Na John Walter-Manyara
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Elim Pentekoste Tanzania, Peter Konki amewaomba Watanzania kila mmoja kwa nafasi yake kufanya maombi kwa ajili ya taifa la Tanzania na rais Samia Suluhu Hassan Mungu aweke walinzi juu ya ufahamu wake ili uamuzi atakaoufanya katika nchi uwe wa busara na wenye tija kwa wote.
Katika maombi hayo alimuombea Rais Samia kuwa Mungu amsaidie, atekeleze majukumu yake katika hali ya busara kubwa na hali ya utulivu mwingi.
“Tumuombee Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan,nyinyi nyote mnajua mwanamke ni mtu wa busara katika kutekeleza majukumu yake na ni mtu wa kujihadhari hapendi kukosea” alisisitiza Askofu Konki.
Askofu Konki ametoa kauli hiyo katika maazimisho ya Jubilei ya miaka 75 ya kanisa hilo hapa nchini ambalo lilianza mwaka 1946.
Askofu Konki akizungumza na mamia ya waumini wa kanisa hilo kutoka maeneo mbalimbali ya nchi ya Tanzania pamoja na wakazi wa mkoa wa Manyara katika uwanja wa Kwaraa mjini Babati, amesema katika miaka 75 ya kanisa hilo wamefanikiwa kuwajenga watu kiimani pamoja na kuisadia serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo kwenye Afya na Elimu.
Aidha ametoa wito kwa serikali ya chama cha Mapinduzi kuendelea kuwa sikivu katika kuwatumikia wananchi na kutoa maamuzi yasiyoumiza.
Amesema waelewe kuwa ni vizuri kuwasikiliza wananchi kwani wanalalamika juu ya tozo za simu zilizopo kwa sasa.
“Wananchi wakilalamika mioyoni watakuwa adui wa serikali kitu ambacho hakipendezi” alisema Askofu Konki.
Ametoa wito kwa wale walio karibu na wananchi na wanaomshauri rais kuwa wawajali watu wao kwa kuwasaidia ili waendelee kuipenda nchi yao inayoongozwa na chama cha Mapinduzi.
Aidha ametoa wito kwa viongozi wa juu wa chama cha Mapinduzi kuacha kuwashambulia kwa namna yeyote mtu au watu wanapoishauri au kuikosoa serikali kwa kuwa ni njia mojawapo ya kujenga nchi kwa pamoja.
Amesema wataendelea kukipenda chama cha Mapinduzi na serikali yake na kuendelea kuiombea nchi Amani iendelee kudumu lakini isikilize wananchi wake.
Katika hatua nyingine Askofu Konki amezindua mkakati maalum wa kutimiza malengo ya kanisa hilo.
Naye mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange amesema serikali itaendelea kushirikiana kwenye masuala mbalimbali na kanisa hilo huku akiwaahidi kuwapa nafasi ya ujymbe katika kamati maalum iliyoundwa wilayani hapo kukabiliana na ugonjwa wa Uviko 19 kwa kuwaelmisha wananchi kuchukua tahadhari na umuhimu wa wa chanjo ya uviko 19 ambayo inatolewa katika vituo mbalimbali vya afya nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...