Benki ya CRDB imezindua upya huduma za CRDB wakala kupitia Shirika la
Posta Tanzania kwa ajili ya kuwawezesha wateja na Watanzania kwa ujumla
kupata huduma za benki hiyo kwa urahisi na unafuu. Hafla ya uzinduzi
ilifanyika katika makao makuu ya Posta jijini Dar es salaam na
kuhudhuriwa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa
Dkt. Faustine Ndungulile pamoja na viongozi mbalimbali wa taasisi hizo.
Akizungumza
katika hafla hiyo, Waziri Ndungulile alisema kuwa ubia huo wa Benki ya
CRDB na Posta utasaidia kuongeza ujumuishi wa kifedha nchini kwa
kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi. Aidha alibainisha kuwa
Serikali kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano imejipanga
kuhakikisha matumizi ya njia mbadala za kutoa huduma za kifedha
yanaongezeka ili kuwafikia wananchi wengi zaidi hususani waliopo
vijijini.
“Nimefurahishwa sana kuona Benki ya CRDB ikiwa mstari wa mbele katika
eneo hili, kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika mifumo ya kidijitali ya
kutolea huduma ikiwamo CRDB Wakala. Niwaombe mkasimamie vizuri ubia huu
ili huduma zinazotolewa zikawe na manufaa kwa Watanzania wengi,” alisema
Waziri Ndungulile.
Waziri Ndungulile aliwataka wananchi kutumia
vizuri fursa hiyo ya CRDB Wakala kupitia Shirika la Posta kupata huduma
za kibenki hasa ukizingatia kuwa shirika hilo lina ofisi katika kila
wilaya nchi nzima.
“Ripoti ya Ujumuishi wa Fedha ya Finscope
inayoonyesha ni asilimia 16.7 tu ya Watanzania wote ambao wanapata
huduma za benki.
Tukiitumia fursa hii vizuri tutakwenda kuongeza idadi
ya watanzania waliounganishwa katika mfumo rasmi wa kifedha,”
alisisitiza huku akizitaka Benki ya CRDB na Shirika la Posta kutoa elimu
ya kutosha juu ya huduma hiyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alimweleza Waziri
Ndungulile kuwa kupitia ubia huo Benki ya CRDB itatumia ofisi zaidi
ya100 za Shirika la Posta kufikisha huduma kwa wateja kutumia mfumo wa
CRDB Wakala.
Alisema uzinduzi wa huduma hiyo ni sehemu ya mkakati wa
Benki ya CRDB kubuni namna bora ya kufikisha huduma kwa wateja ili
kusaidia jitihada za Serikali katika kuongeza ujumuishi wa kifedha.
“Niwakaribishe
wateja wetu wote nchi nzima na hata wale wasio wateja kupata huduma
zetu kupitia Shirika la Posta kwani huduma zote zinapatikana kupitia
madirisha ya CRDB Wakala,” aliongezea Nsekela huku akibainisha kuwa
kupitia ubia huo wateja wataweza kunufaika na huduma nyingi za benki
hiyo ikiwamo kufungua akaunti, kuweka na kutoa fedha, kulipia Ankara,
kulipa tozo na kodi za Serikali, kulipia bima na huduma nyengine nyingi
za kibenki.
Akielezea mafanikio ya CRDB Wakala tokea kuanzishwa kwake mwaka 2013, Nsekela alisema mpaka sasa Benki hiyo ina zaidi ya mawakala 20,000 waliosambaa kote nchini mijini na vijijini. Alibainisha zaidi kuwa mfumo huo umesaidia kupunguza gharama ya kufikisha huduma kwa wateja lakini pia kutoa ajira kwa watanzania na hivyo kukuza kipato cha wananchi.
Akielezea mafanikio ya CRDB Wakala tokea kuanzishwa kwake mwaka 2013, Nsekela alisema mpaka sasa Benki hiyo ina zaidi ya mawakala 20,000 waliosambaa kote nchini mijini na vijijini. Alibainisha zaidi kuwa mfumo huo umesaidia kupunguza gharama ya kufikisha huduma kwa wateja lakini pia kutoa ajira kwa watanzania na hivyo kukuza kipato cha wananchi.
“Ninajivunia kusema tumepata mafanikio makubwa sana kupitia
mfumo huu wa CRDB Wakala, sasa hivi zaidi ya asilimia 40 ya miamala ya
wateja hufanyika kupitia CRDB Wakala kulinganisha na matawi,” alisema
Nsekela.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Posta,
Bwana Macrice Mbodo alimhakikishia Waziri Ndungulile kuwa shirika lake
limejipanga kikamilifu katika kuhakikisha malengo ya ubia huo ya
kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki kwa wananchi yanafikiwa.
Alisema ubia huo utakua na manufaa kwetu kwao kwa kuwezesha kupata
kamisheni, hivyo kuwa sehemu ya vyanzo vya mapato vya shirika.
“Tunajivunia
kuwa sehemu ya suluhisho la upatikanaji wa huduma za kifedha kwa
wananchi. Nikuahidi Mheshimiwa Waziri tutasimamia vizuri utoaji wa
huduma kwa wateja ili kuhakikisha wanapata pia kutoa huduma kwa urahisi
na haraka,” alisema Mbodo huku akiishukuru Benki ya CRDB kwa mafunzo
ambayo wameyatoa kwa wafanyakazi wa shirika ili waweze kutoa huduma kwa
weledi wa hali ya juu.
Mkurugenzi wa Mawasiliano Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa akizungumza katika hafla hiyo ya uzinduzi wa huduma za CRDB Wakala kupitia Shirika la Posta
Mkuu wa Kitengo cha CRDB Wakala, Ericky Willy akiwasilisha mada kuhusu huduma zinazopatikana kupitia madirisha ya CRDB Wakala katika ofisi za Shirika la Posta
Msanii Mrisho Mpoto akitumbuiza wakati wa uzinduzi huo
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...