Aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi, Dkt. Leonard Chamuriho, amesema Wizara hiyo imeendelea kutekeleza kwa mafanikio Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka mitano (2021/22 - 2025/26) kwa kukamilisha miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa madaraja makubwa Tisa.
Akizungumza wakati wa kumkabidhi ofisi Waziri mpya wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa jijini Dodoma leo, Dkt. Chamuriho ameyataja madaraja yaliyokamilika kuwa ni daraja la Magufuli (Kilombero), Nyerere (Kigamboni -Dar es Salaam), Magara (Manyara), Kavuu (Katavi), Mlalakuwa (Dar es Salaam), Momba (Rukwa), Lukuledi (Lindi), Mara (Mara) na Sibiti mkoani Singida.
Aidha, Dkt. Chamuriho amesema daraja jipya la Selander, daraja la Msingi (Singida), daraja jipya la Wami, Kitengule, Ruhuhu na Kigongo – Busisi, ujenzi wake unaendelea na uko katika hatua nzuri.
“Kuhusu usafiri wa anga, jumla ya ndege 11 zimenunuliwa na tayari mkataba wa ununuzi wa ndege nyingine mpya tano umeshafanyika”, amesisitiza.
Naye Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amemuomba aliyekuwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho kuendelea kushirikiana na Wizara hiyo, ili kuwatumikia vyema watanzania.
Aidha, alimuelezea Dkt. Chamuriho kuwa ni kiongozi makini, mwenye utaalamu na ambaye amefanya mambo makubwa nchini kwa weledi ili kuhakikisha Watanzania wanapata miundombinu iliyo bora.
"Siwezi kuandika historia yangu bila kukutumia, tumetatua changamoto nyingi za Wizara hii hususani Sekta ya Uchukuzi tukiwa pamoja, hivyo nakuomba tuendelee kusaidiana kuwatumikia Watanzania," amesisitiza Prof. Mbarawa.
Makabidhiano hayo ya Ofisi yanafuatia mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri yaliyofanywa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...