Na Mwandishi Wetu, Kibaha
WAHITIMU wa kidato cha nne wa shule ya Sunshine ya Kibaha Mkoa wa Pwani wametia fora kwa namna walivyoweza kuelezea masomo ya baiolojia na uhandisi wa umeme kana kwamba ni wakufunzi waliokwisha kuhitimu kwenye masomo hayo.

Hayo yametokea kwenye mahafali ya 14 ya shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo jana Septemba 25,2021na kuhudhuriwa na wazazi na walezi wa wanafunzi hao.

Mwanafunzi Rogers Titus na wenzake waliweza kuwashangaza wageni kwenye mahafali hayo kwa namna walivyomudu kuelezea moyo wa binadamu unavyofanyakazi na kisha kuufanyia upasuaji.

Kitendo hicho kiliibua shangwe kwa wageni waalikwa kutokana na namna Rogers na wenzake walivyokuwa wakimudu kujielezea kwa ufasaha kwa kutumia lugha ya kingereza kuhusu moyo unavyofanya kazi na kisha kuupasua.

Wanafunzi wengine walionyesha umahiri kwenye masuala ya umeme baada ya kuonyesha namna wanavyoweza kutengeneza umeme kwa kutumia vifaa mbalimbali walivyobuni wenyewe.

Wakati huo huo, Wanafunzi wanaosoma shule za St Anne Marie Academy ikiwemo Sunshine ya Kibaha watakaofiwa na wazazi wao na kushindwa kulipa ada ya hawatafukuzwa shule na badala yake wataendelea na masomo kama kawaida.

Ahadi hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa shule ya Sunshine Jasson Rweikiza kwenye mahafali ya 14 ya shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo Kibaha Mkoa wa Pwani.


Umesema kwa mwaka huu pekee wazazi 93 wamefariki dunia kwasababu mbalimbali na kusababisha baadhi ya wanafunzi kuacha masomo kwa kukosa ada.

" Tumekuwa tukipoteza wazazi wengi na mwezi huu pekee tumepoteza wazazi watatu na hali hii imekuwa ikiathiri sana wanafunzi lakini kuanzia sasa hakuna atakayefiwa ambaye atafukuzwa shule kwa kukosa ada," amesema

" Kama yuko darasa la kwanza ataendelea kusoma mpaka darasa la saba na kama ni sekondari ataendelea mpaka kidato cha nne," amesema Dk. Rweikiza ambaye ni Mbunge wa Bukoba Vijijini CCM.

Dk. Rweikiza amesema katika mpango wa kuinua taaluma shuleni hapo wameandaa zawadi mbalimbali zikiwemo fedha taslimu kwa awatakaofanya vizuri kwenye masomo yao.

Amesema mwanafunzi atakayepata daraja la kwanza atapata sh 600,000 na atakayepata daraja la II atapata Sh 200,000 na kwamba lengo ni kuhakikisha hakuna daraja la nne wala daraja la tatu shuleni hapo.

Kwa upande wake, Mkuu wa shule ya Sunshine, Frank Raphael amesema wahitimu hao wameandaliwa vizuri kitaaluma na wanatarajiwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao.

Amesema wanafunzi hao wamewezeshwa kufikia hapo na walimu wenye taaluma na uzoefu wa kutosha huku akimshukuru Mkurugenzi wa shule hizo, Dk. Rweikiza kwa kuendelea kufanya maboresho.

Amesema Dk. Rweikiza amewawezesha kupata maabara iliyosheheni vifaa vya kutosha, vifaa vya kufundishia kama vitabu, projekta, mashine ya kudurufia, maji safi, ulinzi na huduma bora za afya.
Mhitimu wa kidato cha nne wa shule ya Sunshine ya Kibaha Mkoa wa Pwani, Titus Rogers akionyesha umahiri wa kuelezea moyo wa binadamu unavyofanyakazi wakati wa mahalai ya 14 ya shule hiyo yaliyofanyika Jumamosi mkoani humo.
Wanafunzi wa kidato cha nne wa shule ya sekondari ya Sunshine ya Kibaha Mkoa wa Pwani wakielezea namna mfumo wa umeme wa solar unavyofanya kazi wakati wa mahafali yao yaliyofanyika Jumamosi mkoani hapo.
Wahitimu wa kidato cha nne wa shule ya sekondari ya Sunshine ya Kibaha Mkoa wa Pwani wakiserebuka na mwalimu wao mkuu, Francis Raphael wakati wa mahafali ya kidato cha nne Jumamosi shuleni hapo.
Mkurugenzi wa shule za St Anne Marie Academy zinazomiliki shule hiyo ya Sunshine ya Kibaha akilishwa keki na mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo kwenye mahafali yaliyofanyika Jumamosi shuleni hapo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...