Raisa Said,Tanga.


Wajumbe wa  Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT) Mkoa wa Tanga wameazimia kwa pamoja kupeleka Ombi la Kuongezewa Posho ya Madiwani kutoka  sh laki 350/= wanazolipwa sasa hadi kufikia  Milioni moja ( 1,000,000/=)  lengo likiwa ni kuboresha maslahi ya wawakilishi hao wa wananchi ngazi ya kata.

Wakizungumza katika kikao cha Kwanza cha Jumuiya hiyo kilichofanyika katika ukumbi wa Jiji la Tanga ,walisema posho wanayolipwa sasa haitoshelezi mahitaji ukilinganisha na majukumu waliyonayo.

Hoja nyingine watakayopeleka katika Mkutano wa Alat Taifa utaofanyika hivi karibuni  ni kutaka kuwe na Mfuko wa Kata kama ilivyo Mfuko wa Jimbo ili kuweza kuchochea maendeleo kwa wananchi sababu madiwani wanamajukumu mengi na ndio wanakwenda hadi kwenye vitongoji kuhimiza shughuli za maendeleo.

Madiwani nao wanatakiwa kuangaliwa maslahi yao kwa mapana ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi na heshima tofauti na sasa, kwani wameonekana wanapata heshima kubwa kwa kuitwa waheshimiwa, lakini kwenye maslahi wanazidiwa na watendaji wa vijiji"Alisema Diwani CHewaja

Diwani wa Kata ya Tanganyika, Wilaya ya Muheza Shafii Chewaja alisema Diwani amekuwa anafanya kazi kwenye mazingira magumu nakwamba hata pesa anazotumia Iasilimia 80 ni pesa yake ya mfukoni, hivyo umefika wakati diwani apewe sh. milioni moja kwa mwezi badala ya 350,000.

Diwani wa Kata ya Nguvumali ambaye pia ni Mstahiki Meya Mstaafu wa Jiji la Tanga Mustapha Seleboss, alisema wanaomba posho ya mwezi ya diwani ifanane na hadhi yao, kwani huenda baadhi ya migogoro ama kutoheshimiana kati ya madiwani na watendaji, inatokana na posho ndogo ya madiwani.

Diwani wa Viti Maalumu Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Mwanaid Gogo alisema madiwani wanafanya kazi nyingi kwenye jamii ikiwemo kuwasaidia wagonjwa kufika kituo cha afya ama hospitali ya wilaya kwa kuwapa nauli. Lakini pia kama madiwani waliotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wana jukumu la kuwasaidia nauli viongozi wa chama ngazi ya kata na vijiji kwenda wilayani zaidi ya kilomita 60.

"Tunadharauliwa na watendaji wa vijiji kuwa huyu ni mtu wa maneno tu, lakin kwenye mshahara hawatuzidi. Sisi kila siku tunagongewa milango na wananchi wenye shida wakitaka kusaidiwa kwa shida mbalimbali ikiwemo zinazohitaji fedha. Bado viongozi wa chama wakienda wilayani karibu kilomita 60, unatakiwa umpe nauli " alisema Gogo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga Amani Kasinya alisema anaomba Serikali Kuu na wabunge kuweza kuwatetea madiwani, kwani kwenye Uchaguzi Mkuu wao ni sehemu ya wagombea wanaopigiwa kura, hivyo baada ya kupita kwenye uongozi, waendelee pamoja badala ya kuwaacha njiani.

"Kwenye iyena iyena (Kampeni za Uchaguzi Mkuu) tupo mafiga matatu, lakin baada ya ushindi, figa moja linapigwa teke. Ndiyo najiuliza ni kwa nini niliemsaidia ashinde (Mbunge), posho yangu ya mwezi yeye ni posho yake ya kikao chake cha siku moja. Mwenyeviti wa Halmashauri kupewa gari kwenda kwenye msiba ni hisani ya Mkurugenzi, itategemea siku hiyo Mkurugenzi ameamkaje. Lakin sifa anazopewa Mwenyekiti utasikia, Mwenyekiti hii ni Halmashauri yako, wewe ndiyo mkubwa na ndo Kila kitu kwenye Halmshauri"alisema Kasinya

Makamu Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Meya wa Jiji la Tanga Abdulrahamn Shiloow alisema nia yao ni kuunganisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa (MSM) na Serikali Kuu ili kuona zinafanya kazi kwa ushirikiano na uwajibikaji wa pamoja, kwani kama hawatafanya kazi kama timu moja, watashindwa kufanya kazi kwa ufanisi.

Shiloow ambaye ametangaza nia ya kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa ALAT Taifa kwenye uchaguzi ujao, amewataka madiwani na watendaji kwenye MSM kufanya kazi kwa nidhamu, uwajibikaji na kuheshimiana ambako kutaleta ufanisi kwenye utendaji wa kila siku.

Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Tanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Sadick Kallaghe aliunga mkono hoja ya kuanzishwa Mfuko wa Kata, kwani mfuko huo utaongeza nguvu kwenye miradi ya maendeleo ambapo fedha hizo zitaweza kupunguza kero ndogo ndogo za wananchi kama kumalizia ujenzi wa vyoo vya shule, kukamilisha ujenzi wa ofisi za vijiji, vitendea kazi (shajala) za ofisi na miradi ya wananchi.

"Jimbo la Korogwe Vijijini kwa mwaka linapokea sh. milioni 57 za Mfuko wa Jimbo. Kwa jimbo lenye Kata 29, vijiji 118, vitongoji 610 na Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mombo, fedha hiyo sh. milioni 57 haitoshi. Diwan ambaye ana jimbo dogo angalau angepewa fedha sh. milioni tano hadi 10 ili awe na uwezo wa kununua mifuko 10 ya saruji kwa wananchi wake, pia ingesaidia kusaidia na Mfuko wa Jimbo kuleta maendeleo ya haraka.

Pia alisisitiza posho ya madiwani kwa sasa haitoshi. Posho hiyo kwa sasa ni sawa na sh. 11,000 kwa siku. Tunataka iwe 30,000 kwa siku sawa na sh. milioni moja kwa mwezi. Posho hiyo itaongeza ari ya utendaji kwa madiwani na kuweza kuhudumia jamii yao kwa mapana zaidi," alisisitiza Kallaghe.

Kallaghe ambaye pia anagombea Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ALAT Taifa, alisema mapato ya halmashauri ndiyo uti wa mgongo, hivyo Wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri, washirikiane na madiwani na watendaji kuona mapato ya ndani ya halmashauri yanakusanywa  ili kufikia azma hiyo ni lazima kuwe na uadilifu katika kukusanya mapato hayo.




 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...