Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 26 Septemba, 2021 amewasili Jijini Dodoma akitokea Jijini Dar es Salaam na kupokelewa na wananchi wa Jiji hilo wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Anthony Mtaka, Mawaziri, Wabunge mbalimbali pamoja na Madiwani.
Mhe. Rais Samia amewashukuru wananchi wa Jiji la Dodoma kwa kujitokeza kwa wingi kumpokea na kueleza kuwa mbali na kuhudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lakini pia imemuwezesha kukutana na Marais wenzake na Wakuu wa Taasisi mbalimbali na kuahidiwa kuwa wapo tayari kufanya kazi na Serikali ya Tanzania katika kuwaletea Wananchi maendeleo.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema katika kipindi cha miezi sita tangu Serikali ya Awamu ya Sita kuingia madarakani idadi ya wawekezaji na wafanyabiashara wameongezeka kwa kiwango kikubwa hivyo kuchochea kasi ya maendeleo.
Mara baada ya kuwasili Chamwino, Mhe. Rais Samia amepokelewa na wakazi wa Wilaya hiyo ambao walimkaribisha rasmi kama mkazi mwenzao na kumpatia zawadi ya Ng’ombe wa maziwa, kumvika mavazi ya kimila na kumkabidhi Ngao na Mkuki kama ishara ya Kinga na Ulinzi wa Nchi.
Mhe. Rais Samia amewahakikishia wananchi hao kuwa atahakikisha anazitatua changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na zile zilizoahidiwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais Samia ameahidi wananchi hao kuwa Serikali itaboresha huduma za jamii ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, madarasa ya wanafunzi pamoja na kuwajengea Soko la biashara.
Mhe. Rais Samia amewaomba wananchi wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla kuendelea kudumisha amani ili kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo na kukuza uchumi wa nchi.
Jaffar Haniu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.
Mzee wa Kimila wa Kabila la Kigogo Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma Bw. Goden Wenga akimkabizi Ngao na Mkuki Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kama ishara ya ukaribisho mara baada ya kuwasili Chamwino Ikulu akitokea Jijini Dar es salaam leo Sept 26,2021. PICHA NA IKULU
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akisalimiana na Wananchi wa Wilaya ya Dodoma Mjini waliofika kumpokea
katika eneo la Chinangali mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege
wa Dodoma akitokea Jijini Dar essalaam leo tarehe 26 Septemba ,2021.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,
akivalishwa Vazi la Kimila na Wazee wa Kimila wa Kabila la Kigogo wenye
asili ya Dodoma Wilayani Chamwino kama ishara ya ukaribisho mara baada
ya kuwasili Chamwino Ikulu akitokea Jijini Dar es salaam leo Sept
26,2021.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...