Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
CHAMA Cha Mapinduzi( CCM) kupitia Katibu wake wa Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka kimesema kitaendelea kuweka misingi imara ya kuendeleza sanaa nchini na kuwahakikishia wasanii wanathamini na kuendelezwa.
Akizungumza kupitia Jukwaa la Wasanii liloandaliwa na Kampuni ya Marketing Africa mkoani Dar es Salaam,Shaka amsema Serikali inadhamira njema ya kukuza na kuwathamini wasanii huku akifafanua Rais Samia Suluhu Hassan ameanzisha Wizara maalum ya Sanaa na utamaduni.
"Lengo likiwa ni kushughulikia changamoto za wasanii zilizopigiwa kelele kwa muda mrefu.Kupitia hotuba ya Rais Samia katika Baraza kuu la umoja wa mataifa, ameeleza suala la sanaa kwa sasa litachukua mkondo mpya katika uwanja mpana wa kimataifa,"amesema.
Shaka amesema sasa wasanii wa Tanzania watashirikiana na wasanii wengine wa duniani katika uwekezaji mkubwa katika sanaa kupitia sera ya diplomasia ya uchumi.
"Tuitumie sanaa kama silaha ya ukombozi wa matatizo ya kijamii na kamwe isiwe chanzo cha mfarakano na vurugu kwani Tanzania ni nchi Tajiri, yenye rasilimali za kila aina, na rasilimali namba moja ni vipaji tulivyonavyo hivyo Wasanii wakiamua wataweza , kila mmoja wetu ana jukumu la kufanya sanaa yake kwa bidii na maarifa,"amesema na kuongeza.
"Huu ni wakati wa Suluhu, hivyo wasanii wawe wazi kuacha kufanya sanaa kwa mazoea,katika zama tulizonazo, kazi ya sanaa imegeuka kuwa kimbilio kubwa kwa vijana kama sehemu ya soko la ajira hivyo ni wajibu wetu wasanii kuhakikisha kuwa imani ya Jamii kwetu inaendelea kwa kulinda mila, desturi na utamaduni wetu,"amesema.
Jukwaa ili limeandaliwa kwa lengo la kutoa elimu ya masoko, uzalishaji bora wa kazi sanaa sambamba na kutoa ushauri wa kibiashara.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...