Mwandishi,Michuzi TV
TAASISI ya Taasisi ya Doris Mollel Foundation imekabidhi msaada wa vifaa tiba mbalimbali katika hospitali ya Maswa mkoani Simiyu kwa ajili ya kuwahudumia na kuwalea watoto wanaozaliwa kabla ya wakati(Njiti) hatua itakayosaidia kupunguza safari za watoto kupelekwa Bugando kwa ajili ya kuhidhiwa na kupewa huduma.
Msadaa una thamani ya zaidi Sh.milioni 50 umetolewa na taasisi hiyo akishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo Benki ya NCBA ambao wamekuwa bega kwa bega na Doris katika jitahada hizo za wakusaidia watoto njiti.
Miongoni mwa vifaa tiba hivyo ni mashine mbili za kupumulia,mashine za kusaga nafaka ili kuleta ahueni kwa kina mama wanaohudumia watoto katika hospitali, magodoro, runinga, vitanda na mashuka
Msaada wa vifaa utasaidia kupunguza hali ya kuwasafirisha watoto kwa njiti kutoka Maswa hadi Bugando kwa ajili ya matibabu kwa kuwa watakuwa na vifaa vyao kuwalea watoto hao.Awali vifaa hivyo vilipatikana Buģando kwa sasa vitapatikana Maswa na kusaidia mkoa wote wa Simiyu.
Akizungumza wakati wa tukio la kukabidhiwa kwa vifaa hivyo, Mkurugenzi wa Doris Mollel Foundation Doris Mollel amesema anamshukuru Mungu kwa kuumpa kibali cha kuwawahangaikia watoto waliozaliwa kabla ya wakati ili nao waweze kuishi kama watu wengine.
"Najua kazi hii ni ya Serikali kupitla Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto lakini sisi wadau ambao tuko katika mashirika yasiyo ya kiserikali tunafanya kazi kupitia miongozo yao na tunafurahi kuwa hapa Maswa kuchangia vifaa hivi kwa ajili ya watoto Njiti ambavyo vitaleta auheni kwa watoto hao,"amesema Mollel.
Kwa upande wake Meneja NCBA tawi la Mwanza Doreen Lushiba ambaye taasisi yake ilichangia sehemu ya msaada huo amesema wameamua kuwasaidia watoto hao ili kupunguza vifo vinavyotokana na kukosa mahitaji mahimu katika malezi na matibabu huku akiwashauri wadau wengine kuunga juhudi hizo.
" Tumetoa msaada wa mashuka katika wodi ya kina mama wanaojifungua watoto njiti.Hii ni njia mojawapo ya kurudisha kwa jamii tunachokipata pia ni sehemu ya kuisadia Serikali kuboresha huduma za afya," amesema.
Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Maswa Dk.Mporwa Dorati kati ya watoto 25 wanaozaliwa hospitalini hapo kwa mwezi nusu yao ni watoto njiti hivyo changamoto ya kuwalea ipo na uhitaji wa vifaa tiba ni mkubwa.
"Tumepokea baadhi ya vifaa kutoka kwa wafadhiri, kwa sasa tutakuwa na changamoto ya majengo kwa ajili ya kuweka vifaa hivi tulivyo vipokea" alisema Dk.Mpolwa.
Aidha ameongeza kwa sasa wameanza kupanua jengo la wodi ya wazazi ili kuweka vifaa hivyo katika wodi hiyo ili viendelee kutoa huduma kwa watoto wanaozaliwa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...