Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV


MWEKEZAJI na Mwanahisa wa Klabu ya Simba SC, Mohammed Dewji (MO Dewji) ametangaza kuachia ngazi katika nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi wa Wakurugenzi wa Klabu hiyo badala yake amemtaja Makamu Mwenyekiti, Salim Abdallah (Try Again) kuwa mrithi wake.

MO Dewji ametangaza kuachia nafasi hiyo mapema leo kupitia ukurasa wake rasmi Instagram kwa kuweka kipande kifupi cha video kikimuonesha akitoa kauli hiyo. Amesema amefanya uamuzi huo kutokana na yeye muda mrefu kusafiri nje ya nchi.

 “Makubaliano yaliyofikiwa Septemba 21, 2021 tukikubaliana kuwa Mwenyekiti wa Bodi uwepo wake muda wowote katika kuiongoza Klabu ni muhimu, hivyo kwa makubaliano hayo namteua Salim Abdallah kuanzia sasa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba SC”, amesema MO Dewji.

Pia amesema licha ya kuachia ngazi katika nafasi hiyo ya Mwenyekiti wa Bodi ataendelea kuwa Mwekezaji na Mwanahisa, amesema na kuahidi ataendelea kuipenda Simba SC hadi siku ya kufa kwa muda wote.

“Katika kipindi cha miaka minne nikiwa Mwenyekiti wa Bodi tumefanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na tumepata mafanikio ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara nne na kufanya vizuri katika Michuano ya Kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, natoa Shukran kwa Viongozi wa Simba, Wanachama na Mashabiki”, ameeleza MO Dewji.

Hata hivyo, MO Dewji amesema Salim Abdallah (Try Again) ana uzoefu wa kazi hiyo kutokana na kufanya kazi kwa ushirikiano wakiwa wote kama Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bodi, ameahidi kushirikiana naye katika nafasi hiyo sambamba na Uongozi wote wa Simba SC.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...