Na Zainab Nyamka, Michuzi TV
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dk Faustine Ndugulile amezitaka taasisi kuwatumia watendaji waliomaliza muda wao kujifunza na kushirikiana nao ili kuleta mabadiliko.
Hayo ameyasema katika kikao kazi cha Mameneja wa Mikoa na Watendaji wa Shirika la Posta Tanzania (TPC) chenye lengo la kutoa mafunzo ili kuboresha huduma.
Dk Ndugulile amesema, ili taasisi au Shirika lifike mbali lazima watendaji waipe thamani nembo na iwe inavutia kwa wateja.
“Tanzania ya sasa ina vijana wengi sana kuliko wazee lazima nembo ya Shirika la Posta ivutie tuipe thamani ‘Brand’ tutoke katika mfumo uliopo na twede kidigitali,” amesema Dk Ndugulile.
Amesema, anataka fedha zinazopatikana ndani ya Shirika zitumike katika mabadiliko na Posta iwe ni kitovu cha biashara.
“Tunataka kuwekeza katika mfumo wa utoaji huduma kwa ubora na kufika kimataifa ili kushindana na nchi mbalimbali duniani.” Amesema.
Dk Ndugulile ameongeza kuwa, Shirika la Posta limekuwa na mabadiliko ya kiutendaji, muonekano na malengo na amewataka kuendelea kusimamia rasilimali za Shirika na kuendelezwa vizuri.
Aidha, Dk Ndugulile amesema kikao kazi cha Mameneja na watendaji wa Shirika la Posta Tanzania kitaleta tija na watakuwa na malengo sawa yatakayosimamia fursa, ubunifu na masoko.
Akizungumzia mashirikiano ya kiutendaji, Dk Ndugulile amesema anawapongeza taasisi zote ambazo ziko chini ya Wizara yake kwa ushirikiano wanaoufanya kiutendaji na hilo linaleta chachu ya mabadiliko.
Kwa upande wa Kaimu Postamasta Mkuu Macrice Mbodo amesema kikao kazi wa watendaji wa Shirika hilo kitaangaalia katika mambo makuu nane ambayo ni muhimu.
Mbodo amesema katika kikao hicho wataangalia zaidi mafunzo ya kiungozi, kupata uzoefu wa pamoja kutoka taasisi nyinginezo. Kupata mafunzo ya vitendo kutoka EGA ili kuweza kutumia mifumo ya kiserikali na usalama na utunzaji wa siri.
Aidha, Mbodo amesema kuongeza uelewa kupitia mifumo mbalimbali ya tehama , tathmini ya shirika na kupata mafunzo kutoka Ofisi ya waziri Mkuu.
Kikao hicho cha siku tano kimewakutanisha mameneja wa mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar, Watendajj kutoka Makao Makuu ya Posta ambapo watapata mafunzo hayo kutoka taasisi mbalimbali za kiserikali ikiwemo Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA.)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...