zitaenda sambamba na punguzo la leseni kwenye Redio hizo.

" Niwapongeze UCSAF na TBC kwa ushirikiano wenu huu wa kuanzisha Redio Jamii ambayo Sasa inakwenda kuwa na manufaa kwa wananchi wa Mikoa ya Kanda ya Kati, niwahakikishie kama Wizara tutaendelea kushirikiana nanyi katika kuleta usikivu wa mawasiliano," Amesema Dk Ndugulile.

 Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote UCSAF, Justina Mushiba amesema gharama halisi ya ukarabati na ununuzi wa vifaa vya Radio Jamii hiyo ni Sh Bilioni 1.71 huku TBC wenyewe wakitoa Sh Milioni 163.

Mushiba amesema uzinduzi wa Radio hiyo ni muendelezo wa Mfuko huo kurahisisha mawasiliano ambapo awali walishafanya hivyo jijini Arusha na leo ni zamu ya Dodoma.

" Tarehe 30 tutazindua kituo kingine cha kurusha matangazo katika eneo la Kisaki ambacho pia tumekifadhili sisi lengo ni kuhakikisha Radio yetu ya Taifa inasikika kila kona.

Sisi na Shirika letu la TBC tuna miradi mingine tunajenga ya kurushia matangazo kwenye mipaka ya Nchi yetu ili kuzuia Wananchi wetu wasipate matangazo na taarifa kutoka Nchi zinazopakana na sisi," Amesema Mushiba.

Nae Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dk Ayoub Ryoba ameishukuru UCSAF kwa ufadhili huo huku akiwataka wananchi wa Dodoma na Mikoa jirani kuitumia Redio hiyo katika kujikwamua kiuchumi, kielimu na kijamii.

Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano Kwa Wote UCSAF, Justina Mashiba (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dk Ayoub Ryoba wakipeana hati ya makabidhiano ya Radio Jamii Dodoma ambayo imefadhiliwa na UCSAF. Tukio hilo limefanyika leo jijini Dodoma.
Waziri WA Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile akizungumza kwenye uzinduzi wa Radio Jamii ambayo imezinduliwa leo katika Ofisi za Makao Makuu ya Shirika la Utangazaji TBC.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wengine mara baada ya kuzindua Radio Jamii jijini Dodoma leo.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...