Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) limewahimiza Watanzania waishio nje ya nchi  kuchangamkia fursa za kibiashara na uwekezaji zilizomo nchini sambamba na kuwashawishi wawekezaji wengine kuwekeza Tanzania.

Akizungumza kwenye kipindi maalumu cha Radio Kilimanjaro nchini Marekani juu ya uwekezaji wa Diaspora Tanzania, Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Godwill Wanga, amewataka Watanzania waishio ughaibuni kuelewa kwamba mazingira ya biashara na uwekezaji yameboreshwa sana,  na kuwataka waje Tanzania  kuwekeza.

“Wakati umefika sasa kwa Watanzania waliopo nje ya nchi kuwa mabalozi wa kutangaza vivutio vya biashara na uwekezaji vilivyomo nchini ili Tanzania ipate wawekezaji wengi  na nchi ipige hatua kimaendeleo na kiuchumi,” alisema Dkt. Wanga

Alisema kuna fursa za biashara na uwekezaji kwenye sekta za utalii, miundombinu, kilimo na biashara na kuwataka wanadiaspora kuchangamkia fursa hizo na kuwekeza katika sekta hizo ili taifa linufaike na uwekezaji huo.

“Ujenzi wa miradi ya kimkakati ya reli ya kisasa(SGR), Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere ni miradi kwa aina fulani  inaohamasisha  uwekezaji kwenye hoteli, vituo vya afya na maeneo ya biashara.  Uwekezaji katika maeneo hayo kutachochea ukuaji wa uchumi wa nchi,” alisema Dkt.Wanga

Ameeleza pia kuwa kuna fursa za uwekezaji kwenye miundombinu ya barabara za mwendokasi, uwekezaji kwenye mifumo ya maji na afya, ujenzi wa maeneo ya biashara katika viwanja vya ndege  na kuwataka washirikiane na Serikali ili waweze kufanya biashara katika mazingira wezeshi.

Alieleza pia fursa ya uwekezaji kwenye viwanda vya kuunganisha simu na vifaa vyake na aina nyingine za viwanda  vya elektroniki na kuongeza kuwa fursa hii inatokana na kuwepo kwa soko kubwa la simu za mkononi Tanzania na nchi nyingine za Afrika.   “Tunawaomba Watanzania waishio nje kutangaza vivutio yetu ili kusaidia kukuza ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa nchi,” alisema Dkt.Wanga

Mwenyekiti wa Tanzania Diaspora Hub (TDH), Bw. Nassor Basalama, alisema wanadiaspora wamejipanga kufanya tathimini  ya mikakati ya  kuwekeza nchini Tanzania.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji jambo ambalo litazidi kutupa nguvu ya kufanya uhamasishaji wa kurudi  Tanzania na  kuwekeza na hata kuvutia wawekezaji wengine kuja kuwekeza nchini,” alisema Bw.Basalama

Alisema TDH imebeba dhamana ya kuhakikisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanarudi kuwekeza nchini ili kukuza uchumi wa nchi na kuzalisha ajira zaidi nchi.

“Tutaendelea kushirikiana na Serikali kupitiaofisi za balozi zetu ili kuendeleza juhudi za kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji kuwekeza nchini Tanzania,” aliaahidi  Bw.Basalama.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw  Francis Nanai, amesema TPSF ndio kiungo kati ya wafanyabiashara na serikali na kuhimiza  ushirikianao kati ya wanadiaspora  na TPSF ambao amesema utuchochea uwekezaji zaidi nchini na nchi kupata maendeleo.

“Wanadiaspora ni sehemu ya sekta binafsi na tayari TPSF imeandaa utaratibu maalum ambao utawawezesha wenzetu kupata taarifa zote muhimu juu ya biashara na uwekezaji ili kuleta urahisi wa wao kutambua fursa zilizopo na kuja kuwekeza,” alisema Bw.Nanai

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...