Na Mwandishi Wetu, DSM
 
Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi amefungua Mashindano ya Ulimwende ya Vyuo Vikuu (Miss High Learning 2021) usiku wa Septemba 25, 2021 na kuwahakikishia washiriki na wadau wote wa urembo kuwa Serikali itaendelea kusimamia na kuboresha eneo la sanaa ya urembo ili kuibua vipawa na vipaji vya wasanii hatimaye  waweze kunufaika.
 
Dkt. Abbasi ameyasema hayo kwenye hafla ya ufunguzi wa mashindano hayo iliyofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es salaam ambapo amesisitiza kuwa urembo ni sanaa muhimu inayotoa ajira duniani hivyo washiriki wake wanatakiwa kujiamini na kuzingatia maadili ya taaluma  hiyo ili waweze kufika  mbali  na kunufaika nayo. 
 
“Mashindano ya urembo kwa Vyuo Vikuu ni miongoni mwa mashindano makubwa hapa nchini hivyo sisi kama Wizara inayosimamia Sekta ya Sanaa tumejipanga vizuri kushirikiana na waandaaji ili kuyapa heshima inayostahili”. Amefafanua Dkt. Abbasi
 
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuinua Sekta ya Sanaa nchini na ndio maana imeweka mikakati mbalimbali ya kuwasaidia wasanii ikiwa ni pamoja na kuwaanzishia Mfuko maalum wa Maendeleo ya Sanaa ambao utatumika kuwawezesha wasanii kwenye kazi zao.
 
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha mapenzi makubwa katika sanaa na michezo ametoa kiasi cha shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa na Utamaduni,” Amesisitiza Dkt. Abbasi.
 
Kwa mujibu wa Dkt. Abbasi michango mikubwa iliyotolewa na Serikali katika kipindi hiki kwenye tasnia ya Sanaa na michezo ni pamoja na kutenga kiasi cha shilingi Bilioni 9.5 kwa ajili ya kujenga viwanja vya  wazi vya michezo kwa ajili ya wasanii na wanamichezo.

Pia amesema Serikali inakusudia kujenga ukumbi wa kisasa (Arts & Sports Arena) utakaokuwa na uwezo wa kuchukua zaidi ya watu  elfu kumi na tano kwa mara moja kwa ajili ya kusaidia kuweka michezo mbalimbali kwenye ukumbi huo ambapo amefafanua kuwa michoro ya ukumbi huo ipo mbioni kukamilika na ikikamilika itapelekwa kwenye mamlaka husika kwa ajili ya hatua zaidi.

Ameongeza kuwa katika kuboresha miundombinu ya michezo ikiwemo sanaa Serikali imesamehe kodi ya nyasi bandia za viwanja vya michezo na kutaka asilimia tano ya mapato ya kwenye michezo ya kubahatisha  kwenda katika mfuko wa kuendeleza michezo hapa nchini.
 







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...