SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO)  mkoani Ruvuma kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) limefanikiwa kusambaza umeme katika vijiji 119 kati ya lengo la kusambaza umeme vijiji 161.

Meneja wa TANESCO Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Florence Mwakasege amesema mradi huo umetekelezwa kupitia REA awamu ya tatu mzunguko wa kwanza ukihusisha pia ujenzi wa njia mbili za umeme wenye urefu wa Kilometa 106 kuelekea kituo cha kufua umeme wa maji Nakatuta Mto Ruvuma.

Amezitaja gharama za mradi huo kuwa ni zaidi ya shilingi bilioni 43 na kwamba vijiji ambavyo bado havijasambaziwa umeme utekelezaji wake upo katika hatua mbalimbali.

Mhandisi Mwakasege amesema tayari wateja 5,902 wa awali wameunganishiwa kati ya lengo la kuunganishiwa wateja 6,178 mradi huo utakapokamilika kwa asilimia 100

Amesema Mkoa wa Ruvuma una jumla ya vijiji 551,kati ya hivyo vijiji vyenye umeme ni 295,vijiji visivyo na umeme vilivyoomba kupitia  REA awamu ya tatu mzunguko wa pili 256 na vijiji vitakavyokuwa na umeme baada ya miradi inayoendelea kukamilika ni 295.

Hata hivyo amesisitiza kuwa hadi kufikia Desemba 2022 vijiji vyote ambavyo havijapatiwa umeme katika Mkoa wa Ruvuma vinatarajiwa kumfikiwa na umeme.

Kuhusu upatikanaji wa umeme mkoani Ruvuma,Mhandisi Mwakasege amesema upatikanaji wa umeme ni wa kuridhisha baada ya Mkoa kuunganishwa na Grid ya Taifa katika Wilaya za Songea,Namtumbo,Mbinga,Nyasa na Tunduru.

“Mkoa wa Ruvuma pia unapata umeme kutoka kwa wawekezaji binafsi wa Kampuni  za Tulila na Andoya ambao wana uwezo wa kufua umeme megawati 5.5 na kuingiza kwenye Grid ya Taifa’’,alisema Mwakasege.

Amewataja wateja waliounganishiwa umeme katika kipindi cha Julai 2020 hadi Machi 2021 kuwa ni 7,411 ukilinganisha na lengo la mwaka la kuunganisha wateja 6,000 sawa na asilimia 123.

Imeandikwa na Albano Midelo

Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma

Julai 8,2021

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...