Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
BARAZA la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Tanzania (NACOPHA) limewatoa hofu Watu wenye maambukizi hayo ya Virusi vya Ukimwi kuhusu ugonjwa wa COVID-19 baada ya Tanzania kukumbwa na wimbi la tatu la ugonjwa huo ulioenea duniani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari mkoani Dar es Salaam, Mwenyekiti wa NACOPHA, Bi. Leticia Mourice Kapela amesema Baraza hilo linawatoa hofu Watu hao wenye VVU huku likiwataka kuchukua tahadhari na kufuata miongozo yote inayotolewa na Mamlaka za Afya katika kupambana na janga hilo.
“Jamii yetu inapaswa kuondokana taarifa potofu zinazoenezwa juu ya COVID-19 kwa Watu wenye VVU, Watu hawa ni sawa na watu wengine kwani wapo wenye VVU waliugua Corona na wakapona kwa kuzingatia Tiba sahihi kutoka kwa Wataalamu wa Afya”, amesema Bi. Leticia.
Bi. Leticia amewataka Watu wanaoishi na VVU kuwa macho na kuchukua tahadhari zote kutokana na madhara makubwa ya COVID-19, pia amewashauri kuendelea kupata huduma stahiki za VVU katika kipindi chote bila kuathiriwa na Corona huku ikiwataka kutoa taarifa pale wanapoona mabadiliko yoyote katika utoaji na upatikanaji wa huduma za Afya katika maeneo yao.
“Wafanyakazi, Viongozi na Waratibu wa Konga za Baraza hilo, Vikundi wezeshi waendelee kuchukua tahadhari na kuzingatia maelekezo ya Wataalamu wa masuala ya Afya katika mapambano ya janga hili ambalo ni tishio kwa Taifa na Dunia”, ameeleza Bi. Leticia.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa NACOPHA, Deogratius Rutatwa amesema wameotoa tamko hilo baada ya kuwepo mkanganyiko kuhusu janga la COVID-19 kwa Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi zilioenea sehemu mbalimbali.
Rutatwa ametaka Watu wenye VVU kujikinga na janga hilo kutokana na athari zake kuwa kubwa katika jamii, pia amewataka kufuata miongozo ya Serikali katika mapambano dhidi ya Corona.
NACOPHA imeipongeza Serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya COVID-19 pamoja kuiomba na kuishauri kutoa Elimu kwa Makundi mbalimbali kuhusu Janga hilo na chano yake kwa ujumla.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Tanzania (NACOPHA), Bi. Leticia Mourice Kapela akizungumza na Waandishi wa Habari wakati akitoa taarifa juu ya ugonjwa wa COVID-19 kwa Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa NACOPHA, Deogratius Rutatwa (wa kwanza kutoka kushoto) akizungumza na Waandishi kuhusu tamko la Baraza hilo kuhusu ugonjwa wa COVID-19, wa Pili ni Mwenyekiti wa NACOPHA, Bi. Leticia Mourice, wa mwisho ni Naibu Afisa Mtendaji Mkuu wa NACOPHA, Scolastica William
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...