Muonekano wa mradi wa ujenzi wa jengo la makazi na biashara linalojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), jijini Arusha, ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 80. Jengo hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kuhudumia kaya 22 na ujenzi wake unagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 5.2.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya, akikagua mradi wa ujenzi wa jengo la makazi na biashara linalojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania, jijini Arusha. Kulia ni Kaimu Meneja TBA mkoa wa Arusha Eng. Juma Dandi.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), mkoa wa Arusha Eng. Juma Dandi, akimuonesha mandhari ya nje Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya, wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la makazi na biashara linalojengwa na kusimamiwa na wakala huo jijini Arusha.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), mkoa wa Arusha Eng. Juma Dandi, akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa jengo la makazi na biashara kwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya, wakati alipofanya ziara ya ukaguzi wa miradi inayoendelea ya Wakala huo, jijini Arusha.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya, akitoa maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), mkoa wa Arusha Eng. Juma Dandi, wakati akikagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo la makazi na biashara, jijini Arusha.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
********************************
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya, ameuagiza Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kukamilisha mradi wa ujenzi wa jengo la makazi na biashara linalojengwa na wakala huo mkoani Arusha haraka iwezekanavyo ili liweze kutoa huduma kwa watumishi na kuongeza mapato ya wakala huo na kwa Taifa.
Eng. Kasekenya amesema hayo jijini Arusha, wakati akikagua maendeleo ya mradi ujenzi wa jengo hilo ambalo litakuwa na uwezo wa kuhudumia kaya 22 pindi litakapokamilika na kuupongeza Wakala huo kwa kuwa wabunifu kwa kuongeza majengo ya kibiashara hasa katika majiji makuu.
“Niwapongeze kwa kuwa wabunifu kwani matunda haya ni matokeo ya mapato yenu ya ndani, hivyo hakikisheni mnalikamilisha jengo hili mapema zaidi na kuanza ujenzi wa majengo mengine mengi zaidi katika majiji kwani mahitaji ni makubwa sana”, amesema Naibu Waziri Kasekenya.
Aidha, ameutaka Wakala huo kuweka kipaumbele katika mji mkuu wa Serikali wa Dodoma kwa kuanza kujenga majengo ya viongozi, watumishi pamoja na ya kibiashara kwa ajili ya kukodisha kwa watu binafsi ili kuongeza mapato yao ya ndani.
Naibu Waziri huyo amewaasa wafanyakazi kazi wa TBA kuongeza kasi ya utendaji kazi kwa umakini, kujituma, uaminifu na kuwa wabunifu kila siku ili kuongeza vyanzo vya ndani vya mapato.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Wakala wa Majengo nchini (TBA), mkoa wa Arusha Eng. Juma Dandi, amesema kuwa jengo hilo linakusudiwa kutoa makazi kwa watumishi wa umma ili kupunguza pengo lililopo la mahitaji halisi ya makazi kwa watumishi wa umma mkoani humo.
Amefafanua kuwa jengo hilo linagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 5.2 ambapo ujenzi wake mpaka sasa umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2022.
Mradi wa ujenzi wa jengo la makazi na biashara uliopo mkoani Arusha ni moja ya mikakati ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), katika kutoa huduma ya nyumba za kupanga kwa watumishi wa umma pamoja na kuongeza pato kwa wakala huo
Mhandisi Kasekenya yuko mkoani Arusha kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali inayosimamiwa na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...