Watoto wa Chekechekea wanavyokuwa makini darasani wakiwa katika hali ya kushiba. 

Siku ya Chakula Duniani (World Food Day) kila ifikapo Oktoba  kila mwaka.


Na Abby Nkungu, Singida


ZAIDI ya asilimia 90 ya shule za Msingi za Serikali Manispaa ya Singida hazitoi chakula cha mchana kwa wanafunzi wake hali inayoathiri usikivu, umakini, uelewa na ufaulu hasa kwa watoto chini ya miaka minane ambao bado wanahitaji lishe bora kwa ajili ya ukuaji ubongo ili waweze kufanya  vyema darasani.

Taarifa ya Ofisa elimu Msingi  Manispaa ya Singida, Eugene Shayo inaonesha kuwa kati ya shule 50 za Serikali, nne tu zinazotoa chakula kwa wanafunzi wake wakati kwa binafsi shule zote 16 zinatoa huduma hiyo.

Taarifa hiyo imekuja wakati Tanzania ikiungana na nchi nyingine duniani kote kuadhimisha Siku ya chakula Duniani ambayo hufanyika kila mwaka Oktoba 16, ambapo kwa mwaka huu ilifanyika Kitaifa mkoani Kilimanjaro kauli mbiu ikiwa ni “Uzalishaji na mazingira endelevu kwa lishe na maisha bora”

Hata hivyo, kwa Manispaa ya Singida hakuna matumaini mema juu ya mustakabali wa wanafunzi wa shule za msingi kutokana na kutopata chakula shuleni hivyo kuathiri kiwango cha taaluma.

“Sababu ya shule nyingi za Serikali kutowapatia chakula wanafunzi ni wazazi kukataa kuchangia wakati hizo nne zinatoa chakula kwa sababu zina wanafunzi wenye mahitaji maalum; hivyo Serikali hubeba mzigo huo”  alisema Shayo na  kuongeza  kuwa  shule binafsi ni lazima zitoe chakula kwa kuwa Wazazi wanalipa ada.

Alikiri kuwa kiwango cha ufaulu darasani kwa Wanafunzi wanaopata chakula cha mchana ni kizuri zaidi ikilinganishwa na wale wasiopata chakula.

“Kwa ujumla, mitihani ya kuhitimu darasa la saba  ni kielelezo tosha kwani wanafunzi kutoka shule binafsi wanafanya vizuri kuliko shule za Serikali; ingawa pia kuna sababu nyingine zinazochangia” alisema.

Mmoja wa walimu wanaofundisha chekechea ambaye hakupenda jina lake litajwe anasema hali ni mbaya zaidi kwa wanafunzi wadogo walio chini ya miaka minane ambao licha ya kuwahi kutoka shuleni, mara nyingi ikifika saa 4:00 tu asubuhi huwa wanaanza kusinzia kwa njaa na uchovu hivyo kukosa usikivu.

“Kwa hivi vitoto vya chekechea vilivyopo shule za Serikali hali ndio mbaya zaidi kwani ikifika mchana utavihurumia; vyote utakuta vinasinzia na kupiga miayo  kwa njaa na uchovu” alisema na kuongeza kuwa  kuna haja kwa Serikali kuchukua hatua katika suala hilo  ili watoto wote wapate lishe  shuleni.

Mmoja wa wazazi, Hatibu Ismail mkazi wa Ipembe Singida mjini  alisema kuwa tatizo sio  wao kugoma kuchangia bali  viongozi na watendaji kushindwa kutimiza vyema  wajibu wao wa kuhamasisha juu ya  umuhimu wa suala hilo kwa maendeleo ya mwanafunzi shuleni.

Mtaalamu wa lishe Mkoa wa Singida, Teda Sinde alisema kuwa ulaji duni au ulaji usiozingatia makundi matano ya chakula huathiri ukuaji wa ubongo hivyo kusababisha mtu kutokufundishika kirahisi na kuwa mzito kwenye kufikiria na kutoa uamuzi, pia husababisha upungufu wa damu mwilini.

Alisema  kuwa lishe duni kadhalika huathiri mfumo wa kinga ya mwili katika  kupambana na magonjwa, mtoto kupata utapiamlo na magonjwa mengine hivyo kuweza kusababisha vifo.

Takwimu za utafiti wa Kitaifa za mwaka 2018 juu ya hali ya lishe mkoani Singida zinaonesha kuwa asilimia 29.8 ya watoto walio chini ya miaka mitano wana udumavu, asilimia 5 ukondefu na asilimia 15 wana uzito mdogo.

Aidha, utafiti huo unabainisha kuwa asilimia 27.9 tu ya watoto hao ndio walionyonyeshwa maziwa ya mama kwa kipindi cha miaka miwili kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya na asilimia 3 tu ya watoto walio chini ya miaka miwili ndio angalau hupata mlo unaokubalika katika tafsiri ya lishe bora. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...