Na Munir Shemweta, KONDOA
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC) limesema limeanza kufanya ukarabati wa nyumba zake katika maeneo mbalimbali nchini ili ziwe katika ubora.
Hayo yalibainishwa leo tarehe 21 Sept 2021 wilayani Kondoa mkoani Dodoma na Meneja wa Kitengo cha Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa Muungano Saguya Dodoma wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa huo.
"Shirika letu la NHC lilianzishwa mwaka 1964 na sasa tumeanza kuzifanyia ukarabati nyumba zetu katika maeneo mbalimbali zikiwemo zile za Dar es Salaam ambapo kuna asilimia 60 ya nyumba zote za shirika" alisema Saguya
Kwa mujibu wa Saguya, NHC ina takriban nyumba 18,000 nchi nzima zinazotumika kwa shughuli za biashara na makazi na ukarabati unaofanyika utasaidia nyumba hizo kuwa na ubora na muonekano mzuri wa kuvutia.
Hata hivyo, Meneja huyo wa Kitengo cha Habari na uhusiano NHC aliongeza kuwa, pamoja na ukarabati wa nyumba zake unaoendelea shirika la NHC linadai takriban shilingi bilioni 26 kutoka kwa wapangaji wake na kuwataka wote wanaodaiwa kuhakikisha wanalipa madeni yao kwa wakati ili fedha hizo zitumike kuendesha miradi mingine ya Shirika.
Saguya alibainisha kwa kusema, Shirika la Nyumba la Taifa, kwa sasa linaendelea na miradi yake ya ujenzi wa nyumba za kuuza na zile za kupangisha kwenye mkoa wa Dodoma na sasa linakamilisha mradi wa nyumba 300 eneo la Iyumbu na nyumba 100 eneo la Chamwino.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema, katika kuwezesha ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kabla kuanza ujenzi shirika la nyumba linatakiwa kufanya mawasiliano na taasisi kama TARURA, Maji na TANESCO ili kusaidia uwezeshaji miundo mbinu katika eneo la mradi.
Alibainisha kuwa, NHC kwa sasa inajenga nyumba kwa wanaohitaji kulingana na chaguo la mteja hivyo ni fursa kwa halmashauri kulitumia shirika katika miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...