Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
LIGI Kuu Soka Tanzania Bara (VPL) rasmi imehitimishwa leo kwa michezo Nane ikizikutanisha timu 16 zinazoshiriki Ligi hiyo zikijitupa kwenye viwanja mbalimbali huku Wekundu wa Msimbazi, Simba SC wakiibuka Mabingwa wa Ligi hiyo baada ya kufikisha alama 83 katika Msimamo.
Katika mchezo wa mwisho uliopigwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Simba SC ilipata ushindi wa bao 4-0 dhidi ya Namungo FC, mabao hayo yamefunywa na Medie Kagere, Chris Mugalu na John Bocco.
Simba SC imeibuka Mabingwa wa Ligi hiyo wakati Yanga SC wakishika nafasi ya Pili, Azam FC nafasi ya Tatu na Biashara United nafasi ya Nne wao wakipata nafasi ya kushiriki Michuano ya Kimataifa kwa mara ya kwanza katika historia ya Soka la Tanzania na Taifa kuwakilishwa na timu Nne kwenye Michuano hiyo ya Kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.
Wakati Simba SC wakitawazwa Mabingwa wa VPL, timu za Mwadui FC, Ihefu SC, JKT Tanzania na Gwambina FC tayari zimeshuka daraja na msimu ujao zitacheza Ligi daraja la kwanza (First Division League) huku timu za Coastal Union na Mtibwa Sugar wakicheza na timu za Ligi Daraja la Kwanza, Pamba FC ya Mwanza na Transit Camp katika mchezo wa kutafuta timu zitakazorudi kwenye Ligi Kuu msimu ujao (Play Off).
Coastal Union watacheza na Pamba FC na Mtibwa Sugar watacheza na Transit Camp FC katika michezo hiyo ya Play Off kati Julai 21 na michezo ya marudiano Julai 24, 2021.
Timu za Simba SC, Yanga SC, Azam FC, Biashara United, KMC FC, Polisi Tanzania, Tanzania Prisons, Dodoma Jiji FC, Namungo FC, Mbeya City, Ruvu Shooting FC na Kagera Sugar zimesalia kwenye Ligi hiyo Msimu ujao na zitaungana na timu za Mbeya Kwanza FC na Geita Gold FC msimu ujao.
Katika Ligi hiyo Mshambuliaji na Nahodha wa Simba SC, John Raphael Bocco ameibuka kuwa Mfungaji Bora baada ya kufunga mabao 16 akiwaacha Chris Mugalu (Simba SC) aliyefunga mabao 15, Medie Kagere wa Simba SC mabao 13 na Prince Mpumelelo Dube wa Azam FC mabao 14 katika kinyang’anyiro hicho cha kuwania Kiatu cha Dhahabu.
Julai 25, 2021 siku ya Jumapili kutapigwa mchezo wa kumaliza msimu katika Kombe la Shirikisho la Azam Sports Federation Cup (ASFC) msimu huu wa 2020-2021 baina ya Simba SC na Yanga SC katika dimba la Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...