Na Mwandishi wetu

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) Shaka Hamdu Shaka amesema Chama hicho pamoja na Serikali yake vinatambua na kuheshimu mchango wa vyombo vya habari nchini katika maendeleo ya Taifa.

Shaka amesema hayo leo Agosti 8,2021 na kufafanua Serikali yoyote  duniani, vyama vya siasa, vyama vya kijamii, NGOS na mashirika  hiari ya kijamii na mashirika ya dini ili yafikie  malengo yake kisera, hutegemea kupata msukumo wa nguvu za kitaaluma  na kuungwa mkono na vyombo vya habari.

Akielezea zaidi Shaka aliyefanya ziara ya kutembelea Ofisi za gazeti la Majira amesema tasnia ya habari inapokuwa huru na waandishi wakiandika kwa uwazi, uhalisia na  ukweli na kutumia kalamu zao kwa weledi na maadili husaidia kuharakisha maendeleo. 

"Ni vigumu kwa sekta ya umma au sekta ninafsi kutimiza shabaha zake unapokosekana uhuru wa habari.Chama Cha Mapinduzi tunaheshimu mchango wa vyombo vya habari,tunathamini na tutaendelea kushirikiana nao,lengo letu sote ni kujenga maendeleo ya nchi yetu,"amesema.

Aidha amesema  vyombo vya habari na waandishi wanatakiwa kuzingatia  na kuheshimu sheria za nchi, kufuata maadili, miiko na kanuni za taaluma ya uandishi wa habari unaojenga nchi badala ya kalamu zao kupotosha au kuchochea mifarakano.

Ameongeza CCM kama ilivyoahidi katika Ilani ya Uchaguzi (2020 – 2025) Sura ya 06, Fungu la 125, kitaendelea kuzielekeza Serikali zake kuheshimu tasnia ya habari huku wakiwahimiza  waandishi wa habari kuandika habari  zitakazojenga nchi badala ya zile za kulibomoa Taifa

"Chama kitahakikisha uhuru wa vyombo vya habari unaimarishwa na kulindwa, na kwamba wamiliki na wanahabari wanazingatia maadili na weledi katika kazi zao. Chama kinafurahi pale waandishi wa habari wanapoandika kwa kuzingatia weledi katika tasnia yao baada ya kupata habari kutoka vyanzo ama  mamlaka husika na si habari za kuifarakanisha jamii,"amesisitiza.

Amesema CCM inavikumbusha vyombo vya habari  kutambua vina haki na wajibu wa mashambani na Wafanyakazi viwandani na kwamba kalamu zao zisiache kuandika ukweli kuhusu maendeleo  ya kilimo, mifugo, madini, uwekezaji, afya na jamii ya Watanzania, lakini vikosoe na kurekebisha kama kuna haja ya kufanya hivyo.

Pia vyombo vya habari  viendelee kufichua  na kupiga vita vitendo  vya ufisadi, vikemee ubadhirifu  wa mali za umma, wizi na kushamirisha mapambano  dhidi ya adui rushwa na matumizi mabaya ya madaraka kwa viongozi wa Umma. 

Shaka amesema Chama hicho kitafanya kila linalowezekana kuimarisha vyombo vya habari vya Chama ili vifikishe habari za kisera na kimaendeleo kwa haraka na kwa uhakika katika jamii. Vyombo vya habari na waandishi wa habari  wana kazi na wajibu wa kueleimisha, kufundisha na kuburudisha jamii.

 "Kwa muktadha huo CCM inawataka wanahabari  kutimiza majukumu ya kufichua badala ya kuficha  ukweli kwa kuzingatia maadili na miiko ya kisheria iliyopo.Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza angependa kusikia  habari za kweli zikiwafikia Wananchi kwa haraka mahali popote  walipo mijini au vijijini,"amesema Shaka.

 Kuhusu tofauti kati ya viongozi wao na upinzani vivyo hivyo katika ubora wa muundo na sera CCM amesema chama cha siasa ambacho hakiwezi kuheshimu matakwa ya wanachama,  wananchi na Taifa  hutanguliza maslahi binafsi ya viongozi kuliko maslahi mapama ya umma kama wafanyavyo upinzani na hapo ndipo penye tofauti kati yao na Chama tawala.

Amesema kwanza vyama  upinzani hivyo  ukiacha kuwa ni vichanga, havijawa na uzoefu wa kutosha, viongozi  wake wamepatikana nje ya mifumo yenye kuaminika kwa jamii ikiwemo kutokimbazana na mahitaji ya wakati.

"Mfano Chadema kingelikuwa kinafanya tathmini au tafiti za kisiasa toka kwa wanachama wake na makundi mengine ndani ya umma kutaka kufahamu ni ajenda  ipi ni kipaumbele kwa wakati huu kati ya uchuni na katiba mpya, basi takwimu zingewaonesha kipaumbele namba moja ni uchumi.

"Katika hili tunawakumbusha wakafanye rejea kwenye utafiti wa TWAWEZA sauti za wananchi ambao ulionesha vipaumbele vya wananchi na katika hivyo katiba haikuwepo zaidi wananchi walitaja maji, afya, elimu, rushwa, miundombinu na uchumi. Kutokana na chama hicho kushindwa kufanya  tafiti za msingi zenye kwenda sanjari na mahitaji ya wakati,"amesema Shaka.

Ameongeza kwamba  ndiyo  maana kila wakati  kimekuwa kikijikuta kikishindana na nguvu za upepo kwa mujibu wa  wakati ndio maana hakijui kama uchumi wa watu kwanza na vingine hufuata baadaye."Chama bora na makini hujikita katika tafiti za kitaalam kila mara ili kuweza kufahamu mahitaji ya wananchi na Taifa pamoja na namna nzuri ya kuyafakamilisha. 

" Yanapopishana matakwa na mahitaji ya wakati na kuchomoza  ukaidi wa viongozi hiyo ni dosari na kiashiria kuwa chama husika kimepoteza ushawishi wake na kipo hatarini kuingia makumbusho ya kisiasa. Nguvu ya ushawishi sio uwezo wa kupaza sauti bali ni uwezo wa kuyaishi mahitaji ya wakati kwa njia sahihi,"amesema Shaka.

Aidha amesema  viongozi wasiojiamini kamwe hawawezi kuendeleza  malengo  yao ya msingi na kusisitiza viongozi wasiojiamini hawana moyo wa uvumilivu na subiri, hivyo ni vigumu kumudu migogoro ndani ya vyama wanavyoviongoza. Vyama vya upinzani vina viongozi wa aina hii wasiojiamini ndio sababu migogoro haikomi na vinadumaa.

"Sifa ya CCM ni  bidii, utayari, umoja  wake madhubuti, subira na ustahimilivu. Hayupo anayeweza kutenda na kutekeleza mawazo au fikra zake bila kupatikana uamuzi na msimamo wa  pamoja. Hivyo vikao ni muhimu sana kuliko uwezo binafsi wa mtu. Siku zote CCM huamua mambo yake kwa kutazama mahitaji ya wengi kupitia vikao,"amesema.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...