WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais wa awamu ya sita Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuwatumikia, kuwahudumia na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi kwa ajili kuboresha maendeleo yao.
Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Mheshimiwa Samia anataka kuona kila Mtanzania anapata huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za afya, elimu, maji, nishati ya umeme na miundombinu katika maeneo yao ya makazi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Septemba 24, 2021) wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Ndungu wilayani Same, Kilimanjaro baada ya kukagua maboresho ya kituo cha Afya cha Ndungu akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.
“Wajibu wetu sisi wasaidizi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kutekeleza maelekezo ya Rais Mheshimiwa ambaye anataka kuona huduma za kijamii zikiwafikia Watanzania. Tumejipanga na tutahakikisha huduma mbalimbali zinaendelea kuimarishwa na kuboreshwa zikiwemo za afya.”
Mheshiwa Majaliwa amesema ujenzi wa miradi ya vituo vya afya nchini umeboreshwa ambapo kwa sasa vinauwezo baada ya kujengwa majengo ya kutolea huduma za upasuaji, mama na mtoto, maabara, wodi za kulaza wanaume na wanawake pamoja na chumba cha kuhifadhia maiti.
Amesema kuwa katika kipindi cha kuanzia Machi, 2021, Rais Mheshimiwa Samia ametoa shilingi bilioni 3.74, ambapo Julai, 2021 ameongeza tena shilingi bilioni 2.8 kwa ajili ya kuimarisha vituo vya afya, zahanati, ununuzi wa madawa na vifaa tiba mkoani Kilimanjaro.
Pia, Waziri Mkuu amewataka wakazi wa maeneo hayo waendelee kushirki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ikiwemo kilimo cha .zao la mpunga na mkonge. “Ninyi ni wachapakazi, kilimo cha mkonge kinalipa, nimeona mkenge unastawi vizuri huku, limeni mkonge mpate pesa.”
Akiwa katika Kituo cha Afya cha Ndungu, Waziri Mkuu alipokea taarifa ya maboresho ya kituo hicho iliyowasiliwa na Mganga Mfawidhi wa kituo hicho Dkt. Tatizo Mwakatuya ambaye pamoja na mambo mengine alielezea changamoto zinazokikabili kituo hicho ikiwemo ya upungufu wa madaktari pamoja na jokofu la kuhifadhia maiti.
Kufutia taarifa hiyo, Waziri Mkuu alimuelekeza Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima ahakikishe daktari wa upasuaji anapelekwa haraka kituoni hapo kwani kwa sasa kituo hicho kina daktari mmoja tu wa upasuaji. Pia alielekeza lipelekwe jokofu la kuhifadhia maiti.
Kwa upande wake, Zaina Bakari ambaye amelazwa katika wodi ya wazazi baada ya kujifungua kituo hapo, ameishukuru Serikali na kumpongeza Rais Mheshimiwa Samia kwa kuboresha huduma za afya.”Hapa huduma zinatolewa bure na ni nzuri na kama zitaendelea hivi mambo yatakuwa mazuri sana.”
Pia, Mheshimiwa Majaliwa alikagua chanzo cha mradi wa maji Mwanga-Same-Korogwe katika eneo la Nyumba ya Mungu wilayani Mwanga ambapo ameuagiza viongozi wa Wizara ya Maji wahakikishe mradi huo unakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma hiyo kama ilivyokusudiwa.
Mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya maji inayotekelezwa na Serikali kwa takribani shilingi bilioni 600 kwa lengo la kumaliza kero ya maji kwa wakazi wa wilaya za Same, Mwanga na Korogwe. Jumla ya wananchi wapatao 438, 931 wanatarajiwa kunufaika na mradi huo mara utakapokamilika.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Ndungu katika Jimbo la Same Mashariki, Tatizo Mwakatuya (wa tatu kulia) wakati alipotembelea chumba cha upasuaji cha kituo hicho, Septemba 24, 2024. Wa pili kulia ni Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wa Kata ya Ndungu
katika Jimbo la Same Mashariki baada ya kukagua maboresho ya Kituo chao
cha Afya akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro, Septemba 24,
2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Zaina Bakari wakati alipotembelea
wodi ya wazazi kwenye Kituo cha Afya cha Ndugu katika Jimbo la Same
Mashariki, Septemba 24, 2021. Bibi Zaina amejifungua mtoto wa kiume
katika kituo hicho. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...