Ukuaji wa maendeleo ya Nchi Kiuchumi unachangia changamoto mbalimbali katika Mazingira kama, mabadiliko ya tabia ya Nchi, kelele na mitetemo na changamoto nyingine zinazohatarisha Mazingira.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mh.Hamad Hassan Chande, wakati akifungua Warsha kwa Wamiliki wa Kumbi za Starehe, Bendi za Muziki , Baa na Wadau wa Muziki. Warsha hiyo imefanyika katika ukumbi wa Kisenga Millenium Tower jijini Dar es Salaam na imeandaliwa na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Alisema kwa sababu ya Changamoto hizo ameona ni vizuri kukutana na wadau hao ili wapatiwe elimu kuhusu kelele na mitetemo ili kulinda na kuokoa Mazingira na afya ya vizazi vilivyopo na vijavyo.
“ tumeona kuna umuhimu mkubwa wa kukutana pamoja ili kutoa elimu kuhusu kelele na mitetemo ili kulinda Mazingira na afya ya vizazi vyetu vya sasa na vijavyo”. Amesema Mhe.Chande
Aidha ameongeza kuwa kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la kelele na mitetemo katika maeneo yanayozunguka jamii zinazotokana na shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
“Tafiti mbalimbali Duniani na hapa nchini zimefanyika zinaonyesha kwa sasa kelele na mitetemo ni changamoto kubwa inayokuja kuathiri afya za Wananchi wetu. Mfano, Shirika la Afya Duniani(WHO) limebainisha keleleni ni kisababishi cha madhara katika Maisha ya binadamu. Aidha, “European Environmental Agency” katika ripoti yao ya mwaka 2018 imeonyesha kuwa kelele inachangia vifo vya mapema vya Watoto, Watoto takribani 12000 kila mwaka hufariki katika Bara la Ulaya”.
Alitanabaisha kuwa hapa Nchini pia kuna tafiti zinaendelea
na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) wameanza
jitihada hizo katika Kanda mbalimbali, Mfano NEMC Kanda ya Kaskazini wamefanya
tafiti ndogo kuhusu kelele na mitetemo katika Mkoa wa Arusha, tafiti hii
imeonyesha kuwa kelele na mitetemo imekuwa changamoto kubwa katika jamii.
Wananchi wengi wameonyesha kuathirika moja kwa moja na athari za kelele na
mitetemo. Katika tafiti hii, maeneo yaliyo ongoza kwa kusababisha kelele
chafuzi ni maeneo ya starehe kwa 33% na Viwanda 24
%.
Amezitaja baadhi ya athari za kelele na mitetemo kwa jamii zetu ni kama: kuathirika kwa akili na kusababisha wasiwasi, msongo, hofu, kichefuchefu, maumivu ya kichwa, ubishi, mabadiliko ya hisia kwenye tendo la ndoa “sexual impotence”, Kuharibika kwa utendaji wa kazi na matatizo ya kupoteza kumbukumbu na Usumbufu wa usingizi ambapo hali hii husababisha kuwa na shinikizo la damu, mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida hutokea (haraka au polepole).
Naye Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Muhandisi Samuel Gwamaka, akiongea katika Warsha hiyo amesema kuwa kwa kipindi cha hivi karibuni Baraza limepokea taarifa nyingi za malalamiko kutoka kwa wananchi mbalimbali juu ya matukio yanayohusiana na kelele na mitetemo. Hivyo basi ndiyo maana Baraza limeamua kuandaa warsha hiyo kwa Wadau hao kuhusiana na kelele na mitetemo.
”Katika kulitafutia ufumbuzi jambo hili kwa kushirikiana na Wizara mbalimbali, kwa pamoja kama serikali tumekubaliana kelele na mitetemo ni janga linalokuja kwa kasi katika jamii yetu. Pamoja na kuwepo Sheria mbalimbali za kisekta, pia tumeandaa Mwongozo wa udhibiti wa uchafuzi wa Mazingira utokanao na Kelele na Mitetemo ambao unaonesha muundo wa wadau wa utekelezaji wa udhibiti kelele na mitetemo”. Alimalizia Dkt Gwamaka.
Mgeni Rasmi ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mh. Hamad Hassan Chande akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wadau wanaomiliki kumbi za Starehe, Wadau wa Muziki, Wamiliki wa Bendi na Wamiliki wa baa katika warsha iliyoandaliwa na NEMC kuhusu sualala kelele na mitetemo kwa Wadau hao.
Sehemu ya Wadau waliohudhuria warsha hiyo inayohusu mitetemo na sauti kwa Wadau mbalimbali wakiwemo Wamiliki wa kumbi za starehe, wamiliki wa Baa, Wamiliki wa Bendi na Wadau wa Muziki jijinI Dar es Salaama iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mgeni Rasmi ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mh. Hamad Hassan Chande akiwa meza kuu pamoja na Mkurugenzi wa Bodi ya NEMC Profesa Esnath Chaggu, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka na Mkurugezi Msaidizi- Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Bi Kemilembe Mutasa wakifuatilia kwa ukaribu mada iliyokua ikiwasilishwa wakati wa warsha ya mitetemo na sauti.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...